📌 Yakoshwa na ETDCO kuongeza ufanisi wa kazi
📌Kapinga asema Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa Nishati safi ya Kupikia
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza kuridhishwa kwake na majukumu yanayotekelezwa na Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake katika kuiimarisha Sekta ya Nishati nchini.
Pongezi hizo zimetolewa baada ya Wizara ya Nishati kupitia Taasisi zake za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Kampuni Tanzu ya TANESCO ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yake kwa Kamati hiyo.
“Naipongeza Serikali kwa namna ambavyo imejipanga katika kusimamia Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ili lengo la asilimia 80 la Watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 liweze kufikiwa.” Amesema Mhe. Mathayo
Aidha, amempongeza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko kwa usimamizi wa Kampuni ya ETDCO ambayo inaendelea kutekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi ambao umefikia asilimia 80 na utakapokamilika utawezesha Mkoa wa Katavi kuunganishwa na gridi ya Taifa.
Mradi mwingine unaotekelezwa na ETDCO ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi wilayani Urambo ambao umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme Urambo na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa michango yao katika kuboresha sekta ya nishati nchini.
” Kuimarika kwa Kampuni hii ya ETDCO ni jitihada za kiongozi wetu Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati katika kuiongezea ufanisi, kampuni hii ili iweze kufanya vizuri.” Amesema Mhe.Kapinga
Ameongeza kuwa Wizara ya nishati itaongeza nguvu katika kusimamia miradi ya umeme ili ikamilike kwa wakati.
Akiongelea kuhusu Nishati Safi ya kupikia, Mhe. Kapinga amesema Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa nishati hiyo na kuongeza kuwa, mbali ya majiko ya gesi kuna majiko ya umeme ambayo yanatumia umeme kidogo na kwamba kinachohitajika sasa ni suala la jamii kubadili fikra.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba amesema Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka kumi na hivi sasa upo hatua za awali za utekelezaji wake.
“Mkakati huu umezinduliwa mwezi wa sita mwaka huu, vitu vingi vipo kwenye hatua za mwanzo tunaendelea na mazungumzo na Mawakala ili kufunga mita kwenye mitungi ya gesi.” Amesema Mha. Mramba