Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imesema imeridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari ya Tanga hasa baada ya maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali bandarini hapo.

Kauli hiyo ya Kamati imetolewa tarehe 13 Machi,2025 na Mwenyekiti wake Mhe. Moshi Kakoso (Mb) baada ya kumaliza ziara yao ya kutembelea na kukagua miradi ya maboresho na miundombinu ya Sekta ya Uchukuzi katika Mkoa wa Tanga.

“Tunatoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Uchukuzi na TPA kwa maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga. Bandari sasa ufanisi unaonekana na mapato yameongezeka, hakika tumeridhishwa”. Amesema Mhe. Kakoso.

Mhe. Kakoso pia amesema kamati yake itaendelea kuisaidia TPA ili kutimiza maono ya Mhe. Rais na kufikia malengo yao na Serikali kwa ujumla.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (Mb) ameishukuru Kamati kwa ziara yao iliyowawezesha kujionea kazi kubwa inayofanywa na Serikali Katika Sekta ya Uchukuzi. Aidha Mhe. Naibu Waziri Kihenzile ameihakikishia Kamati hiyo kuwa maoni, ushauri na maelekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha Mkoa wa Tanga unafunguka zaidi kiuchumi kupitia maboresho yanayoendelea kufanywa Miundombinu ya Uchukuzi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw.Plasduce Mbossa, amesema kukamilika kwa awamu mbili za maboresho ya Bandari ya Tanga kwa gharama ya shilingi Bilioni 429.1 kumekuwa chachu ya maendeleo na ufunguo kwa ushoroba wa Kaskazini.

“Manufaa mtambuka ya Bandari ya Tanga yatapelekea maeneo yanayozunguka bandari kufunguka kiuchumi hivyo ushirikiano na wadau wote ikiwemo Kamati yako Mheshimiwa Mwenyekiti ni muhimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa”. Amesema Bw. Mbossa.

Pia Bw. Mbossa ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa TPA ili Mamlaka iweze kutekeleza mipango ya kuboresha miundombinu ya Bandari na kuwa chachu ya Maendeleo ya Uchumi wa Taifa. Aidha amesema TPA inathamini ushirikiano inaoupata kutoka Serikalini, Bunge na Wadau wote wa Sekta ya Bandari na itaendelea kusimamia bandari ya Tanga ili iendelee kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.