Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Selemani Moshi Kakoso, imefanya ziara katika ofisi za Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kukagua shughuli za taasisi hiyo, ikiwemo mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ubunifu cha TEHAMA cha Upanga, Dar es Salaam.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kakoso aliipongeza Serikali na Tume ya TEHAMA kwa hatua ya ujenzi wa kituo hicho pamoja na uanzishaji wa vituo vingine vinane vya ubunifu wa TEHAMA vinavyoendelea kujengwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Aidha, Kamati imepongeza kuanzishwa kwa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI) kinachotarajiwa kujengwa Dodoma, ambacho kitatoa fursa kwa vijana wengi kupata mafunzo bila kujali kiwango chao cha elimu au kuwa na vyeti rasmi huku akisisitiza kuwa, wataalamu wa TEHAMA watahitajika sana nchini hivyo lazima waandaliwe vyema ili kusukuma mbele juhudi za Serikali za kutaka kuufikia kwa kasi uchumi wa kidigitali.
Ili kufikia malengo hayo, kamati hiyo imeshauri vijana wabunifu kuendelezwa na kulindwa katika bunifu zao, akitolea mfano kuwa, wapo vijana waliowahi kubuni vitu mbalimbali ikiwa mitambo ya kufua umeme, helikopta na kadhalika, lakini waliishia katika changamoto zilizowakatisha tamaa.
“Nchi inahitaji wataalamu wa kila aina. Wenye ubunifu waendelezwe na bunifu zao zilindwe,” alisema akiwasisitiza vijana kuchangamkia fursa za uwepo wa vituo hivyo vitakavyotoa fursa mbalimbali kwa vijana ili waweze kujikita zaidfi katika fani zao bila ya malipo, lkini Serikali itawapa fursa ya kujifunza zaidi, kutumia maeneo ya vituo kama ofisi zao na pia furs ana kupikwa kibiashara, kisheria na kadhalika waweze kumudu kujiajiri na kusimamia shughuli zao.

Kamati hiyo pia ilishauri kuandaliwa kwa Sera na Sheria zitakazowalinda wabunifu wa TEHAMA, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na changamoto za wabunifu wengi kushindwa kufanikisha bunifu zao au hata kuzuiliwa kuziendeleza.
Kakoso aliongeza kuwa Tanzania inalenga kuwa jamii isiyotegemea fedha taslimu (cashless society), hivyo kuna haja ya kuwa na wabunifu wengi wa TEHAMA watakaobuni mifumo ya kidijitali inayohitajika.
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi, alisisitiza kuwa wizara yake inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha bunifu za vijana zinakuwa na tija.
“Vijana wengi wa Tanzania ni wabunifu na wamekuwa wakitengeneza bunifu mbalimbali, lakini wamekuwa wakifanya kazi kiholela. Sasa tunakwenda kurasimisha bunifu zao ili ziwe halali na ziwe na manufaa,” alisema Naibu Waziri Mahundi.
Kituo Kikuu cha Ubunifu cha Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU – International Telecommunication Union), kilichopo jijini Dar es Salaam, ni moja kati ya vituo 17 duniani vilivyoanzishwa kwa lengo la kukuza na kuunganisha wabunifu wa kidijitali duniani kote.

Akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, alisema kuwa tume hiyo inaendelea kutekeleza ujenzi wa Kituo Kikuu cha Ubunifu cha TEHAMA jijini Dar es Salaam, huku fedha zikiwa zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa jengo lililopo Upanga.
Dkt. Mwasaga alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusisha ukarabati wa jengo kuu, na unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku awamu ya pili ikihusisha ukarabati wa majengo ya nyuma, inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania Project – DTP).
“Lengo mahususi la kutekeleza mradi huu ni kuchochea mabadiliko ya kidijitali kwa kutumia mbinu ya kipekee ya ekosistimu na kuimarisha uwezo wa kuendeleza ubunifu, ujasiriamali, na ukuaji wa uchumi wa kidijitali,” alisema Dkt. Mwasaga.