Mara kwa mara Bunge linapounda kamati teule na ripoti yake kusomwa bungeni, zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani kwa watendaji mbalimbali.
Mwaka 2008, Waziri Mkuu, Edward Ngoyai Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya Kamati Teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond kumgusa.
Mwaka jana Bunge liliunda Kamati Teule kuchunguza matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa kuchangisha Sh milioni 50 kufanikisha upitishwaji wa bajeti.
Matokeo ya ripoti hiyo yanadaiwa kuchangia Rais Kikwete kufumua Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa, kuwabadilisha na kuwateua wengine.
Hatua hiyo pia ilisababisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, David Jairo, kuondolewa katika wadhifa huo.
Kutokana na hatua ya Bunge kuunda kamati teule ili kuchunguza baada ya malalamiko kadhaa, mwaziri wanaotakiwa kuchunguzwa na kamati hizo ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Majibu yatakayotolewa na kamati hizo ndiyo yatakayoamua ama mawaziri hao kuendelea kushika nyadhifa zao ama kuziachia.
Hakika nyadhifa zao ziko shakani baada ya wabunge kuwatuhumu kushindwa kuwajibika ipasavyo na kusababisha migogoro ya wafugaji na wakulima.
Bunge pia limeamua kuunda kamati teule kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imesababisha vifo, ukiukwaji wa haki za binadamu na upotevu mali.
Operesheni ya kupambana na ujangili iliyopewa jina la ‘Tokomeza’ na ile ya kuwaondoa wafugaji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini, Bunge limeamua kazi hiyo ifanywe na Kamati ya Kudumu ya Maliasili na utalii.
Kamati hiyo itapita na kuwahoji wananchi mbalimbali kuhusu ukatili uliofanywa na kikosi kazi. Wasiwasi wa kuondolewa madarakani kwa mawaziri hao unatokana wabunge kupinga operesheni zinazoongozwa na Serikali.
Dalili mbaya kwa viongozi hao zilianza kuonekana baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutangaza kuwa amekubali hoja za wabunge wawili waliotaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili jambo la dharura.
Iwapo wataondolewa katika nyadhifa zao, mawaziri hao watarusha lawama kwa Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, aliyelitaka Bunge lijadili kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na Mbunge wa Mwibala, Kangi Lugola, aliyetaka Bunge lijadili vitendo vinavyofanywa na watendaji katika ‘Operesheni Tokomeza’.
Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi ng’ombe waliowakamata kwenye kazi hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo David, kuelezea ‘Operesheni Tokomeza’ na migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza operesheni hiyo inavyofanyika, ambapo alisema inalenga kutokomeza ujangili ulioshamiri hapa nchini kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.
Hata hivyo, Kagasheki amesema kutokana na malalamiko ya watu mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo, Serikali imeamua kuisitisha ili kufanya tathmini.
Waziri huyo pia amesema mifugo yote iliyokamatwa ndani ya hifadhi kabla na baada ya jambo hilo iachiliwe bila gharama yoyote na watu wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi wawasilishe vielelezo ili achukue hatua zaidi.
Mara baada ya Kagasheki kumaliza kutoa taarifa hiyo, Waziri Mathayo alitoa taarifa kuhusu migogoro kati ya wafugaji na wakulima, ambapo aliwaomba radhi waliopata hasara ya kujeruhiwa, kupoteza mifugo au vifo katika operesheni za kukamata mifugo.
Wabunge wakacharuka
Mara baada ya mawaziri hao kumaliza kutoa taarifa zao, Spika Makinda alitoa fursa kwa wabunge kuchangia. Mbunge wa Kilolo, Prof Peter Msolla (CCM), alitoa hoja ya Bunge liunde kamati teule kuchunguza migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amesema anashangazwa na mawaziri Nchimbi, Vuai, Kagasheki, Mathayo kuendelea kuongoza wizara wakati damu za wananchi waliofariki katika operesheni zinazohusisha wizara wanazoziongoza zinawakabili.
Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM), aliifananisha Serikali na ugonjwa wa sotoka ambao miaka ya nyuma ulikuwa ukiua ng’ombe wengi.
“Hii Serikali ya ajabu sana, yaani ukiwa na mifugo mingi ni kero kwao badala ya kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi, mimi naifananisha na sotoka,” amesema.
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), aliwataka wabunge wa CCM waache unafiki na wamuondoe Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kuwa hachukui hatua kila anapopelekewa matatizo.
“Wewe Waziri Mkuu taarifa kiintelijensia hazikufikii? Je, husomi magazeti ujue kinachotokea kwenye maeneo mbalimbali na mbona huchukui hatua, nyinyi watu wa CCM msileane,” amesema.
Mbunge wa Viti Maalum, Pauline Gezul (Chadema), amemtaka Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi mawaziri wake waliosababisha operesheni za kikati zilizosababisha vifo vya binadamu, mifugo na unyanyasaji.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), amesema Serikali inatia aibu kwa kusikia inakamata pembe za ndovu lakini inashindwa kuwakamata majangili waliohusika.
Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM), aliwataka mawaziri waache porojo za kisiasa wanapoambiwa matatizo ya wananchi na wabunge.
“Wabunge humu ndani tunaeleza matatizo ya wananchi, eti waziri anasema si mambo ya msingi…acheni porojo, fanyeni kazi maana tuna ushahidi wa kile tunachokisema. Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Vullu (CCM) ameitaka Serikali kuhakikisha inafanya kila linalowezekana ili kudhibiti migogoro inayojitokeza kati ya wakulima na wafugaji.
Aidha, mbunge huyo alisema kuna kila sababu ya kuziwezesha halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji kwa lengo kuondoa mapigano ya mara kwa mara.
Vullu alitoa kauli hiyo wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Mipango ili kujadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/15.
Akichangia mpango huo pia alisema kuwa anashangazwa na Serikali kudai kuwa uchumi unakua wakati wakulima na wafugaji wanaendelea kupambana kila kunapokucha.
Amesema kuwa ili kutatua mgogoro huo ni lazima Serikali iziwezeshe halmashauri kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakulima wanatengewa maeneo yao na ya wafugaji ili kuondokana na machafuko ya mara kwa mara.
Mbali na hilo, aliitaka Serikali kuangalia jinsi ya kuisaidia Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuwezesha kiwanda cha saruji kiweze kuendeleza uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Moja ya matukio yanayolalamikiwa
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa Usinge wilayani Kaliua, Kipara Issa, aliuawa baada ya kupigwa kwa muda mrefu na watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa wanaoendesha operesheni ya kusaka silaha haramu na kulinda misitu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Tukio hilo lilifanyika hivi karibuni, ambapo maofisa hao wakiwa katika magari ya operesheni hiyo, waliokuwa wamevalia sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, maofisa Usalama na Maliasili wanadaiwa kufika nyumbani kwa mtu huyo kwa nia ya kutaka kumfanyia upekuzi, baada ya kumshuku anamiliki silaha kinyume cha sheria.
Wakiwa katika upekuzi huo, walikutana mke wa Kipara, Tabu Maganga, ambaye ni askari polisi katika kituo cha Usinge na kuanza kumhoji kuhusu mumewe na shughuli anazozifanya, huku wakidaiwa kumpiga hadi akapoteza fahamu mara kadhaa.
Hali ilivyokuwa
Wakati mke wa Kipara, ambaye ni askari polisi mwenye nambari WP 6985 akiendelea kupata suluba kutoka kwa maofisa hao, waliokuwa na bunduki na rungu, watoto wa umri wa kati ya miaka 13 na 17 waliokutwa nyumbani hapo pamoja na bibi yao, nao walishambuliwa.
Magreth Kajoro, mama wa Kipara (marehemu), akielezea mkasa huo, alisema wakati amekaa nyumbani kwa mwanaye huyo, alishangazwa kuwaona maofisa hao walivyofika na kuanzisha tukio hilo la kinyama, na kwamba alipojaribu kuhoji walianza kumpiga.
“Walinikamata na kuniingiza ndani wakanilazimisha nioneshe silaha ambayo walidai inatumiwa na mtoto wangu, lakini baya zaidi mmoja wao ambaye alikuwa kavaa mavazi ya Jeshi la Wananchi aliniwekea bunduki kichwani huku wakiniambia nisali sala yangu ya mwisho,” alieleza Magreth.
Aliendelea kueleza; “Baada ya muda mfupi nilisikia kishindo kikubwa na baadaye kufuatiwa na kauli ya amri ya kukatazwa kufyatua risasi, ndipo Kipara akafika hapo nyumbani akipigwa huku akiambiwa aoneshe bunduki anayofanyia uhalifu, jambo ambalo lilikuwa ni geni sana kwetu hapo nyumbani.”
Katika upekuzi huo, maofisa hao ambao imedaiwa kuwa walipata taarifa za uhalifu zilizowahusisha watu wanane wa maeneo ya Wilaya ya Kaliua akiwamo Kipara, kwamba mbali ya kumiliki silaha haramu, ilidaiwa alikuwa anamiliki sare za JWTZ ambazo huzitumia kufanyia vitendo vya kihalifu na akizihifadhi ndani ya magunia ya mahindi na mpunga nyumbani kwake.
Askari hao wa operesheni maalum wakati wa kusaka silaha na sare za JWTZ kabla ya kumwadhibu Kipara hadi akafariki dunia, walimwaga unga wa mahindi na mpunga wakiamini kwamba watakuta silaha na sare hizo za jeshi hilo bila mafanikio.
Watoto Said Auma (14), Anthony Gabriel na Said Kalungumya, walijikuta wakipata adhabu kali ya kubebeshwa milango ya nyumba ambayo ilikutwa ndani kwa ajili ya biashara huku wakipigwa hadi kupata majeraha makubwa katika maeneo mbalimbali ya miili.
Hata hivyo, baada ya kutekeleza unyama huo, askari hao wa operesheni hiyo waliamua kuondoka na Kipara, lakini wakati huo alikuwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na kipigo kikali.
“Nilimshuhudia kaka yangu wakati wanamtoa ndani akiwa amelowa damu nyingi baada ya kukosa hiyo silaha waliyokuwa wakiitafuta, wakampakiza kwenye gari wakaondoka naye,” alisema Maneno Issa. Muda mfupi baadaye familia hiyo iliamua kwenda Kituo cha Polisi Usinge kufungua kesi wakiwa na mke wa Kipara, Tabu, ambaye inadaiwa kuwa wakati akipata kipigo alidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo akiamuriwa na maofisa hao wa operesheni kugaragara kwenye maji machafu.
DC Kaliua
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Saveli Maketa, alithibitisha kupata taarifa za tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kufanyika kwa uchunguzi.
Alibainisha kuwa anachokijua kuhusu Kipara aliyeuawa ni kwamba alikuwa mhamiaji haramu na mtuhumiwa wa ujambazi, anayehifadhiwa na mke wake huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Usinge.
“Sasa unafikiri ndugu mwandishi hao maofisa wangeenda kufanya upekuzi hapo nyumbani kwa huyo jambazi bila kufanya kashkash hata kidogo, lazima waende kijeshi kama walivyofanya kwa kuwa tuna taarifa rasmi kuwa anamiliki silaha,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo, hakuzungumzia vitendo vya udhalilisha dhidi ya askari huyo wa kike na kuwapiga watoto na mama mzazi wa Kipara.
Maiti ya Kipara Issa
Baada ya saa kadhaa kupita huku familia ya marehemu Kipara Issa wakishirikiana na baadhi ya wanakijiji cha Usinge, walianza harakati za kumtafuta Kipara kwa kupiga simu na kuuliza kwenye vituo vya Polisi kuhusu tarafa zake wilayani bila mafanikio.
Wakati mdogo wa Kipara, Maneno Issa, akifuatilia huko wilayani Urambo, alipata taarifa kuwa kaka yake amepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Urambo tayari akiwa amekufa, jambo ambalo lilimlazimu afike haraka na kuhakiki maelezo aliyoyapata.
“Niliingia mpaka chumba cha kuhifadhia maiti nikamkuta kweli ni yeye, nikajaribu kumwangalia kwa haraka haraka, lakini kilichoniuma zaidi ni kuona kang’olewa meno na uso wake ulikuwa umevimba mno,” alisema Maneno.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Tabora
Kufuatia tukio hilo ambalo lilikuwa likitafutiwa njia ya kufichwa, hatimaye taarifa zilizagaa hadi zikamfikia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa, na kuamua kufunga safari akiwa na wajumbe wa kamati hiyo kwenda kujiridhisha katika tukio hilo la ukatili.
Ujumbe huo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ulifika na kutoa pole kwa wafiwa na baadaye kuzungumza na wakazi wa Usinge, ambao walitoa kilio chao kuhusu mauaji yaliyofanywa na maofisa hao sambamba na kumdhalilisha askari wa kike na kuwashambulia watoto sita wa familia hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa baada ya kusikiliza kwa makini malalamiko ya wakazi hao dhidi ya unyama waliofanyiwa, kwa niaba ya Serikali aliomba radhi tukio la mauaji hayo huku akieleza kuwa licha ya kuwa operesheni hiyo ni halali, lakini nguvu iliyotumika si halali na hivyo kuahidi kuwa Serikali italishughulikia kwa makini na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, matukio ya mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola katika Wilaya za Urambo na Kaliua yamekuwa yakitishia amani kwa wananchi, hasa wakati wa operesheni hizo za maliasili, ambapo wananchi wamethibitisha kuwa askari wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwadhulumu raia badala ya kutekeleza malengo ya operesheni hizo.
Mei 28, 2011 saa 10 jioni eneo la Usinge ya Kati, askari polisi waliwafyatulia risasi mfululizo wananchi baada ya kukamata ng’ombe 6,301 wao, na katika tukio hilo, Juma Said (21) alipoteza maisha kwa kupigwa risasi mgongoni na wengine wanne kujeruhiwa na hakuna hatua zilizochukuliwa kwa wahusika.
Matukio mengi ya mauaji yanayofanyika kimya kimya katika maeneo hayo yamekuwa yakijenga taswira mbaya na kuonesha kuwa Serikali haichukui hatua, hali ambayo inafanya watu wengi kudhani huenda inabariki uovu huo unaofanywa na taasisi zake