Na Tiganya Vincent,Tabora

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo tarehe 14 Machi, 2023 imekagua Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora ambapo wameonesha kuridhishwa na ukarabati huo na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa Miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake kwa maana ya ujenzi na ukarabati.

Akizungumza mara baada ya ziara ya siku moja ya ukaguzi wa Utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo amesema kuwa Mahakama ni moja ya Taasisi inayofanya vizuri katika miradi yake ya ujenzi na hivyo kuwasihi Watumishi wa Mhimili huo kutoa huduma zinazoendana na uzuri wa miundombinu hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kulia) akiwapitisha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati walipokuwa wakikagua Mradi wa Ukarabati na upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Tabora.

“Kama Kamati tuna ‘oversee’ mambo mbalimbali yanayofanyika Serikalini, hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali unaoendelea ikiwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya majengo, kwakweli mnaupiga mwingi,” amesema Mhe. Kyombo.

Mhe. Kyombo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya utoaji haki kwa wananchi.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kiteto ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Edward Ole Lekaita amesema ubora wa majengo ya Mahakama unaridhisha na kuongeza Mahakama imeitendea haki fedha waliyopewa na Serikali kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukarabati.

Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pindi walipotembelea Mradi wa Ukarabati na upanuzi wa Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Tabora leo tarehe 14 Machi, 2023. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe.  Florent Laurent Kyombo (Mb)

Amesema uboreshaji na ukarabati wa Mahakama hiyo umewawezesha Maafisa wa Mahakama na Wadau wao kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa haki kwa wananchi katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Khadija Shaaban almaarufu Keysha amesema Mahakama imeitendea haki fedha za ukarabati walizopatiwa na Serikali na kushauri kuweka ‘Lift’ maalum kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mradi huo umetumia kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 2.5 na ulianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka 2021 na kukamilika Septemba, 2022.

Amesema kuwa, hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambayo ni sawa ya asilimia 61 na bado anadai milioni 900 ambazo wanaendelea kushughulikia.

Prof. Ole Gabriel, ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kuahidi kuwa watahakikisha kuwa haki inapatikana kwa ubora.

Aidha Mtendaji huyo amewataka Wajumbe wa Kamati hiyo kuisaidia Mahakama kwa kuwaeleza wananchi kuhusu uboreshaji wa huduma mbalimbali za Mahakama unaoendelea ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakati ufunguaji wa mashauri na usikilizaji wa mashauri.

Kamati hiyo inatarajia pia kutembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Mwanza tarehe 16 Machi, 2023.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Florent Laurent Kyombo (Mb) akizungumza jambo baada la wasilisho lililotolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Mwenyekiti huyo amepongeza kazi nzuri ya ukarabati na upanuzi wa jengo wa Mahakama Kuu Tabora ulivyofanyika. Kulia ni Katibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Bw. Frank Nkya.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kushoto) akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kibao cha uzinduzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora pamoja na kuelezea historia jengo hilo ambalo awali lilikuwa likitumika kama
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo alipokuwa ofisini kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwasilisha taarifa ya Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea Mradi huo mapema leo kwa ajili ya ukaguzi.