Kamati Kuu ya Halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeteua wajumbe wapya saba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Akitoa taarifa ya kikao hicho leo Januari 14, 2023, Shaka Hamdu Shaka ambaye alikuwa katibu Mwenezi wa CCM, amesema kikao maalum cha Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema kuwa katika kikao kilichoongozwa na mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan imeteua wajumbe saba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Shaka amewataja wajumbe kutoka Bara kuwa ni Hassan Wakasuvi (mwenyekiti CCM Tabora),Mizengo Pinda (Waziri Mkuu mstaafu), Halima Mamuya ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa umoja wa wanawake Tanzania.
Kwa upande wa Zanzibar amemtaja injinia Nasri Ally naMohamed Abood Mohamed na Leyla Burhan Ngozi akisisitiza kuwa kila upande nafasi mbili zilikuwa za wanaume na nafasi mbili wanawake.
Amesema nafasi ya Katibu Mkuu ameendelea Daniel Chongolo, Naibu Katibu Mkuu Bara Annamringi Macha, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mohemed Said Dimwa.
Amesema nafasi yake ya Katibu Itikadi na Uenezi imechukuliwa na Sophia Edward Mjema, Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha,Dkt. Frank Hawasi, Katibu siasa na uhusiano wa kimataifa Mbarouk Nassoro na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Haji Usi Gavu.
Hata hivyo Shaka ametumia fursa hiyo kuaga rasmi huku akivishukuru vyombo vya habari na Watanzania kwa ujumla.