Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kamati iliyoundwa kuchunguza mfumko wa bei ya mafuta nchini kati ya mwezi Julai, Agosti na Septemba, itatoa taarifa yake Septemba 16, 2021. Kamati hiyo iliundwa Septemba 2, 2021. Katika hili, ninadhani tunakwenda kufanya uchunguzi kwa suala ambalo liko wazi kabisa. Sina uhakika matokeo watakayokutana nayo wanaochunguza watapanguaje utitiri wa kodi na ujanja ujanja uliomo katika sekta ya mafuta.
Sitanii, kuna mambo yanafanywa hauwezi kuamini kama yanafanywa na watu wa nchi hii. Mwezi Mei na Juni, ambapo wenye mamlaka ndani ya Wizara ya Nishati waliwapa zabuni wanaoitwa kampuni za wazawa, ndio walioanza kufumua mshono. Uamuzi huu unaelezwa kuwa unanufaisha mtandao mpana wa vigogo serikalini badala ya wananchi.
Bei za kusafirisha mafuta ya dizeli zimepanda kutoka wastani wa dola 24 (Sh 55,200) kwa tani hadi dola 47 (108,100) kwa tani katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Agosti, 2021.
Bandari ya Tanga usafirishaji umepanda kutoka dola 48 (Sh 110,400) hadi dola 72 (Sh 165,600) kwa mwezi Agosti na inaendelea kupanda. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza bei za mafuta nchini kwa mtumiaji wa kawaida.
Sitanii, ongezeko hilo linamaanisha kuwa kwa mafuta ya dizeli pekee yanayoshushwa kwenye boya namba 1, 2 na 3 kwa mwezi Agosti, 2021, ambayo ni jumla ya tani 268,314 umeongeza gharama ya kuingiza dizeli nchini kwa wastani wa Sh 13,415,700,000. Hizi fedha zinakamuliwa kwa Watanzania kwenda kuwezesha ‘wazawa’, yaani kampuni zilizosajiliwa Tanzania. Hata kwenye petroli na mafuta ya taa nako kumetokea madhara ya bei kwa uamuzi huu.
Kwa mwezi Julai, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda kwa TZS 156/lita, TZS 142/lita na TZS 164/lita, mtawalia.
Kwa mwezi Agosti, 2021 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa TZS 21/lita, TZS 36/lita na TZS 55/lita, mtawalia. Sehemu ya ongezeko hili inatajwa kuwa imetokana na utaratibu mpya wa kutumia waagizaji mafuta wa ndani ambao wanasafirisha mafuta kwa bei juu kuliko kampuni za kimataifa.
Sitanii, Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) inakuwa haina jinsi, isipokuwa kutumia kanuni kukokotoa bei za mafuta, na uamuzi kama huu madhara yake yako wazi. Lakini pia kuna taarifa kuwa kwa mafuta yaliyonunuliwa mwezi Julai katika soko la dunia bei zimeshuka kutoka wastani wa dola 75, hadi dola 65 kwa pipa. Sasa ninajiuliza, hapa kwetu kwa nini bei ipande?
Nafahamu Rais Samia Suluhu Hassan aliibana wizara na kwamba ulianzishwa mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja (PBPA) kwa nia ya kupunguza gharama za usafirishaji, ununuzi na nyingine, hivyo akawataka warejee katika utaratibu wa zamani.
Cha ajabu, kwa meli iliyoleta mafuta wiki ya kwanza ya Septemba, kila tani moja imesafirishwa kwa dola 6 (Sh 13,800) badala ya dola 47 (Sh 108,100) za mwezi Agosti, 2021 kwa dizeli inayoletwa nchini.
Sasa Ninajiuliza, kwa nini Julai na Agosti tulitwishwa mzigo wote huu? Kama wanataka kusaidia wazawa si wawaondolee hizo kodi wanazosema wanalipa?
Lakini je, mbona bei ya kusafirisha mafuta imeshuka ila bado bei ya mafuta inazidi kupanda? Sina uhakika kama kamati inayochunguza itapata kikokotoo cha kodi zinazotozwa.
Sitanii, mafuta yanatozwa kodi kwa tozo za kufuru. Kila lita moja inatozwa tozo/kodi ya ghala (Sh 20.60), kodi ya maendeleo ya reli (17.40), ada ya kuchakata forodha (Sh 4.80), uzito na vipimo (Sh 1), TBS (Sh 1.20), TASAC (Sh 3.50), EWURA (Sh 6.10), kuweka vinasaba (Sh 14.10), adhabu ya kuchelewesha kushusha mafuta (Sh 5.50), gharama za wapimaji (Sh 0.18), gharama za mtaji (Sh 11.60), kuyeyuka/upotevu wa mafuta (Sh 5.80), tozo ya mafuta (Sh 413) na ushuru wa bidhaa (Sh 379).
Si kodi na tozo hizo pekee, bali pia zipo ada (Sh 100), kampuni za mafuta (Sh 123), wakala za serikali (Sh 1), ushuru wa huduma unaolipwa na wauzaji wa jumla kwa mamlaka za serikali za mitaa (Sh 5.70), faida ya muuzaji wa rejareja (Sh 108), malipo yanayolipwa na wauzaji wa rejareja kwa wakala za serikali (Sh 5.44), usafirishaji wa ndani (Sh 10) na ushuru wa huduma unaolipwa na wauzaji wa rejareja kwa mamlaka za serikali za mitaa (Sh 6.10). Jumla ya kodi/tozo hizi ni Sh 1,243.02 kwa kila lita ya mafuta inayouzwa nchini.
Sitanii, kabla ya kodi mafuta yamefika bandarini Dar es Salaam kwa gharama ya Sh 1,162. Bado na gharama hizi zingeweza kushuka zaidi iwapo zabuni za waagizaji wa jumla zingewabana kuendana na soko la dunia na bei halisi za usafirishaji. Mimi na wewe tujiulize, je, kwa kodi hizi ambazo ukiunganisha na bei ya kuagiza mafuta lita ikiwa Dar es Salaam inakuwa Sh 2,405.02 wauzaji wa rejareja wanaweza kupunguza bei za mafuta kweli?
Ukizipitia kwa umakini kodi hizi, utaona kuna taasisi nyingine zinafanya kazi ileile kwa kulipwa mara mbili. Hivi huu utitiri wa mikono katika mafuta hatuwezi kuwa na chombo kimoja ambacho kitafanya angalau asilimia 60 ya kazi hizi, tukawa na chombo cha pili kama EWURA watakaodhibiti bei na ubora maisha yakaendelea?
Ni wazi kama tusingekuwa na EWURA kwa mchezo huu unavyokwenda, lita moja ingekwisha kuuzwa Sh 5,000. Siamini kama tumesahau yaliyopata kutokea siku za nyuma. Kamati iliyoundwa ninaamini itatuletea majibu kuhusu utitiri huu wa kodi/tozo ili tujue tunatokaje hapa tulipo. Mungu ibariki Tanzania.