Utetezi uliofanywa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Bandari, SACP Robert Mayala, dhidi ya polisi anayetuhumiwa kuiba kofia ngumu ya pikipiki bandarini, umemponza.
Mayapa alijitokeza kumtetea PC Stephen Shawa, anayetuhumiwa kujihusisha na wizi huo licha ya kamera za usalama kurekodi tukio lote.
Siku moja baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika kuhusu wizi huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro amemwondoa SACP Mayala.
Taarifa ambazo JAMHURI limezipata zinasema SACP Mayala amepelekwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar. Nafasi yake imekaimiwa na aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Kikosi cha Bandari, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Theresia Nyangasa.
Kwenye taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa kwa vyombo vya habari Oktoba 9, mwaka huu imeeleza kuwa uhamisho huu ni wa kawaida kwa ajili ya kuongeza ufanisi na utendaji kazi.
Wiki iliyopita JAMHURI liliandikia habari za PC Stephen kuiba kofia ya pikipiki ya mteja bila kujua kuwa tukio hilo lilikuwa limenaswa kwenye mfumo wa kamera za usalama zinazoonesha picha na sauti.
Agosti 8, mwaka huu saa 05:40:28 asubuhi, PC Stephen aliingia sehemu ya wazi kunakoegeshwa pikipiki na kutoweka na kofia ngumu ya mteja.
Mteja alilalamika na ndipo uchunguzi wa tukio hilo ulipofanyika kupitia kamera za usalama na kubaini aliyehusika ni PC Stephen.
“Mteja akalalamika kuwa imekuwaje kofia yake ipotee wakati ameiacha kwenye pikipiki. Kwa kweli alileta tafrani kubwa. DG Kakoko [Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Mhandisi Deusdedit Kakoko] aliingilia kati, IGP (Simon Sirro) alijulishwa akaja hapa,” kimesema chanzo chetu.
Mhandisi Kakoko alikiri kutokea kwa tukio hilo: “Ni kweli huyu askari aliiba kofia ya pikipiki, lakini kwa mfumo wa CCTV tulizonazo tukamnasa vizuri tu.”
JAMHURI lilipozungumza na SACP Mayala kuhusu tukio hilo alikanusha askari huyo kuiba kofia, na kudai kwamba aliiazima tu baada ya kuombwa na mwenzake ampeleke Kariakoo.
“Hapa kwetu kuna eneo ambalo polisi huwa wanaegesha pikipiki zao, sasa yeye alichukua ile ‘helmet’, akijua anakwenda mara moja na kurudi.