Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk. Diodorus Kamala, ameomba Kampuni ya Petra Diamonds ya nchini humo kuongeza uzalishaji na ubora wa almasi inayozalishwa hapa Tanzania.

Kampuni ya Petra Diamonds inauza almasi inayochimbwa nchini Tanzania.

 

Dk. Kamala aliyasema hayo hivi karibuni, alipotembelea kampuni hiyo katika soko la almasi la Antiwerpen nchini Ubelgiji, na kusema kuwa yapo mambo muhimu ya kujifunza kutoka Uholanzi katika uendelezaji na usimamiaji wa sekta ya gesi.

 

Meneja wa Masoko wa Petra Diamonds, Jeschie Widawski, alimweleza Balozi Kamala kwamba kwa mwaka kampuni yake inauza wastani wa carat 20,000 za almasi zenye thamani ya dola milioni 45 za Marekani.

 

Kadhalika, Widawski alisema Kampuni ya Petra Diamonds baada ya kununua Mgodi wa Almasi wa Mwadui, iliwekeza dola milioni 45 za Marekani na kuongeza kuwa imefanikiwa kuongeza ubora wa almasi inayozalishwa na hivyo kuongeza bei kutoka wastani wa dola 90 hadi dola 250 za Marekani kwa carat.

 

Uholanzi walipongundua gesi mara ya kwanza katika eneo la Groningen, ilikadiriwa kwamba kulikuwa na gesi yenye ujazo wa 2 TCF. Eneo hilo hilo baada ya kuanza kuvuna gesi ilibainika lilikuwa na gesi yenye ujazo wa 99 TCF.

 

Kwa sababu hiyo, kiwango cha 43 TCF ambacho kinatajwa kwamba ndicho kimeishagundulika hapa Tanzania, kuna uwezekano mkubwa baada ya kuanza kuvuna kiwango hicho kuongezeka hadi 15,000 TCF ukizingatia uzoefu wa Uholanzi.

 

Takwimu zinaonesha kuwa Serikali ya Uholanzi inapata asilimia 85 ya mapato yote yanayotokana na biashara ya gesi.

 

“Kwa sababu hiyo, Tanzania lazima tujipange ili tuhakikishe Serikali inapata mapato ambayo hayatapishana sana na Serikali ya Uholanzi inavyopata mapato kutoka kwenye gesi,” alisema Dk. Kamala.

 

Balozi Kamala pia alisema kuwa amejifunza kutoka Serikali ya Uholanzi kwamba Serikali inamiliki kwa asilimia zaidi ya 90 miundombinu na biashara ya gesi kwa kutumia kampuni za Serikali kama vile Gusuine, GasTera na EBN.

 

Alisema Serikali ya Uholanzi ina sera mbili zinazoongoza sekta ya gesi ambazo ni sera ya visima vikubwa na sera ya visima vidogo, inayotoa fursa ya uwekezaji na uchimbaji wa gesi katika visima vidogo.

 

Balozi Kamala alimshukuru Edward Rweyememu wa TANSORT anayefuatilia kwa karibu uuzwaji wa almasi ya Tanzania katika soko la almasi la Antiwerpen.

 

Alimweleza kwamba yeye ni jicho la Tanzania na hivyo lazima awe mzalendo na ahakikishe Tanzania inapata mapato yanayotarajiwa kutokana na uuzaji wa almasi kwa kutumia utaratibu wa zabuni.

 

Dk. Kamala alitoa wito kwa wataalamu wa sekta ya madini kuwa wazalendo na wajue Taifa liliwasomesha kwa fedha nyingi, ili walisaidie na siku zote waepuke kulipwa na mtu yeyote kwa nia ya kutaka kutoelewa au kuacha kusimamia rasilimali za Taifa kwa umakini.