Rais Jakaya Kikwete, anatibiwa nchini Marekani. Walimwengu wametangaziwa kwamba Rais wetu amefanyiwa upasuaji wa Tezi Dume. Naungana na wote wanaomtakia siha njema ili hatimaye arejee nchini salama.

Niipongeze Ikulu kwa kuwapa Watanzania habari zinazohusu afya ya Kiongozi wetu Mkuu. Hili ni jambo jema. Wameondoa kitendawili kinachowasumbua wananchi wa Zambia. Hao wenzetu hadi leo hawajui nini kimemuua Rais wao, Michael Sata.

Ikulu yetu imerejea kile kilichofanywa wakati wa Awamu ya Tatu ambako Rais Benjamin Mkapa alikaa kwa wiki kadhaa hospitalini nje ya nchi akisumbuliwa na baridi yabisi. Tunatambua kuwa ugonjwa ni siri ya mgonjwa na walio karibu naye, lakini kwa upekee wa rais, na kwa kuzingatia kuwa huyu ni kiongozi wa watu zaidi ya milioni 45, ni jambo jema kuujulisha umma kama walivyofanya.

Niliposikia Rais Kikwete anaumwa Tezi Dume, nikajaribu kuzungumza na madaktari -marafiki zangu. Jibu nililopewa na wote ni kwamba ugonjwa huo unatibika hapa nchini. Upasuaji wake, kwa gharama za Serikali ni Sh 250,000. Katika hospitali binafsi, gharama yake inasemekana ni Sh 400,000 hadi Sh 600,000. Wakatoa mfano wa Hospitali ya Tumaini, Dar es Salaam ambako upasuaji huo unafanywa.

Nikajiridhisha kwamba kumbe upasuaji huo unawezekana hapa hapa nchini. Kama hivyo ndivyo, iweje Rais Kikwete atibiwe Marekani? Mimi namtetea kwa hilo. Namtetea kwa sababu aliondoka nchini kwenda kuchunguzwa afya yake. Hatukuambiwa anakwenda kufanyiwa upasuaji wa Tezi Dume. Ni rahisi kuamini au kuaminishwa kuwa ugonjwa huo umejulikana baada ya kupimwa afya yake nchini Marekani. Kwa maneno mengine, Tezi Dume ni matokeo ya kupimwa kwake huko ughaibuni. Ni kwa sababu hiyo, hata kama huko Marekani gharama za upasuaji ni ghali, asingeweza kurejea nchini kwenye bei nafuu akafanyiwa upasuaji. Kilichofanywa ni kulimaliza tatizo huko huko baada ya kulibaini. Kama hivyo ndivyo, hapo hakuna mjadala.

Lakini kama kweli alikwenda akijua kinachomsumbua ni Tezi Dume ambayo upasuaji wake unaweza kufanywa hata hapo Kibaha, wananchi wana haki ya kuhoji!

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifia Uingereza alikopelekwa kwa matibabu. Rais Sata, naye kaaga dunia nchini Uingereza akipata matibabu. Mlolongo wa viongozi na watu mashuhuri wa Tanzania na Afrika wanaofia ughaibuni walikofuata tiba ni ndefu mno. Lakini mtu mmoja mashuhuri sana-Mzee Nelson Mandela-yeye kazaliwa na kufia katika ardhi yake ya asili. Mandela hakupelekwa Ulaya, Marekani wala Asia kutafuta matibabu. Alitibiwa nchini mwake kwa sababu yeye na waliomsimamia waliamini nchi yao ina uwezo wa kitabibu ambao kama ingeshindwa, basi huko kwingine wasingeweza.

Mzee Mandela alitibiwa katika hospitali za nchini mwake kwa sababu zina viwango. Kuna watu walifanya kazi kubwa ya kuboresha ngazi zote za huduma za afya nchini humo. Mwenyekiti wetu wa Jukwaa la Wahariri aliposhambuliwa na majahili hata akaumizwa, alipelekwa kupata matibabu katika hospitali hiyo hiyo ya Milpark iliyotumiwa na Mzee Mandela.

Nini ninachojaribu kukisema hapa? Wakati tukiomba Rais wetu apone haraka, tuna wajibu wa kujiuliza tabia hii ya viongozi wetu kwenda kutibiwa ughaibuni hata baada ya miaka zaidi ya 50 ya Uhuru. Lini itafikia tamati? Mwalimu Nyerere alipelekwa Uingereza kwa sababu Hospitali ya Bugando ambayo ipo kilometa 200 na ushei hivi kutoka Butiama; haina vifaa tiba wala dawa.

Mzee Mkapa aliishi miezi kadhaa nje ya nchi akitibiwa kwa sababu hapa nchini hakuna hospitali ambayo ingeweza kumtibu! Rais Kikwete yuko Marekani kwa sababu Muhimbili anayosema imeboreshwa, imeboreshwa kwa maneno; lakini katika uhalisia hakuna vifaa wala dawa. Au basi, kama kweli kuna vifaa tiba na wataalamu, basi atuambie kuwa hataki kutibiwa hapo kwa sababu gani? Je, haamini ujuzi na weledi wa madaktari na wauguzi wetu?

Utaratibu huu wa viongozi wetu kwenda kutibiwa nje kila wanapougua ukiachwa uendelee, maana yake ni kwamba itakuwa ndoto kuona zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu zikiboreshwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa hali na aina zote.

Hapa izingatiwe kuwa Rais Kikwete yeye anatibiwa kwenye hospitali yenye sifa zote za kutumiwa na binadamu, huku akiiacha Muhimbili na wagonjwa wa figo wakikosa Sh 60,000 za kununulia dawa! Anakwenda ughaibuni kutibiwa ilhali maelfu kwa maelfu ya wananchi wakikosa tiba Muhimbili kwa sababu msambazaji dawa (MSD) amekwama kutokana na deni la Sh bilioni 100 hivi.

Ni katika nchi hii pekee, na pengine katika nchi zenye viongozi wa aina ya Tanzania ambako Hospitali ya Taifa inakosa kipimo cha CT Scan, lakini Hospitali ya Regency inakuwa nacho kwa saa zote 24! Ni Tanzania ambako unaweza kukosa kipimo cha X-ray katika Hospitali ya Taifa, lakini ukakipata katika hospitali iliyo Mwananyama au Kigogo uchochoroni kabisa!

Wakati Rais wetu yeye akipata wasaa wa kupokea na kujibu sms za Watanzania na walimwengu wengine akiwa hospitalini, sisi wagonjwa wetu makabwela wanalala sakafuni kwa sababu hawawezi kugharimia malipo ya vyumba vizuri. Hawana salio kwenye simu zao. Wajawazito wanalala wawili wawili (mzungu wa nne) kabla na hata baada ya kujifungua.

Rais hawezi kuwa na furaha moyoni kama anatibiwa ndani ya majengo mazuri huku mamia ya wagonjwa saratani wakiingia Ocean Road na kukosa tiba kwa kuwa, ama hakuna dawa, au mashine zimelemewa idadi ya wagonjwa.

Haya yanatokea katika nchi yetu iliyo kwenye kundi la nchi 10 zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani, lakini wakati huo huo ikiwa katika kundi la nchi 10 zilizo masikini zaidi duniani. Hapa kuna nini?

Mzazi muungwana ni yule asiyekubali kula nyama na mapochopocho mengine akiwa matembezini, ilhali watoto wake wakiloweka chumvi na kuitumia kama ‘kitoweo’. Kitendo cha Rais Kikwete kutibiwa Marekani kimeondoa tambo zote za kwamba Serikali imeboresha huduma za tiba katika hospitali za umma. Bila shaka, yeye au wasaidizi wake wakithubutu kusema wameboresha huduma za afya, swali watakaloulizwa litakuwa: “Kama mmeboresha, kwanini ninyi mnatibiwa Marekani, India na Ulaya?” Swali la aina hii haliwezi kupatiwa jibu.

Wabunge wetu ambao India kwao sasa ni kama Kariakoo, hawawezi kuwa na utashi wa kuibana Serikali kuboresha hospitali au kudhibiti wizi wa dawa na vifaa tiba. Wanajua India, pamoja na matibabu, kuna posho wanazolipwa. Hawa hawawezi kuhangaika na afya za maskini wa Kasesya, Rukwa wala Nyabikere kule mkoani Mara.

Haya ninayoyasema kwenye hospitali, nayasema pia kwenye elimu tunayowapa watoto wetu-kuanzia shule za awali, msingi, sekondari hadi vyuo.

Zamani hizo, watoto wa Tanzania walisoma pamoja bila kujali hali ya familia anayotoka mtoto. Mtoto wa rais aliweza kusoma darasa moja, na hata kuketi dawati moja na mtoto wa mkulima kabwela kabisa. Watoto wa mawaziri, watoto wa makatibu wakuu na kadhalika, walisoma darasa moja na watoto wa wakulima, wafugaji na wale ambao familia zao ni hohehahe.

Utaratibu huo ukawafanya, na kwa kweli ulihalalisha neno mahsusi sana miongoni mwa Watanzania la kuitana ‘ndugu’. Watoto walikuwa wakijiona wamoja na kwa sababu hiyo wakajiona ni ‘ndugu’ wa damu.

Sasa hivi kuna matabaka makubwa katika elimu. Watoto wa matajiri na wanasiasa wanasoma academy. Watoto wa makabwela wanaishia shule za kata. Watoto wenye wazazi wenye uwezo wanawaona watoto wa masikini si wenzao. Mtoto anatoka Kigamboni, anakwenda kusoma Kwembe (kilometa 10 lazima atembee-Makondeko Kwembe-Makondeko), anawaona wenzake wakiwa kwenye mabasi yaliyoandikwa ‘school bus’; huwezi kutarajia hawa wawili wakue wakiwa na akili na ari moja ya kujenga utaifa. Hawatapendana kwa sababu wameshakuwa tofauti tangu ngazi ya awali kabisa ya ukuaji wao. Watoto wanapita kwenye ma-Land Cruiser ilhali wengine wakisota kwenye vituo vya daladala hata wakati mwingine wakiwa hawana nauli.,  Hawa wawili hawawezi kuchumbiana, na kwa kweli ukubwani watakuwa ni ‘mataifa mawili’ tofauti ndani ya Taifa moja.

Elimu yetu imekuwa mbaya kwa sababu hakuna kiongozi anayejali. Hakuna anayejali kwa sababu hakuna watoto wao wanaosoma katika shule za umma. Hapo zamani shule zilikuwa na vitabu, maabara, vifaa na walimu wa kutosha kwa sababu viongozi walijua watoto wao wanasoma katikka shule na vyuo hivyo. Mkuu wa Wilaya ya Kilindi ndiye aliyekuwa na moyo wa kuhama na watoto wake na kuwapeleka kusoma katika sekondari ya kata! Huyu ni mzalendo. Naamini, kwa kutambua kuwa watoto wake wapo shuleni hapo, atahakikisha anatumia juhudi na maarifa yake yote ili shule hiyo iwe na sifa zote za kuitwa shule.

Dawa ya kulimaliza tatizo hili ni kuhakikisha unakuwapo mpango wa kuwashinikiza watoto wa wakubwa nao wasome katika shule hizi za umma. Kufanya hivyo kutawafanya wakubwa watambue kuwa bila kuboresha hizo shule na vyuo, watoto wao nao watakuwa kwenye wakati mgumu wa kujenga maisha yao ya baadaye.

Haya mawili – ya tiba na shule za umma – yanafanana na foleni katika miji yetu. Kama wakubwa wameona njia ya wao kukabiliana na foleni ni kutumia ving’ora vya polisi ili wapishwe, sidhani kama kuna siku watahangaisha vichwa kumaliza matatizo ya msongamano wa magari hasa Dar es Salaam. Tukumbuke Rais mwenyewe keshasema hizo foleni ni alama ya maendeleo! Kwa maneno mengine tuamini kuwa ukiona choo kimefurika, ujue hiyo ni dalili ya njema sana ya familia yako kushiba vizuri; na kwa sababu hiyo ni dalili ya shibe, huna sababu ya kupanua choo! Hatuwezi kuwa na akili za kuleta maendeleo, halafu tukakosa akili za kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na maendeleo. Haiwezekani. Huo si uongozi tunaoutaka.

Sambamba na kumpa pole Rais Kikwete, bado nasema utaratibu huu wa wakubwa kwenda kutibiwa Marekani, Ulaya, India, Afrika Kusini au Kenya usipotazamwa kwa jicho la kukomeshwa, kamwe tusitarajie huduma za afya kuboreshwa hapa nchini mwetu. Nani atahangaika na Muhimbili wakati akikohoa tu anakunjiwa dola za walipakodi kwenda kutibiwa ughaibuni? Ni hayo tu kwa leo.