Oktoba 25, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, katika mkutano wa mwaka wa tafakuri wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alitoa hotuba elekezi kama ifuatavyo:
Asalaam aleykum!
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia afya na kutuwezesha kufika hapa Iringa salama kwa ajili ya mkutano huu muhimu wa tafakuri. Ni jambo la furaha pale wahariri mnapoweza kukutana kwa wingi kiasi hiki maana sote tunajua jinsi asili ya kazi yetu inavyotubana hivyo kwamba kuonana tukiwa katika vituo vyetu vya kazi si jambo rahisi, kwani kila mmoja muda wake ni adimu mno, kila mmoja anakimbizana na deadlines pamoja na headlines! Fursa hii basi ni adhimu sana, na kwa hilo namshukuru Mwenyezi Mungu.
Niushukuru pia uongozi wa Jukwaa la Wahariri kwa kunipa fursa hii ya kuja kutoa hotuba elekezi katika mkutano huu wa tafakuri. Niliwatania wenzangu pale ofisini kwamba na mie leo nimekumbukwa, maana kuonana kwetu katika hali kama hii kumekuwa mara moja kwa mwaka katika Mkutano wa Kilele wa Mashauriano ya MCT na Wahariri unaoandaliwa na Baraza. Asanteni sana!
Ndugu Mwenyekiti,
Mada mliyochagua kwa ajili ya tafakuri yenu mwaka huu, “Usalama wa Wanahabari”, ni mada yenye uzito mkubwa, hasa kwa kutilia maanani matukio ambayo yametokea katika tasnia yetu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Matukio haya ya kusikitisha lazima yatufikirishe sisi kama Watanzania, lakini hasa kama wanahabari ambao ndio tumekuwa waathirika wakubwa. Kwa mara ya kwanza hapa nchini, mwandishi wa habari ameuliwa akiwa kazini, kiongozi wa wanahabari ameshambuliwa na kuumizwa vibaya, wanahabari wametishwa na kupigwa, wengine wamechomewa nyumba na mali zao kuharibiwa. Ufungiaji wa vyombo vya habari umeshamiri kuliko kipindi chochote cha hivi karibuni, na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo miwili yangu Tume ya Jaji Nyalali ilipobainisha ubovu wa sheria zinazo simamia tasnia hii, Serikali imeandaa mabadiliko sio ya kurekebisha au kufuta sheria kama Tume hiyo ilivyopendekeza, bali ya kuiongezea makali!
Ndugu Mwenyekiti,
The media is under siege. Tasnia ya habari imezingirwa. Lengo la kuizingira ni kupoka uhuru wake na kuinyong’onyeza, kuitambarajisha, kuivunja uti wa mgongo ili isisimame wima kuutumikia umma kama ilivyo dhima yake, bali iwatumikie wachache na kulinda maslahi yao huku ikiwa imejawa hofu na udhalili.
Ndugu Mwenyekiti,
Wakati kina Rais Obama wakimsifia Rais wetu kwa kukubali mpango wa serikali yenye uwazi, sisi tunashuhudia serikali hiyo ikichukua hatua ya kushambulia misingi ya uwazi kwa kufunga vyombo vya habari. Wakati maendeleo ya TEHAMA yakiielekeza dunia katika uwazi na mlipuko wa mawasiliano, viongozi wetu wanatunga sheria za kupingana na wakati na wanapeleka wahariri mahakamani kwa kutumia sheria zinazodharauliwa na jumuiya zinazopenda maendeleo. Katika muktadha huu, ni lazima wahariri, kama mlivyoamua, mtafakari kwa makini mustakbali wa taaluma yetu, na mustakbali wa demokrasia yetu changa.
Ndugu Mwenyekiti,
Niruhusu basi niongelee mambo matatu tu katika kuchokonoa tafakuri yenu. Niongelee mfumo wa sheria zinazosimamia habari hapa nchini; niongelee nini wanahabari wanapaswa kufanya au kutofanya kama wanataaluma ili kuboresha hali ya usalama wao; na nitoe maoni yangu kuhusu jukumu la Jukwaa la Wahariri na Baraza la Habari katika kuhakikisha usalama na weledi. Tasnifu yangu itakuwa kwamba usalama wa wanahabari hauwezi kutenganishwa na mfumo wa sheria unaosimamia tasnia hiyo kama jinsi ambavyo hauwezi kutenganishwa na suala la stadi na weledi wa wanahabari.
Ndugu Mwenyekiti,
Usalama wa wanahabari Tanzania unalindwa na sheria zinazowalinda wananchi wote kwa ujumla. Kwa maana hiyo, hakuna vipengele mahsusi vya sheria vinavyoelekezwa katika kumlinda mwanahabari kutokana na asili ya kazi yake. Katika kusemea usalama wa wanahabri, nimewahi wakati fulani kukosolewa na mwanasheria nguli ninayemheshimu sana kwamba nilikuwa naongea kama vile wanahabari tu ndiyo wanaoweza kupatwa na yale yaliyompata Mwenyekiti wa Jukwaa hili; kwamba naongea kama vile wananchi wengine hawastahili kutetewa; kwamba najaribu kuwafanya wanahabari kuwa “watu maalum”. Alinikumbusha mwanazuoni huyo kwamba sote tunaishi katika jamii moja, maisha yetu yakiingiliana na kuhusiana. Kwa hiyo, akaniasa, usalama wa wanahabari hauwezi kujadiliwa nje ya usalama wa raia kwa ujumla.
Bila shaka alikuwa na hoja nzito.
Nilikubaliana naye kwamba madhila yanayowapata wanahabri yanaweza pia kuwapata wananchi wengine, lakini hoja yangu ni kwamba kwa asili ya kazi yao, wanahabari wako katika mazingira mabaya zaidi ya kupatilizwa kutokana na kazi yao kuliko taaluma nyingi nyingine. Nikashikilia kwamba kukataa kuuona ukweli huo ni kukataa kutazama undani wa mambo, ni kung’ang’ania kutazama mambo kijumla jumla tu, na hilo haliwezi kutusaidia kuweka mikakati ya kutatua tatizo. Tujiulize, ni mara ngapi mwalimu, ama daktari, ama dereva, atakumbana na vitisho kutokana na kazi yake? Lakini kazi ya mwandishi ndiyo kazi ambayo mtu unaweza ukaadhibiwa, ukapatilizwa, kwa kufanya kazi yako vizuri mno! Ndiyo kazi yenye sheria lukuki za kuwafunga “vidhibiti mwendo” wanataaluma! Mara ya mwisho tulipotazama tulikuta kuna sheria zisizopungua 17 zinazokwaza utendaji bora wa mwanahabari. Hakuna taaluma nyingine yoyote nchini “inayosimamiwa” na sheria nyingi kiasi hicho, tena zote zikilenga kukwaza utendaji wake na siyo kuurutubisha!
Ndugu Mwenyekiti,
Hatuna sheria za kuwalinda watoa taarifa muhimu kwa maslahi ya umma, yaani whistleblowers. Zipo taarifa kuhusu hujuma kwa umma ambazo zimo ndani ya mafaili yaliyobandikwa nembo ya “Siri”. Kuzitoa taarifa hizo hadharani kunaweza kumpeleka mwandishi na chanzo chake jela.
Hatuna sheria ya kulinda vyanzo vyetu vya habari. Tunaweza kufungwa kwa kukataa kutaja vyanzo vyetu. Mahakama inaweza kutuamuru kutaja hadharani vyanzo vyetu vilivyotupatia taarifa au dokezo kwa misingi ya kuaminiana, kwa misingi ya kwamba tutavihifadhi. Tukikataa kuvitaja, tunaweza kuhukumiwa kwa kuidharau mahakama. Sheria haitulindi sisi wala vyanzo vyetu. Kwa hiyo kila unapoongea na chanzo (source), kinadharia chanzo hicho, kutegemea kinakueleza jambo gani, kinajitia hatarini.
Ndugu Mwenyekiti,
Wakati kuna sheria lukuki za kudhibiti vyombo na wanahabari wasiwe “wakorofi”, hakuna sheria za usalama wao wawapo kazini, hakuna sheria zinazojaribu kuhakikisha maendeleo yao kitaaluma, na hakuna zinazozuia wao kunyonywa. Mfumo wa sheria hautambui umuhimu wao bali umechachamaa kuwavizia, uwashike na makosa na kuwasulubu. Katika mfumo huu, Mwenyekiti, usalama wa mwanahabari unakuwa mashakani maana mzani umezidi uzito upande wa madhila badala ya mafao.
Ndugu Mwenyekiti,
Mfumo huu ni mbovu, haufai, na lazima sote tuungane katika jitihada za kuutokomeza, na kuweka sheria mpya zitakazohimiza kuwapo kwa mazingira mwafaka ya utendaji kazi. Sheria zitakazosimamia haki ya wananchi kujua, sheria zitakazoshamirisha uwapo wa vyombo vya habari anuwai na mujarabu. Ni muhimu tukaelewa, Mwenyekiti, kwamba alimradi sheria hizi zipo, hakuna aliye salama. Vyombo vyote vya habari, wanahabari wote, wawe wanaandikia vyombo vikubwa na vikongwe au vichanga, hawako salama, na vyombo vyao viko hatarini.
Nawaomba, wahariri, waelezeni hivyo wamiliki wa vyombo vyenu. Asijidanganye mwenye chombo kwamba yeye yu salama labda kwa sababu hii leo yuko karibu na watawala. Kesho mambo yakibadilika, naye yatamkuta. Matumizi ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 tuliyoyashuhudia mwezi uliopita yamedhihirisha kwamba ukubwa au ukongwe wa chombo si hoja. Matumizi ya sheria hii tangu waziri Fenella Mukangara ameingia madarakani kama waziri kamili yanatukumbusha kwamba mradi sheria ipo, yuko mtu ataitumia siku moja. Ukweli kwamba akiwa Naibu Waziri alimshuhudia waziri wake akijizuia kuitumia sheria hii ya kikale haukumzuia msomi huyu kuitumia kwa shauku kubwa alipopata wadhifa wa uwaziri kamili!
Ndugu Mwenyekiti,
Ni muhimu basi kuwa na mtazamo mpana tunapoliangalia suala hili. Kukasirika na kupambana gazeti moja linapofungiwa ni wajibu, jukumu na hata haki yetu. Lakini muhimu zaidi ni kukumbuka kwamba magazeti hayo yamefungiwa kwa sababu ipo sheria inayomwezesha waziri kuwa mlalamikaji, mwendesha mashtaka, hakimu, afisa jela na hata mnyongaji! Tusisahau ukweli huu. Tupambane kung’oa shina, sio kukata matawi.
Nimalizie kuongelea sheria kwa kuwaachia swali moja: mwaka 1976 wakati sheria hii ikitungwa, tasnia ya habari ilitawaliwa na vyombo vya serikali na chama tawala. Kwa nini serikali ya wakati huo iliona umuhimu wa kutunga sheria kandamizi kama hiyo wakati ambao uwanda wa tasnia ulitamalakiwa na vyombo vyake? Na kwa nini sasa serikali haitaki kuondosha sheria hiyo na badala yake inataka kupeleka Bungeni marekebisho yatakayoiongezea makali? Tafakarini!
Ndugu Mwenyekiti,
Naomba sasa niongelee jambo la pili ambalo ni umuhimu wa weledi na stadi katika muktadha wa tasnifu yangu kwamba usalama wa wanahabari unahusisha mfumo wa sheria kama unavyohusisha weledi na stadi za kazi.
Kwa miaka mingi hali ya usalama wa wanahabari Tanzania haikuwa mbaya, pamoja na kuwapo kwa sheria zenye misingi katika matakwa ya kikoloni. Mwaka 1994 nilishuhudia kwa mara ya kwanza uso kwa uso udhalimu wa dola dhidi ya wanahabari.
Katika mkutano wa vyama vya kitaaluma vya wanahabari Mashariki mwa Afrika, uliokutanisha nchi saba za Tanzania, Uganda, Kenya, Ethiopia, Seychelles, Mauritius, na Somalia, kila nchi iliwasilisha ripoti ya hali ilivyokuwa nyumbani kwake.
Tanzania iliwakilishwa na Mikidadi Mahmoud akiwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA), Ndimara Tegambwage akiwa mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-Tan) na mimi nikiwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi na Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (AJM).
Kila nchi ilieleza matatizo na mafanikio yake, lakini ilipofika zamu ya Ethiopia, mambo tuliyoyasikia yalitusikitisha sote. Kiasi kwamba mkutano uliazimia kuunda timu ya watu watatu kwenda Ethiopia kuongea na wanahabari na serikali, kujua ukweli, na kutoa mapendekezo.
Katika nchi saba, Tanzania ilipata heshima ya kutoa wajumbe wawili kati ya watatu. Timu iliundwa na Ndimara (Tanzania) kama kiongozi, Mohammed Katende wa Uganda, na mimi. Safari ilidhaminiwa na shirika la Ujerumani la Friedrich Ebert Stiftung (FES). Tulikaa siku tano jijini Addis Ababa na kukutana na watendaji wa serikali, viongozi wa wanahabari, waandishi, wahariri, na muhimu kuliko yote, waandishi waliokuwa korokoroni na gerezani. Nje ya gereza moja la ulinzi mkali, tulipokelewa na kundi la waandishi waliotuimbia nyimbo za hamasa. Baadae tuliruhusiwa kuongea na waandishi waliokuwa gerezani humo. Ilikuwa uzoefu wa aina yake, kuongea na mfungwa ambaye hamfahamiani lakini mnaunganishwa na taaluma na imani yenu katika haki ya kujua na uhuru wa habari.
Tulipokwenda katika ziara hiyo kulikuwa na waandishi 19 gerezani. Baada ya kutoa ripoti yetu waandishi waliobaki korokoroni na waliofungwa walibaki sita tu, baada ya serikali kuwaachia wengine. Tungependa kuamini kuwa jambo hilo halikuwa bahati tu, bali kwamba ripoti ilichangia. Hata hivyo maafisa wa serikali walilalamika kwamba hawakutegemea tungeandika ripoti kama tulivyoiandika hasa baada ya serikali kuonyesha nia njema hadi kuturuhusu kuongea na waandishi waliokuwa gerezani!
Lakini jambo lililofanya nikuelezeni kadhia hii ni kwamba pamoja na matatizo yote ya dola na sheria za Ethiopia tulizozikuta, tulibaini pia ukweli mmoja. Kwamba kiwango cha weledi katika uandishi wa nchi hiyo kilikuwa chini mno, na waandishi aghalabu walijiingiza katika matatizo ambayo wangeweza kuyaepuka kutokana na kukosa stadi stahiki na weledi. Waliingia katika mapambano yasiyo na tija dhidi ya dola na viongozi, na wakati mwingine mapambano hayo yalisukumwa na mambo binafsi badala ya maslahi ya umma. Tulisisitiza umuhimu wa mafunzo na weledi katika ripoti yetu.
Ndugu Mwenyekiti,
Mimi naamini kuwa maadili na weledi ndiyo ngao ya kwanza kabisa ya mwanahabari. Kazi yetu hii ni ya hatari bila hata kuichumbia hiyo hatari. Bila kufanya kosa tunaandamwa, seuze pale tutakapowapa kisingizio kwa udhaifu katika utendaji wetu? Tuepuke tabia na utendaji unaoweza kutuletea matatizo yasiyo ya lazima. Tukiwa watumishi wa kweli wa umma, itakuwa rahisi hata kuulilia umma pale tutakaposonolewa. Umma utatuelewa, umma utatulinda. Lakini kama utatuona tumejaa tadi na kiburi cha wateule, kwa nini ujali pale madhila yatakapotukuta?
Ada ya mwanahabari wa kweli hunena mwanahabari ni mtumishi wa jamii. Mathalan, ni haki kwa chombo cha habari kuwa na msimamo wa kiitikadi, na kuutetea msimamo huo katika safu muafaka. Lakini ni hatari kutumikia makundi, au maslahi ya watu binafsi. Nimepata kulisema hili huko nyuma na sitachoka kulirejea.
Tuwe “vijana wa umma”, sio vijana wa watu binafsi, wawe wanasiasa, wafanyabiashara au hata viongozi wa dini. Sisi ni watu muhimu, na tusiruhusu watu kututumia watakavyo. Tukiruhusu kutumiwa, basi tutaumizwa. Maana tutaingia kucheza ngoma si yetu, ngoma tusiyoijua! Tutachuma maadui tusiowajua, na mambo yakiwa mabaya tunaodhani marafiki zetu watatutelekeza maana hakuna anayemthamini kiumbe anayetumika kama mwanasesere!
Ndugu Mwenyekiti,
Tuepuke vishawishi vya kutumia mambo binafsi na yasiyo binafsi tuliyoyabaini wakati wa kutenda kazi zetu kuwatisha watu ili watupatie fedha au upendeleo fulani. Waingereza wanaita blackmail. Marekani kuna usemi kwamba dawa ya blackmailer ni kumwua! Maana blackmail haina mwisho. Ukipewa leo ukatumia zikaisha utarudi kesho na madai makubwa zaidi.
Tukatae rushwa na kununuliwa. Mtu akikununua anatarajia ubaki umenunuliwa! Hategemei kesho umwambie sasa wewe ni mtu huru, hutaki akutumie! Atafanya kila njia kukudhuru maana atakuona msaliti ama mwasi.
Na tena pia tuzingatie kanuni kubwa kabisa ya kazi yetu, ambayo ni kuwa wakweli. Tuepuke hiana, tuepuke kufanya kazi kwa chuki. Tusiwasingizie watu wasiyoyafanya, tusishuhudie uongo. Tusitunge habari, wala tusibadilishe picha magazetini kuwa tofauti na ukweli kwa malengo ya kuwapakazia watu, hata kama hatuwapendi! Photofiction inafaa katika sanaa lakini sio katika taaluma ya habari.
Ndugu Mwenyekiti,
Nimalizie sehemu hii kwa kusisitiza jambo moja: daima tujipange kushughulikia masuala badala ya watu binafsi: deal with issues rather than personalities! Mambo ya watu binafsi ya nini kama hayagusi maslahi ya umma? Na yakigusa maslahi ya umma basi yamekoma kuwa ya binafsi! Tusihangaike na mambo yasiyo na tija. Stadi zetu ni muhimu sana, haifai kuzitumia kwa mambo ya hovyo.
Ndugu Mwenyekiti,
Niruhusu sasa nitoe maoni yangu kuhusu wajibu na majukumu ya Jukwaa lenu, na Baraza la Habari. Kwa maoni yangu, hivi ni vyombo viwili muhimu kabisa katika maendeleo ya tasnia yetu. Vyombo hivi vyote vimeundwa na wanatasnia wenyewe baada ya kuona wanayo haja ya vyombo kama hivyo. Katika kazi yangu nimeshutumiwa mara nyingi kwamba.
Baraza linadhani waandishi ni miungu-watu, hawakosei, wala hawastahili kusemwa na hata kuadhibiwa! Lakini mimi huwa nawaambia kitu kimoja: kwamba kuundwa kwa MCT ni ushahidi tosha kuwa wanahabari wenyewe wanatambua kuwa wao ni wanadamu wanaokosea, na ndio maana wakajiundia utaratibu huu wa kujikosoa, kujisimamia, kujirekebisha na kusuluhisha matatizo yao na wadau. Hakuna taaluma isiyokuwa na changamoto. La muhimu ni kuazimia kuzifanyia kazi changamoto hizo, na kufuatia maazimio hayo kwa matendo.
Nionavyo mimi, Jukwaa la Wahariri
Tanzania linafanya kazi nzuri. Kuwakusanya wahariri, wakaongea mambo yanayohusu kazi yao, wakakosoana na kupongezana, wakatiana shime na kufarijiana, ni kitu muhimu sana. Nafasi ya uhariri inaweza kuwa kazi ya upweke sana. Maripota wanakuangalia jicho pembe; wahariri wenzio wanatafuta namna ya kuku-scoop; mwajiri anakupumulia shingoni uongeze mauzo au watazamaji na wasikilizaji; wanasiasa wanakupenda pale unapowanyooshea mambo yao lakini hawasiti kutupa jongoo na mti wake wakiona huwasaidii; na wakati mwingine mhariri unaona kuwa hata jamii unayojaribu kuitumikia haikuelewi! Ni kazi ya upweke! Kwa kuweza kuwaunganisha wahariri, kuwaleta pamoja, hilo tu ni jambo kubwa linalostahili pongezi. TEF iendelee hivyo.
Ndugu Mwenyekiti,
Huko tuendako mimi ningependa kuona TEF inakuwa na programu bayana na inayotekelezwa. Shughuli za Jukwaa zisiwe za papo kwa papo, zisiwe ad-hoc. Tumeshirikiana nanyi kuweka walau sekretarieti ndogo. Baraza liko tayari, na lingependa, kushirikiana nanyi kuijengea bodi yenu uwezo, pamoja na sekretarieti. Baraza lingependa kushirikiana nanyi kuandaa mpango mkakati wa TEF unaouzika kwa wahisani wa ndani na nje.
Baraza liko tayari kuwatambulisha na kuwadhamini pale itakapohitajika na mtakapoamua hivyo, mradi miundombinu ya kitaasisi iwepo. Baraza linalitambua Jukwaa kama mdau na mshirika muhimu kabisa. Ni katika maslahi ya Baraza na wadau wake kuwa na Jukwaa la Wahariri lenye nguvu na linaloaminika. Tutafanya kazi nanyi kuijenga TEF.
Kuhusu MCT, Mwenyekiti, niseme nini? MCT ni mali yenu. Itafanya kile ambacho tasnia itaona inahitaji. Na itafanya hivyo kwa uadilifu na weledi mkubwa. Sihitaji kuwaelezeni nyinyi kwamba mmefanikiwa kuwa na Baraza la Habari linalopigiwa mfano duniani kote. Wataaluma wanakuja pale Mwenge kutoka kona mbalimbali duniani kujionea na kujifunza toka MCT.
Wengine wanakuja kukidhi tu dukuduku la kuona kama kweli hayo yanayosemwa yapo. Wengine wanakuja kweli kujifunza. Wengine wanakuja kutafuta ushauri na kusikia maoni ya MCT kuhusu mambo yanayoendelea katika tasnia ya habari nchini, kama walivyokuja mabalozi na wanadiplomasia waandamizi toka nchi 14 za Ulaya na Canada pale Mwananchi na Mtanzania yalipofungiwa. Tunawakaribisha wote, tunaongea nao, maana ni jukumu letu kujenga madaraja yatakayosaidia kuisukuma tasnia yetu mbele.
Ndugu Mwenyekiti,
Wahariri ni lazima wafanye kazi kwa karibu na Baraza. Pamoja na shughuli za uraghbishi, uzengeaji na utetezi; shughuli za utafiti na machapisho; za mitaala na viwango vya mafunzo; Baraza lina jukumu kubwa la kusimamia maadili na kusuluhisha migogoro kati ya vyombo vya habari na raia. Jukumu hili ni muhimu maana ndiyo msingi wa mfumo wa kujisimamia wenyewe, yaani self-regulation. Tunahitaji sana ushirikiano wa wahariri.
Mhariri akilalamikiwa, kisha akapuuza mwito wa MCT, anatujengea sote mazingira ya kuambiwa mfumo huu umeshindwa na bora serikali iingilie kati. Kuhujumu kwa njia yoyote ile kazi ya MCT ya kusimamia maadili na kukuza weledi ni kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hii. Tuelewe wazi kabisa kwamba ombwe lolote litakalotokana na MCT kuonekana inashindwa kutekeleza jukumu hili, litazibwa na serikali. Na halitazibwa kwa kuchekeana, litazibwa kwa kuanzisha sheria mbaya kuliko hata hizi tulizo nazo sasa, na kuzitumia.
Ndugu Mwenyekiti,
Kanuni za maadili zinazosimamiwa na MCT zimekubaliwa na kupitishwa na wanahabari wenyewe. Kanuni hizi zisionekane zinafaa pale zinapombana mshindani wa mmoja wetu lakini zikawa hazifai pale zinapoelekezwa kwake. Ikiwa mnadhani kuna haja ya kufanya mabadiliko katika kanuni, semeni hivyo na fanyeni mabadiliko hayo, maana ni nyie mliozipitisha! Mwakani kuna mapitio ya hiyo Code of Ethics. Nawaalika wote kushiriki ili tuendelee kuwa na mwongozo bora utakaosimamia utendaji wetu.
Kuhusu hatua za moja kwa moja juu ya suala la usalama wa waandishi, pamoja na hatua nyingine, Baraza limedhamini kuandikwa kwa mwongozo wa mafunzo ya utendaji kazi katika mazingira ya hatari (Manual on Covering Volatile Situations). Mwongozo huu umeandaliwa na Watanzania wenye uzoefu wa kimataifa katika mambo haya, Valerie Msoka na Anaclet Rwegayura, na mafunzo yameanza.
Lakini tumeazimia pia, kupitia Muungano wa Haki ya Kupata Habari (Coalition for the Right to Information) unaounganisha asasi kumi ikiwamo TEF, kuomba kuonana na Rais Kikwete kumweleza dukuduku zetu kuhsu masuala ya usalama wa waandishi na sheria zinazosimamia taaluma ya habari.
Baraza tutaendelea kuwasiliana na wahariri katika masuala ya maadili kama ambavyo tumekuwa tukifanya, kwa simu na barua, bila kusubiri watu walete malalamiko. Tutaendelea kudhamini mafunzo na tafiti. Tutaendelea kupigania sera na sheria bora, na tutaendelea kujenga mifumo mtandao itakayoifanya tasnia ishikamane na kuwa imara zaidi.
Ndugu Mwenyekiti,
Na sasa niwasilishe kwako binafsi, na kwa wajumbe wote wa mkutano huu wa tafakuri wa mwaka, salamu za upendo, heri na fanaka kutoka kwa rais wa MCT, Mhe. Jaji Dk. Robert Kisanga, akikuhakikishieni ushirikiano wa Baraza na kurejelea udugu wa taasisi mbili hizi za tasnia yetu.
Nakutakieni mijadala pevu itayopevua urazini wenu kwa manufaa ya taaluma na tasnia yetu.
Asanteni kwa kunisikiliza!