Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Bunda
Juni 11 , 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda imeamuliwa kesi ya Jinai Na.01/2023 mbele ya Mulokozi Kamuntu, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa mahakama hiyo.
Katika shauri hilo lililoendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Bw. William Lyamboko, mshtakiwa Bw. Alloyce James Emanuel ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji Kata ya Chitengule Wilaya ya Bunda, alishtakiwa kwa kosa la kuomba hongo ya sh. 130,000/= kosa chini ya kifungu cha 15(1)(a) na (2 ) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya Mwaka 2022.
Lyamboko alieleza kuwa mnamo Oktoba 14, 2022 mshtakiwa aliomba hongo hiyo kutoka kwa Simon Kadilahna Shija ili aweze kuwaachia ng’ombe wake baada ya kuwakamata wakifanya uharibifu wa mazao katika maeneo ya mashamba ya watu.
Mahakama imemhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. 500,000 kwa kila kosa hivyo kwa makosa yote mawili aliyoshitakiwa nayo alipaswa kulipa sh. 1,000,000.
Mshtakiwa amepelekwa gerezani baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.