*Awatupa Jaji Ihema, Beno Malisa, Daniel Nsanzugwanko
*Pia wamo Mbunge Mwanjelwa, Kijazi, Profesa Rutashobya
*Chanzo ni tuhuma za rushwa ugawaji vitalu vya uwindaji
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ameifuta kazi Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii. Kamati hiyo, pamoja na mambo mengine, imelalamikiwa mno kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa wajumbe wake zaidi ya 10.
Mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, alivunja Kamati iliyoundwa na mtangulizi wake, Shamsa Mwangunga, hata kabla haijaanza kazi. Ilikuwa chini ya uenyekiti wa mmoja wa Watanzania waliobobea katika tasnia ya wanyamapori, Mgana Msindai.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati iliyovunjwa wanatuhumiwa kupokea rushwa wazi wazi kutoka kwa waombaji vitalu. Mgawanyiko mkubwa uliibuka ndani ya Kamati kutokana na kila upande kuvutia kwake. Hali hiyo ilisababisha Kamati ipoteze maana. Hata hivyo, baadhi ya waomba vitalu walikuwa wakiwasifu mno Mwenyekiti Mbano na Profesa Rutashobya kwa msimamo imara wa kutenda haki.
Kamati iliyovunjwa na Balozi Kagasheki ilikuwa ikiongozwa na Bakari Mbano ambaye amepata kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mwaka 1995-1998. Kamati ya sasa iliundwa Machi, 2011, kwa kuzingatia kifungu 38 (3) cha Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Kwa kawaida, kama hakuna kashfa, Kamati hiyo inatakiwa iwe madarakani kwa miaka mitatu.
Pamoja na Mbano, wajumbe wengine walikuwa ni Dk. Simon Mduma (Mkurugenzi Mkuu TAWIRI), Edward Msyani (kwa niaba Mkuu wa Chuo cha MWEKA) na Saidi Nzori (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali). Nzori alishiriki kwenye mchakato wa awali wa kutungwa kwa Sheria Na. 5 ya 2009.
Wajumbe wengine walikuwa Allan Kijazi (Mkurugenzi Mkuu TANAPA), Obeid Mbangwa (Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori –ambaye alifukuzwa kazi hivi karibuni), Jaji Steven Ihema (Jaji mstaafu, na Kamishna wa Maadili), Mbunge wa Viti Maalumu Mary Mwanjelwa (CCM), Profesa Leticia Rutashobya (Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Daniel Nsanzugwanko (Naibu Waziri wa Kazi wa zamani), na Beno Malisa ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Mei, mwaka huu, aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya, alizungumza na waandishi wa habari na kuishutumu Kamati ya Ushauri wa Ugawaji Vitalu, akisema ilikuwa imepoteza maana, na akamshauri Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki, aivunje haraka.
Alisema, “Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge na ile ya Kumshauri Waziri kuhusu Ugawaji wa Vitalu walikwishatumbukia katika mtego na kutoa ahadi kwa kampuni hizo kuwa watalitumia Bunge kugawa vitalu upya na kwamba watasaidia idadi ya kampuni hizo kupanda mpaka asilimia 30 ya uwiano (kutoka asilimia 85 kwa wazawa dhidi ya asilimia 15 kwa wageni).
“Iliandikwa katika gazeti kwamba huko Dodoma baadhi ya wabunge walikarimiwa kwa njia ya semina na mwanasheria anayetumikia baadhi ya kampuni za kigeni. Wabunge hao, kwa mujibu wa taarifa hizo, wanadaiwa walipewa posho nono ya semina hiyo.
Majina yao yanajulikana.”
Masuala ya uwindaji wa wanyama yameelezwa katika vifungu vya 38 hadi 49. Kifungu cha 38 (1) kimeanzisha Kamati ya Ushauri wa kugawa Vitalu ambayo ni chombo cha kumshauri Waziri. Kifungu cha 38(2) hadi (4) kimetoa mamlaka kwa Waziri kuteua wajumbe wa Kamati pamoja na Mwenyekiti.
Majukumu ya Kamati yameainishwa katika Kifungu cha 38(5), nayo ni: Kupokea na kupita taarifa za uwindaji wa kitalii na ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini; kupitia na kutoa ushauri katika maelekezo na Kanuni zinazohusu ugawaji wa vitalu na masuala mengine yanayohusu ugawaji wa vitalu; kumshauri Waziri kuhusu masuala yanayohusu maombi, masharti, ugawaji na vigezo vya ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii; na kufanya kazi nyingine zinazohusiana na ugawaji wa vitalu kama itakavyoagizwa na Waziri.
Mamlaka ya kugawa vitalu yamewekwa kwa Waziri chini ya kifungu cha 38(6) ambako Waziri atagawa vitalu baada ya kupokea ushauri wa Kamati. Dk. Mzindakaya aliongeza, “Kwa hivi sasa tatizo j ingine kubwa ni mgawanyiko ndani ya Kamati ya Kumshauri Waziri kwa vile kuna baadhi ya wajumbe wamekwishajitumbukiza katika vitendo vyenye masilahi binafsi. Majina ya wabunge na wajumbe wa Kamati wanaotumiwa yanafahamika.
“Nashauri kuwa, kwa kuwa Wizara hiyo imepata Waziri mpya, Waziri ashauriwe kuvunja Kamati ya sasa ya Ushauri wa Ugawaji wa Vitalu.” Itakumbukwa kuwa ni Dk. Mzindakaya aliyefanya juhudi za kutungwa kwa Sheria mpya iliyotoa fursa kwa Watanzania kuingia kwa wingi kwenye tasnia ya uwindaji wa kitalii.