Viongozi Maziwa Makuu waufanye kwa uangalifu
Kama kuna nchi ambayo imeweza kurithi vilivyo udanganyifu wa kisiasa na unafiki ambavyo himaya kuu ya zamani ya ‘Roma’ ilikuwa navyo, basi ni Taifa kubwa la sasa ‘Marekani’.
Hakika Marekani ndiyo dola kubwa linaloongoza kwa kuwa ‘wakili wa shetani (the devil’s advocate)’.
Katika enzi hizi za Marekani kuwa dola kubwa, yaani kuwa babeli mkuu, damu ya watu wasio na hatia na wasioujua hata huo ubepari wenyewe imemwagika mno na hakuna hata chembe ya soni au hatia ambayo Marekani imejivisha. Hakika imekuwa Roma. Roma ya ustaarabu na sheria vilivyoleta mateso yasiyomithilika.
Marekani imesababisha mateso ya watu wengi kwa sababu ya lengo moja! Kujitanua ili kujichanua kiuchumi. Imevaa ngozi ya kondoo na kuvuma kama bingwa wa huruma, mtoa misaada mkuu, mfadhili wa miradi ya kimataifa, mtetezi wa haki, mshauri na mdhamini wa sera! Ni mwasisi wa sheria mbalimbali duniani hata hizi za kifirauni!
Kwa juu juu, Marekani imekuwa baba mwema kimipango – tazama imekuwa mnywa damu mkubwa kuliko nchi zote. Mnyanyasaji asiye na haya.
Kwa mahitaji yake ya nafaka, Roma iliziteka, kuzipiga na kuzikatili jamii zote zilizoishi jirani yake kati ya karne ya pili kabla ya Kristo mpaka karne ya tano baada ya Kristo. Miaka mia nane!
Kwa sababu za mahitaji ya nishati, mafuta na gesi, madini ya thamani na masoko, Marekani imetengeneza, imehadaa na kutekeleza unyama mwingi uvukao ubinadamu. Imevamia dola nyingine, imeratibu mauaji (assassinations), imetengua chumi za nchi lukuki na imefanya mataifa mengi kuishi chini ya ujahili.
Rwanda ni moja kati ya wahanga wa hayo. Kwa kuwekeza kwenye udhaifu wa historia ya Rwanda, uroho wa makabila yaliyomo, lakini pia kwa kuandika ‘hundi’ za misaada, Marekani imeitumbukiza nchi hiyo kwenye vipindi vilivyotawanya wananchi na kuleta vilio, jasho, damu na yatima.
Chanzo cha kutumiwa Rwanda kinarejea miaka ya nyuma. Katika makala zilizopita nilionesha kuwa kama miaka ya 1980 Kongo isingekuwa na utajiri ilionao, basi eneo la Maziwa Makuu lingekuwa shwari. Pasingekuwapo na sababu za Marekani na Uingereza kuwekeza kwenye vita isiyoisha!
Vita, pamoja na mabaya yanayoambatana nayo, huleta mianya. Huleta ukosefu wa uthabiti na usimamizi mbovu wa rasilimali! Kwa wasiojua sayansi ya jamii na ufundi wa kisiasa, hawawezi kuiona thamani ya kiuchumi itokanayo na vita. Ni thamani ‘mianya’.
Thamani hiyo ni kutoa mianya ya uporaji rasilimali kwa kutumia ‘mabwana’ wa vita (warlords). Vita za Kongo ni matokeo ya utashi wa makusudi wa baadhi ya nchi kutengeneza mazingira ya ubabe wa kivita ili wanyonye rasilimali.
Thamani ya rasilimali asilia za Kongo inakadiliwa kufikia dola za Marekani trilioni 24. Hili ni sawa na pato la ndani (GDP) la nchi za Marekani na Ulaya Magharibi zikiunganishwa. Ni thamani kubwa ajabu! Naomba niseme kuwa hii hesabu ndiyo iliyochochea mauaji ya halaiki mwaka 1994.
Sote tunajua vizuri bila shaka kuwa Uganda ndiye mwanzilishi wa RPF na Kagame katika ndoto zao za kurudi Rwanda miaka ya 1980 na 1990. Nimelijengea hoja hii katika sehemu zilizotangulia.
Ukweli pia ni kwamba Uganda si nchi tajiri inayoweza kudhamini vita ndefu (a serious and protracted war).
Mbali ya Uganda kutoweza kudhamini vita ndefu, haina teknolojia ya kutengeneza silaha. Uganda si dalali (agent) wa silaha kutoka kokote kuelekea kokote. Hili linamaanisha Uganda ilipata silaha kwingineko ili kuwapa RPF!
Kagame na RPF yake hawakuwa na thamani za kuweza kununua silaha kwa fedha taslimu. Katika utafiti wote nilioufanya juu ya suala hili, nimepata kujua kuwa fedha za michango walizochangisha RPF kutoka kwa Watutsi ndani ya Rwanda, Uganda, Tanzania, Kenya, Burundi, Zaire, Ulaya na Marekani ziliweza kuwalisha wanajeshi msituni, kwa shida, si zaidi ya hapo. Hawakupata mwitikio mkubwa kimakusanyo.
Pamoja na ufinyu wa michango, uwezo wa RPF kuwalisha vizuri na kuorodhesha wapiganaji wapya ulipanuka. Hesabu zinaonesha kuwa wakati uvamizi wa Rwanda unaanza Oktoba 1990, RPF ilikuwa na wapiganaji zaidi ya 4,000. Mwezi mmoja katika mapambano walikuwa wamefyekwa hadi kufikia 2,000!
Baada ya kufyekwa, wakati huo huo kamanda wa uasi, Fred Gisa Rwigyema akiwa ameuawa, Marekani haraka ikamsimamisha masomo ya kijeshi Paul Kagame aliyekuwa chuoni Fort Leavenworth, Kansas. Amri ikatoka akaongoze uasi wa RPF!
Pana jambo kubwa. Huyo mtoka Marekani, rasmi akafika na kusimamisha mashambulizi ya aina yoyote ili ajipange. Akaanzisha kambi Kaskazini mwa nchi kwenye milima iitwayo ‘Virunga’.
Miezi mchache baadaye mahesabu ya wapiganaji wa ‘mtoka Kansas’ yakawa: wapiganaji 5,000 mwanzoni mwa 1991, wapiganaji 12,000 kufikia 1992 na mwaka1994 alikuwa na vikosi vya wanajeshi 25,000, yaani mara tano ya jeshi la Serikali ya Rwanda ambayo ilikuwa na fedha za nchi (wanajeshi 5,200).
Tuseme ukweli zaidi ya takwimu hizo? Hapana. Zaidi ya chochote, takwimu zinaonesha kuwa kuja kwa ‘mtoka Kansas’ kulileta fedha za kuwakonga nyoyo vijana. Vijana walimiminika kujiunga na RPF kutoka pande zote za Maziwa Makuu.
Waliohojiwa wanadai walilipwa vizuri kwa dola za Marekani. Hao Watutsi wanaoisumbua Kongo sasa kama Laurent Nkunda, Bosco Ntaganda, Sultani Makenga na wengineo wengi walimiminika kipindi hiki.
Kagame alikuwa na sehemu gani ya kuzitoa dola hizo za kugharimia wapiganaji 25,000?
Nakumbuka nilimsoma mwandishi wa Uingereza, Ian Birrell, kwenye gazeti la ‘The Independent’ mwaka 2009. Alikuwa amewahoji vijana katika Jiji la Addis Ababa, Ethiopia.
Kwenye makala ile, Mwingereza huyo mashuhuri, mwandishi wa habari na mhariri mkuu, alihadithiwa na mamia ya vijana wa nchini Ethiopia walivyoajiriwa kwenda Rwanda kama mamluki wa RPF miaka ya 1991 mpaka 1994. Walidai pia kulikuwapo na Wasomali wengi tu! “Walikuwapo pia wazungumza Kiswahili wengi,” mmoja wa vijana wale alisisitiza.
Tofauti na wengi tulivyodhani kabla ya hapo, vita ya RPF Rwanda haikuwa ya kiukombozi. Wanyarwanda waliohusika hawakujua, lakini leo hii kwa jinsi ‘walivyofungwa kisiasa’ kwa madai ya usalama, vijana wao walivyochukuliwa na kupelekwa jeshini kwa nguvu hata wenye umri mdogo! Wakafanywa wanajeshi wa uasi wa Kongo kushtuka. Wameanza kujua kuwa ilikuwa ni vita ya kimkakati na iliwahusisha wengi Maziwa Makuu.
Sina budi kumtumia shujaa wangu kiuandishi. Mtu ambaye kunako mwaka 1995 alinivutia kufuatilia siasa za Maziwa Makuu, hasa Watutsi na mitazamo yao. Huyo ni Ben R. Mtobwa, Mtanzania ambaye aliandika makala yenye uchungu. Makala niliyoitunza kwa miaka mingi.
Atashangaa nikikumbushia kuwa makala yake ndefu, yenye sehemu tatu, iliyoitwa “Mpango wa Watutsi kuzitawala nchi za Maziwa Makuu upingwe” ndiyo asili ya utafiti wangu.
Ben Mtobwa kwenye Heko: Gazeti Dume la Kila Siku, alionesha ni jinsi gani matatizo ya vita katika Maziwa Makuu yalivyokuwa yakipangwa na kuratibiwa na watu waliodhani wao wana asili ya kutawala kuliko wengine.
Alifahamisha kwa ushahidi na takwimu kuwa hao Watutsi walikuwa kutokana na asili yao ya kuwa “militalistic and power-mongerists”, yaani ‘asili ya kupambana na kuwa na uchu wa madaraka’ wamejitengenezea kuchukiwa.
Katika hilo, akaonesha kuwa kulikuwapo na mpango wa wao kujaribu kuliteka eneo la Maziwa Makuu na kujifanya tabaka tawala. Waandishi wengine, hasa wa Uganda niliowasoma, wanadai kuwa Watutsi wana ajenda ya kutengeneza mfumo wa siri uitwao “Hima empire” katika Maziwa Makuu.
Kabla ya vita ya Rwanda, Burundi ilikuwa imepata msukosuko wa kutisha mpaka rais wake wa kidemokrasia alichinjwa na jeshi lake mwenyewe.
Rais yule aliitwa Melchior Ndadaye. Hakuna jumuiya ya kimataifa iliyopiga kelele au kumfuatilia kiongozi yeyote aliyepanga hilo. Hali ikaendelea kuchafuka huku Watutsi wa Burundi wakichinja maelfu kama si malaki ya Wahutu.
Kiongozi aliyechaguliwa baada ya Ndadaye, Cyprien Ntaryamira, akasafiri pamoja na rais mwenzake wa Rwanda mwaka 1994 na ndege yao ikadunguliwa muda mfupi kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Kanombe jijini Kigali.
Baada ya mauaji hayo, chinja chinja ya Wanyarwanda ikaanza. Ilikuwa ni ya Wahutu dhidi ya Watutsi, Watutsi dhidi ya Wahutu. Wote waliua na kuuawa.
Wakati mauaji yanaanza, tumeona kuwa Serikali ya Rwanda ilikuwa na wanajeshi 5,200 ilhali RPF ilikuwa na wapiganaji 25,000. Pia RPF ilikuwa kupitia Uganda, lakini kutokea nchi fulani zenye kutengeneza na kuuza silaha inapokea vifaa vya kisasa na vizito ilhali kutokana na vita Serikali ya Mpito ya Rwanda ilikuwa imewekewa vikwazo kununua silaha!
Je, wajua? Mauaji ya halaiki yalifanywa kwa Wahutu, Interahamwe, kutumia mapanga na silaha za jadi. Hili linawakilisha unyonge! RPF walikuwa wengi na walikuwa na silaha za moto.
Hapa fumbo linafumbuliwa! Tunaona kuwa mazingira ya amani kwenye nchi za Rwanda na Burundi tayari yalifikia kukosa matumaini (hopeless) kwa Wahutu. Wa Burundi walikuwa wakiuawa ovyo mpaka marais wao.
Nchi ambayo Wahutu walibaki na madaraka ilikuwa ni Rwanda. Aprili 1994 RPF ya Watutsi ilikuwa ikikaribia kutwaa madaraka! Hofu ikatanda kuwa Rwanda inageuzwa kama Burundi. Wahutu wakaitikia kwa kuwawinda na kuwachinja Watutsi.
Hapa kuna visa vya jazba na kupotelewa matumaini. Wahutu wa Rwanda walikuwa tayari wanatumbukia kwenye mateso kama ya Warundi na hawakuwa na silaha za kuweza kukabiliana na Jeshi la RPF. RPF ilikuwa na vyombo vya kisasa na wapiganaji wengi (25,000).
Kisaikolojia, mtu anapoamua kuvamia kwa mapanga dhidi ya adui mwenye silaha za moto, basi ni wazi mtu huyu amejitoa muhanga kwa sababu anadhani hana jinsi!
Mauaji ya kimbari yalianzishwa na kudunguliwa kwa ndege ya Rais Juvenal Habyarimana. Wadunguaji wa ndege hiyo hawajafuatiliwa wala kupatikana. Mataifa ya nje kama Marekani, Uingereza na Ufaransa sasa yanatuhubiria kuwa wadunguaji walikuwa ni wanajeshi ambao hawakuridhia uamuzi wa Habyarimana kukubali serikali ya mpito.
Tujuavyo sisi watafiti, huo ni mtizamo wa RPF toka imeiteka Rwanda. Kwanini mataifa makubwa yanakwepa kufanya uchunguzi ili yatoe ‘objective proofs?’
Jibu halitoki mbali. Wana-Magharibi wanaficha ukweli ili wasiumbuke.
Patrick Karegeya ambaye alikuwa mkuu wa ujasusi na operesheni za kiupelelezi ndani ya RPF wakati Habyarimana anadunguliwa, amekufa baada ya kuitangazia dunia kuwa ana ushahidi wa kuihakikishia kuwa Kagame alipanga mauaji hayo na kuyatekeleza.
Aliiambia dunia kuwa wao, RPF, walifanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wahutu ndani na nje ya Rwanda. Baada ya hapo akatolewa uhai.
Theogene Rudasingwa alikuwa ni meja wa jeshi katika RPF na alikuwa katibu mkuu wa chama. Amefika mahakamani nchini Hispania na amewasilisha ushahidi kuwa bosi wake Kagame alimtaarifu kwa mdomo kuwa ‘sisi ndiyo tumemdungua’ Habyarimana.
Je, kuna ushahidi mwingine mzito wa kuonesha nani alianzisha mauaji ya halaiki? Inadaiwa wadhamini wa mapigano yale walikuwa Marekani na Uingereza, Kagame alitekeleza wakati Interahamwe na RPF walitengeneza muziki.
Inadaiwa hao ndiyo wauaji wa Wanyarwanda kwa sababu ya uchu wa mali na madaraka!