Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
KAMISHNA wa Idara ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila amesema sababu ya kuundwa kwa taasisi hiyo ulitokana na kuwepo kwa mikataba mibovu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 16, 2023, wakati wa kikao kazi na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), jijini Dar es Salaam kilicholenga kueleza majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake.
“Sera mahususi ya ubia ilianza 1996 kutokana na kuwepo kwa mikataba mibovu baina ya Serikali na sekta binafsi.
“Kanuni iliundwa mwaka 2011, 2015 na kufanyiwa marekebisho mengine mwaka 2018, na sasa kuna marekebisho tena,” amesema Kafulila.
Kafulila amesema, PPP msingi wake ni kuondoa migogoro kati ya sekta binafsi na serikali ambayo ilikuwa ikitokea mara kwa mara.
Amesema, kutokana na umuhimu wa sekta binafsi, Serikali lazima itafute njia ili kuhakikisha sekta hiyo inaondolewa vikwazo.
“Lazima Serikali itafute njia ambazo inaweza kuhakikishia sekta binafsi inakuwa, ndio maana imekuwa ikifanya marekebisho ya sera yake mara kwa mara,” amesema Kafulila.
Amesema, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kiwango kikubwa, unasaidia kupunguza msongamano, mvutano na migogoro kati ya sekta za serikali, pia kusaidia watu kupata huduma kwa uraisi na haraka zaidi.
Akizungumzia Tanzania na ujenzi wa miradi mikubwa, Kafulila amesema, bado Tanzania inayo nafasi nzuri ya kuendela na ujenzi wa miradi ya namna hiyo kulinganisha na nchi nyingi za Afrika.
“Katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Tanzania ipo vizuri kwenye kupima uzito wa deni, kwamba tuna afadhali.
“Kutokana na utafiti uliofanywa na Global Credit Agency Mwaka 2017, 2021, na 2022 katika kupima madeni ya nchi, tuko vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amesema, kuna umuhimu mkubwa wa kulinda sekta binafsi kwa kuwa ndio inaendesha uchumi wananchi.
Amesema, ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi unapaswa kuimarishwa na kuondolewa vimelea vyovyote vya uadui.
“Ushirikiano kati ya PPP na serikali ni muhimu, ulinzi wa PPP ni muhimu kwa kuwa unakuza uchumi wa nchi,” amesema.