Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliyerejea chama chake cha zamani – Chadema – amesema kuwa moja ya mambo anayofikiria ni kugombea tena ubunge.
Akizungumza na JAMHURI, Kafulila amesema kuwa ubunge ilikuwa ni moja ya ngazi ya kumuinua hata kufikia malengo yake, huku akijinasibu kwamba Chadema imekuwa ni sehemu ya maisha yake, chama hicho kitamfanya ajiimarishe kisiasa.
“Mwanasiasa yeyote kama mimi, lazima awe na malengo. Hali hiyo husaidia kutimiza ndoto. Binafsi natarajia kutoa mchango wangu katika jamii ya Watanzania kwa lengo la kuchochea mabadiliko ambayo ni kilio cha wengi.
“Nahitaji kuona rasilimali tulizonazo zinaakisi hali halisi ya maisha ya Watanzania wengi,” amesema Kafulila.
Mwanasiasa huyo ambaye mwaka 2014, akiwa Mbunge wa Kigoma Kusini, alitoa mchango mkubwa katika sakata la Escrow, ameiambia JAMHURI, kuna siku Tanzania itakuwa na siasa zenye uwiano sawa, tofauti na hali jinsi ilivyo sasa.
“Kwa mfano, inapofikia wakati wa upatikanaji wa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), dola inashiriki kwa kiasi kikubwa na hasa kutoa ripoti ya Usalama wa Taifa. Kwa hiyo, wakati mwingine wagombea lazima waanzie huko ili kujenga mazingira ya kuwa watawala,” amesema Kafulila.
Akizungumzia sababu za kurejea Chadema, chama ambacho kilimkuza na baadaye kumtimua, huku akitolewa maneno ya kejeli na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, akimfananisha na ‘sisimizi’, huku akimaanisha kwamba Kafulila hakuwa chochote ndani ya chama hicho.
Kafulila ambaye amekuwa akijinasibu kama mmoja wa vijana wa kizazi cha kuhoji, amesema amehamia Chadema baada ya kutafakari na kuona chama hicho ndicho chenye mipango ya kuchochea mabadiliko ya kweli na si vinginevyo.
Ikumbukwe kwamba akiwa NCCR-Mageuzi, baadhi ya vyama vya upinzani viliungana, vyama hivyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi pamoja NLD, huku vikitumia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Umoja huo ulianza wakati wa mchakato wa Katiba na baadaye ukaendelea mpaka kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.
“Nilikuwa na lengo kurejea Chadema tangu 2015, ila wakati huo ndiyo ilipoanzishwa Ukawa. Insigekuwa busara kujiunga wakati kuna mchakato huo, sikutaka kuingilia misingi ya utaratibu huo.
“Hata siku za hivi karibuni nikiwa NCCR-Mageuzi nimeshiriki shughuli mbalimbali za Chadema katika mikoa kadhaa na nilishiriki pia katika kampeni za mke wangu wakati huo akigombea ubunge Jimbo la Iramba. Tangu 2011 nimekuwa karibu sana na chama hicho kikuu cha upinzani,” amesema Kafulila.
Katika hatua nyingine, Kafulila amesema ushawishi mwingine ulianzia katika Jimbo lake la Kigoma Kusini, ambapo kuna baadhi ya wanachama waliomshawishi kuhamia Chadema, huku wakisema kasi yake itaendana na Chadema.
Kumekuwa na tuhuma za wanasiasa kununuliwa na kuhama vyama vya siasa, hilo halionekani kama ni sehemu ya mkakati uliomuondoa David Kafulila NCCR-Mageuzi na kuhamia Chadema. Kafulila amesema mpango wa namna hiyo ni mgumu kufanywa na vyama vya upinzani.
“Utaratibu wa kununuliwa kwa wapinzani ni mgumu kwa sababu wanaonunuliwa hupewa ahadi kadhaa na watawala, kwa hiyo hadi hapo ni vigumu kwa upinzani kwa sababu hawajafikia hatua ya kuwa watawala,” amesema Kafulila.
Akizungumza kuhusu kujiondoa Chadema, mwaka 2009, Kafulila amesema kujiondoa huko kulichangiwa na mgogoro uliokuwa ukifukuta ndani ya chama hicho, amesema kwa sasa mgogoro huo ni historia.
Mwanasiasa huyo kijana anayo imani kwamba ipo siku Tanzania itaongozwa na Rais atakayetokana na vyama vya upinzani, huku akitoa mfano wa hali kama hiyo kutokea kwenye nchi za Kenya, Nigeria, Ghana na hata Gambia.
“Rais John Magufuli alikuwa jaribio la mwisho kwa CCM kubaki madarakani. Kwa maoni yangu, CCM haikushinda uchaguzi, bali aliyeshinda ni Magufuli. Ndiyo maana kuna baadhi ya watu wanashangaa utawala wake,” amesema mwanasiasa huyo.
Kafulila anatoa ushauri kwa NCCR-Mageuzi kutumia fursa ya kuwa katika Ukawa kujiongezea nguvu na kujijenga zaidi kisiasa kwa kujiongezea wawakilishi katika ngazi zote.
“NCCR-Mageuzi itumie nafasi hii ya kuwa katika Ukawa kupata wawakilishi katika mitaa, vitongoji, madiwani na wabunge,” amesema Kafulila.
Umaarufu wa Kafulila
Kafulila alipata umaarufu mwaka 2014 akiwa mbunge, baada ya kutoa hoja bungeni kujadili ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya akaunti ya mabilioni ya Tegeta Escrow.
Baada ya mjadala huo baadhi ya mawaziri wakiwamo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.
Hata hivyo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Kafulila alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge, akishindwa na Husna Mwilima wa CCM. Alipinga matokeo mahakamani huku akishindwa Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora.
Pamoja na kupata umaarufu kupitia sakata la Escrow, Kafulila amesema sakata hilo hatalisahau katika maisha yake, jinsi lilivyompa wakati mgumu.
“Wakati wa sakata la Escrow nilikuwa silali kabisa na usalama wangu ukawa mdogo, ilifika hatua fulani nikawa tayari kwa lolote.
“Nakumbuka siku moja aliniita…… na kunihoji kuanzia saa 4 usiku hadi saa 8. Baadaye usiku huo wakaja watu wengine usiku huo kunihoji. Niliongea nao gizani na nakumbuka walikuwana magari matatu,” anasema Kafulila.
Kauli ya NCCR-Mageuzi
Akizungumza na JAMHURI, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju, amesema kuondoka kwa Kafulila hakujaacha pengo kwa sababu kuna watu wengi walishaondoka na chama kikaendelea kuwapo.
Juju ameiambia JAMHURI kwamba Kafulila ni mwanasiasa mwenye uzoefu, mtumiaji mzuri wa sanaa katika kuwasilisha hoja zake.
“Aliaga vizuri katika barua aliyotuandikia, naamini kuwa ataendelea kuwa mzuri. Bahati nzuri ameenda katika chama ambacho tunashirikiana nacho kupitia Ukawa,” amesema Juju.
Kauli ya Machali
Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini, Moses Machali, kupitia NCCR-Mageuzi, kabla ya kuhamia chama cha ACT-Wazalendo na baadaye CCM, amesema siyo dhambi kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine.
“Siamini suala la mtu kuwa mfungwa wa chama kimoja. Mimi binafsi naamini katika ukweli. Vyama vingi vya siasa vina watu waongo, ndiyo maana hata mimi niliamua kuhama kutokana na uongo niliokutana nao,” amesema Machali.
Akitoa maoni yake juu ya baadhi ya wanasiasa kutumiwa ili kudhoofisha vyama vingine, Machali anasema, ni vigumu kutambua kama jambo hilo linatendeka kweli na kuwa wakati mwingine ni mbinu za kisiasa.
“Wakati mwingine vyama vinahukumiwa kutokana na historia yake. Lakini pia vyama vyote vya siasa vina tabia ya kufanya propaganda kupitia wanasiasa maarufu na hasa inapokaribia wakati wa uchanguzi.
“Kwa ufupi sikubaliani na dhana ya wanasiasa kutumiwa, japokuwa ni jambo linalowezekana pia. Kama kuna wanasiasa wanaotumika kwa mtindo huo, kuna siku wataumbuka, kwa sababu huwezi kuwadanganya watu wote kwa wakati mmoja na siku zote ukweli haujifichi.
“Kwa mfano, miaka kumi iliyopita nilikuwa kati ya wabunge waliokuwa wakipigania haki na kupinga ufisadi. Kwa sasa baadhi yao wanashindwa kusifu jitihada zinazofanywa na Serikali ya sasa kukomesha vitendo hivyo,” amesisitiza Machali.
Alikotoka Kafulila
David Kafulila alizaliwa mwaka 1982 katika Kijiji cha Mtego, Tarafa ya Nguruka, mkoani Kigoma, mahali ilipo ngome yake kubwa kisiasa hadi sasa.
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Uvinza kabla ya kuhamia Shule ya Msingi Kinganamo, alipomalizia elimu hiyo.
Alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Wazazi Chumvi, kabla kujiunga Shule ya Sekondari ya Shinyanga. Baadaye alihitimu Shahada ya Biashara na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisoma kozi ya Uongozi katika Taasisi ya Wajerumani ya Fedrick Elbert Stiftung (FES) mwaka 2007. Alipata fursa nyingine ya kusomea kozi ya siasa na uongozi kwa vijana Afrika Mashariki katika Taasisi ya Marekani ya National Democratic Institute (NDI) 2009. Alisoma kozi nyingine ya uongozi katika Chuo cha Galile, nchini Israel mwaka 2014.
Kafulila anafafanua kuwa moja ya mambo yaliyomtia moyo hapo awali ni pamoja na tuzo alizowahi kupata zinazoashiria jitihada zake katika utendaji wake wa kazi.
“Nimebahatika kupata tuzo kimkoa mwaka 2002 ya mwanamazingira siku ya mazingira duniani ambayo kimkoa ilifanyika Kambi ya wakimbizi Rugufu, tuzo hiyo ilitolewa na shirika la kuhudumiwa wakimbizi duniani UNHCR.
“Mwaka 2015 nilipata tuzo ya Uongozi wenye maono chini ya Taasisi ya Dream Success ambapo nilikabidhiwa ngao na Mwanasheria Mkuu wa kwanza Mwafrika Serikali ya Tanganyika, Jaji Mark Bomani.
“Mwaka huo huo nilipata Tuzo ya Ujasiri katika vita ya Ufisadi kutokana na mchango wangu kwenye sakata la ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyotolewa na Taasisi Human Rights Defenders katika maadhimisho ya kufunga mwaka mbele ya ushiriki wa Balozi za Marekani na Ulaya zilizopo nchini Tanzania,” anakumbuka.
Safari yake kisiasa
Kafulila amekuwa mfuasi wa Chadema tangu mwaka 1994 akiwa Darasa la Nne, kijijini kwao Uvinza. Anasema alipata hamasa kubwa kutokana na vuguvugu la uchaguzi wa kwanza wa ubunge mwaka 1994 Kigoma mjini, baada ya Dk. Walid Kabourou kuja kugombea kupitia Chadema akitokea Marekani, na wakati huo Kigoma Kusini aliyekuwa anajiandaa kwa tiketi ya Chadema kwa ajili ya uchaguzi wa 1995 akiwa kijana, Kiffu Gulam Hussein.
Hussein alikuwa amemaliza masomo yake Chuo cha Mzumbe, lakini hakufanikiwa kushinda pamoja na kuleta upinzani mkubwa, badala yake alishinda katika uchaguzi wa mwaka 2000 kupitia NCCR-Mageuzi.
“Kwa kifupi hamasa ya Dk. Kabourou ilikuwa kubwa sana ingawa hakuijenga Chadema katika majimbo mengine zaidi ya Jimbo lake la Kigoma Mjini.
“Zaidi ya hamasa hiyo, pia nilikuwa mfuatiliaji sana habari za kitaifa na kimataifa katika umri mdogo, tangu nikiwa darasa la tano. Sikukubali kabisa kupitwa na taarifa za habari za BBC, DW na Sauti ya Amerika.
Mwaka 2005, Kafulila alikuwa kati ya vijana waliojihusisha na siasa Makao Makuu ya Chadema akiwa mmoja ya waratibu Uchaguzi Jimbo la Ubungo, ambapo John Mnyika aligombea na kushindwa na Charles Keenja.
Mwaka 2006, Kafulila alipata fursa ya kuwa Ofisa wa Vijana, kabla ya kukwaa cheo cha Afisa wa Habari na Chadema. Mwaka 2009 alijiunga NCCR-Mageuzi na kugombea ubunge Kigoma Kusini kwa mafanikio mwaka 2010.
“Nikiwa NCCR-Mageuzi nilikuwa Katibu Mwenezi Taifa kuanzia mwaka 2009 ingawa mwaka huo, nilijikita zaidi mkoani Kigoma, ambapo kwa mara ya kwanza NCCR ilivuna majimbo manne (Kigoma Kusini, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini na Muhambwe) kati ya manane, huku CCM wakiambulia majimbo matatu ya Kigoma Mjini, Buyungu na Kasulu Magharibi, wakati Chadema ikishinda Kigoma Mjini tu.