Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kadi za mpiga kura zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi (NEC) mwaka 2015 na 2020 zitaendelea kutumika kwenye chaguzi kuu zijazo. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima amesema wapiga kura wenye kadi hizo hawahusiki na utaratibu wa uboreshaji Daftari la kudumu la Wapiga Kura.’

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kadi za mpiga kura zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi (NEC) mwaka 2015 na 2020 zitaendelea kutumika kwenye chaguzi kuu zijazo. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima amesema wapiga kura wenye kadi hizo hawahusiki na utaratibu wa uboreshaji Daftari la kudumu la Wapiga Kura.

Kailima alisema hayo jana wakati wa ziara kukagua vituo vya kuandikishia wapiga kura katika Halmashuari ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

“Kwa wale ambao kadi zao ni zile zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wanadhania kuwa kubadilika kwa jina la tume kunasababisha kubadili kadi, watambue kuwa kadi zao ni halali kwa mujibu wa Kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024,” alisema Kailima.

Amesema wenye kadi zilizoharibika, zimepotea au wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine wanahusika kwenye uboreshaji Daftari la kudumu la Wapiga Kura.

“Nimebaini kuwa wapo wapiga kura wenye kadi za zamani zilizotolewa kabla ya mwaka 2015 (zile za karatasi) hao waje vituoni ili waandikishwe upya kwa kuwa mfumo uliotumika wakati huo ni tofauti na mfumo wa sasa,” alieleza Kailima.

Amewakumbusha wananchi wa mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi kuwa zimebaki siku tatu kumaliza kazi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye mikoa yao hivyo wajitokeze kuzitumia siku hizo. Uboreshaji wa daftari kwenye mikoa hiyo ulianza Julai 20, mwaka huu na utafanyika hadi Julai 26, mwaka huu. Vituo vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na vinafungwa saa 12:00 jioni