Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome amemuomba Msajili wa vyama vya siasa kutengua maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho yaliyofanyika Januari 22, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 08, 2025 jijini Dar es Salaam, Mchome amesema amewasilisha malalamiko kwa Msajili wa vyama vya siasa akilalamikia mambo mawili ambayo ni kutokutimia akidi katika Baraza kuu pamoja uwepo wa wasio wajumbe wa Baraza Kuu na kushiriki kwenye maamuzi kitu ambacho ni kinyume na Katiba ya Chama hicho.
“Tayari nimeshamwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu malalamiko haya ambapo nimemuomba kubatilisha Baraza Kuu lililoketi Januari 22, mwaka huu na viongozi wote nane walioteuliwa uteuzi wao ubatilishwe.
“Msajili aitake ofisi ya Katibu Mkuu iitishe Baraza Kuu upya ambalo litakuwa na akidi ya asilimia 75 ili kuweza kuwapitisha wajumbe hawa wa Kamati Kuu, cha muhimu wapatikane kwa njia sahihi na ambayo haitakuja kutuletea matatizo huko mbele,” amesema na kuongeza:
“Na ninashukuru tayari nimepokea nakala ya barua ambayo Msajili wa vyama vya siasa amemuandikia Katibu wa zamani John Mnyika kuhakikisha anatoa majibu ya malalamiko hayo ndani ya siku tatu. Nataka Watanzania waelewe nafanya haya kwaajili ya mapenzi mema ya chama, kukilinda pamoja na kukisaidia,” alisema.

Aidha Mchome amemtaka Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho, Tundu Lissu kukubali kukosolewa ili kukijenga Chama hicho.
“Chama chetu ni chama cha kidemokrasia, tumekuwa tukijinasibu kuwa ni chama cha kidemokrasia hivyo ni lazima tuwe mfano kuonesha demokrasia. Sasa leo ni kitu cha kushangaza kama tunakuwa na viongozi ambao wanajiita wana demokrasia lakini sio waumini wa demokrasia, tulikuwa na kiongozi aliyepita Mbowe, alikubali kupokea yote, alikubali kukosolewa, kusemwa na hakuna mahali alipotukana aliposemwa.
“Leo kwa masikitiko makubwa tuna kiongozi mkuu wa chama hakubali kukosolewa, kiongozi huyu ambaye alimwita Magufuli Dikteta uchwara, hayo aliyokuwa anayasema leo tunayaona kwake. Mwenyekiti wa chama ambaye unahubiri Demokrasia huna uwezo wa kupokea hata unaposemwa? hutaki kukosolewa umekuwa Mungu? kwanini tusikukosowe? kwanini tusilete hoja mbadala ambazo wewe kama Mwenyekiti wa chama taifa unapaswa ukae chini na kuziangalia.
“Hivyo nimuombe Mwenyekiti wangu akubali kukosolewa ili tuijenge Chadema imara na ule umoja wetu tuliokuwa nao awali. Mwenyekiti ayapokee maana siasa lazima uwe na ngozi nene na kama huwezi kuwa na ngozi nene achana na siasa,” amesema.
Vilevile, amesema anapingana na kauli ya Chama hicho kutokushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwani hatua hiyo itaua chama.

“Chama hiki tumekijenga kwa jasho kubwa sana wengine tumekuwa wahanga wakubwa katika kukijenga chama hiki, hatuwezi kukubali kuona chama hiki kinaenda kufukiwa kwenye kaburi.
“Kama tunaweza kutumia nguvu kuzuia uchaguzi usifanyike ni bora tutumie hizo nguvu kulazimisha tushinde uchaguzi na tukishinda tutangazwe,” amesema.