Kachero mstaafu wa Jeshi la Polisi, Thomas Njama, ambaye anadai mafao yake yaliyoyeyuka katika hali ya kushangaza, amerudishwa tena Jeshi la Polisi ambako ameambiwa ndiko anakoweza kupata ufumbuzi wa suala lake.

Hatua hiyo imekuja baada ya Njama kukutana na maofisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taasisi za Umma (PSSSF) ambao baada ya kupitia nyaraka zake walimweleza kuwa Jeshi la Polisi ndilo lenye uwezo wa kumpatia ufumbuzi wa madai yake hayo.

Hatua hiyo imemweka Njama kwenye wakati mgumu kwani analalamika kuwa sakata hilo lote limetokana na maofisa wa Jeshi la Polisi kutengeneza vielelezo bandia ili wafanikiwe kuhujumu mafao yake ya kustaafu.

Njama ambaye amestaafu utumishi wa jeshi hilo Julai 2015 anaidai PSSSF mafao yanayofikia Sh 47,162,559 lakini hadi sasa hajalipwa chochote.

Njama alitengenezewa kesi ya mauaji, akafungwa na anadai kuwa wakati akiwa gerezani baadhi ya maofis katika Jeshi la Polisi walitengeneza nyaraka bandia na kumfungulia akaunti ya hifadhi ya jamii katika uliokuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Serikali (GEPF) wakati tayari alikuwa anachangia katika uliokuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSPF). Mifuko hiyo miwili imevunjwa kutokana na mabadiliko ya sheria ambayo yameiweka mifuko yote inayohusu watumishi wa umma chini ya PSSSF.

“Ni kweli nilikwenda Dodoma kwenye ofisi za makao makuu ya PSSSF na nilikutana na maofisa wao. Baada ya kuzipitia nyaraka zangu walinieleza kuwa Jeshi la Polisi ndio wanaweza kulimaliza suala langu kwa sababu wao ndio walikuwa waajiri wangu,” ameeleza Njama.

Baada ya kurejea kutoka Dodoma, Njama amesema alikwenda kuonana na Afisa Utawala wa Jeshi la Polisi aliyemtaka kuandika maelezo.

Amesema aliyaandika maelezo hayo na kuyapeleka na akaelezwa kuwa atajibiwa.

“Lakini hawajaniambia chochote hadi leo, ninasubiri majibu yangu,” ameeleza Njama.

Kabla Njama hajakwenda Dodoma, Jeshi la Polisi lilishaeleza kuwa haliwezi kumlipa mafao hayo kwani vielelezo vinaonyesha kuwa baada ya kuachiwa kutoka gerezani Njama alikubali kulipwa bakishishi badala ya pensheni.

Lakini Njama anavikana vielelezo hivyo akisema vimebeba taarifa za uongo dhidi ya utumishi wake, akidai kuwa vimetengenezwa wakati alipokuwa mahabusu kwa tuhuma za kuua mfungwa.

Mathalani, anadai kuwa katika nyaraka alizonazo hati inayoonyesha mwenendo wa makato ya uanachama wake iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda GEPF mwaka 2015 yenye taarifa za uanachama wa Njama imejaa upungufu.

Hati hiyo aliyopewa na GEPF Agosti 24, mwaka 2015 inayoonyesha kuwa amejiunga na mfuko wa GEPF Januari 1, 1960 kipindi ambacho kwa mujibu wa hati yenyewe alikuwa hajazaliwa.

Kama hilo halitoshi, hati hiyo inaonyesha kuwa alijiunga na GEPF miezi sita kabla hajazaliwa, kwani inaonyesha alizaliwa Julai 1, 1960.

“Hii nyaraka nimepewa na GEPF wenyewe, ina maana taarifa zilizojazwa na polisi kwenye hati hii ni za uongo. Naamini walifanya hivi wakiamini kuwa mimi sitatoka gerezani, wakaanza kuchezea taarifa za msingi kuhusu kustaafu kwangu lakini hawakuwa makini,” amesema Njama.

Hati hiyo inaonyesha Njama amelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 43 na siku 23, ilhali utumishi wake halali katika jeshi hilo ni miaka 37.

Amehoji kama nyaraka hiyo ya GEPF inamtambua kuwa mwanachama tangu mwaka 1960 mahesabu ya kuchangia mfuko huo kwa miaka 16 waliyatoa wapi?

“Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa hati hii, GEPF ilitakiwa niwadai kiinua mgongo changu tangu mwaka 1960 wanaposema nimejiunga kuwa mwanachama wao,” amesema Njama.

Amekiri kuwa alilipwa Sh 7,767,884 na GEPF kama kiinua mgongo lakini anaamini kuwa kiasi hicho kilikadiriwa tu kwani taarifa walizotumia kuhalalisha malipo hayo haziko sahihi.

Aidha, Njama anamiliki hati mbili za kustaafu kazi, moja ikionyesha kuwa amestaafu kazi Januari 23, 2003 na nyingine kuonyesha kuwa amestaafu kazi Julai 2015.

“Nina hati mbili kwa sababu moja iliandaliwa wakati nikiwa gerezani ili wapange namna ya kuiba fedha zangu, wakaamua kunistaafisha. Kama wasingefanya hivyo ina maana pesa zangu zingechukuliwa na serikali na kurudishwa hazina, hivyo wasingeweza kuzipata, sasa ili wazipate ilibidi wacheze na nyaraka zangu,” amesema Njama.

Lakini Jeshi la Polisi nalo linasema nyaraka alizonazo Njama ni za kughushi, wakati zile walizonazo wao zina makosa ya kiuandishi.