Mwishoni mwa mwaka jana Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga, alifanya ziara ya siku moja nchini Burundi ili kuangalia hali ya huko kuhusu vurugu zinazoripotiwa. Aliporudi alieleza kuridhishwa na “hali ya utulivu” aliyoikuta Burundi.

Waziri alisema: “Kulikuwa na utulivu na watu waliendelea na shughuli zao…sikusikia mlio wa risasi na sikuwa na haja ya kusindikizwa na polisi kwenye ziara… labda kama ni mikoani, lakini jiji (Bujumbura) lilikuwa tulivu.”

Balozi Mahiga pia alisema Serikali ya Burundi ilimhakikishia kwamba inashiriki kikamilifu katika mazungumzo ya kurejesha amani yanayofanyika nchini Uganda. Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pia zinashiriki.

Wengine walioalikwa ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Mataifa (UN) na Marekani.

Ziara hiyo ya Balozi Mahiga ilitokana na agizo la Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa EAC, kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa ulioikumba Burundi kutokana na makundi yanayompinga Rais Pierre Nkurunzinza kuongoza awamu ya tatu baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Julai, mwaka jana.

Mie sina hakika iwapo ziara ya siku moja ya Balozi Mahiga inatosha kujua iwapo kuna utulivu au machafuko nchini. Pia kama kuna utulivu, kwanini yafanyike mazungumzo ya kurejesha amani? Lakini ndivyo tulivyoelezwa.  

Pia ni vizuri tukajiuliza iweje katika amani ya Burundi inayozungumziwa nchini Uganda waalikwe wajumbe kutoka Ulaya na Marekani? 

Kuna wasiwasi kuwa mgogoro huu unaweza ukaibua tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yaliendelea kuanzia 1993 hadi 2006. Wakati huo wananchi wa Kihutu walio wengi nchini walipambana na jeshi lililokuwa na Watutsi wengi. Matokeo ya mapigano haya ni kupotea kwa roho za raia 300,000.  Hii ndio Burundi ambayo leo inakumbukwa kwa masikitiko makubwa.

Mapigano  hayo yalimalizika baada ya makubaliano ya Arusha yaliyosainiwa na pande zilizokuwa zinapingana. Walikubaliana kuunda jeshi la pamoja na serikali ya mpito iliyoongozwa na Nkurunziza.

Sasa mgogoro umeanza upya tangu Aprili mwaka jana wakati Rais Nkurunziza  alipotangaza nia yake ya kugombea urais kwa muhula wa tatu ambao yeye anasema ni wa pili. Anadai muhula wa kwanza ni ile serikali ya mpito. Hata hivyo, Mahakama ilikubaliana naye na kusema kuwa ana haki ya kugombea kwa vile katiba inamruhusu. Wapinzani walipinga na kusema jopo la majaji lililazimishwa kutoa uamuzi huo, hasa kwa vile mmoja wa majaji hao aliamua kutoroka nchini kwa vile alipinga uamuzi huo.

Mara moja baadhi ya makamanda wa jeshi walifanya jaribio la kuipindua serikali ya Nkurunziza. Walishindwa na Julai, 2015 uchaguzi ukafanyika na Nkurunziza alitangazwa mshindi. Wapinzani wakayakataa matokeo.

Alimradi nchi imekosa utulivu. Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Amnesty International) limeripoti kuwa Desemba 11, mwaka jana majeshi ya serikali yaliwashambulia wananchi  katika Jiji la Bujumbura. Ripoti hiyo inasema watu wasiopungua 87 waliuawa, wanane wakiwa wanajeshi. Kwa ujumla watu zaidi ya 300 inasemekana wamekufa tangu Nkurunziza kuchaguliwa.

Aidha, zaidi ya watu 220,000 wamelazimika kuikimbia nchi yao na kwenda nchi za jirani kama Tanzania. Wengine wengi wamegeuka wakimbizi ndani ya nchi yao. Machafuko kama haya kwa hivyo hayawezi yakawa ya nchi moja peke yake. Ni lazima nchi za jirani zitahusika kwa namna moja au nyingine. Burundi ni mwanachama wa EAC. Ndio maana jumuiya hiyo imeamua kuingilia kati na kusuluhisha. EAC imemteua Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuzikutanisha pande husika.

Mwishoni mwa Desemba, mwaka jana Waziri wa Ulinzi wa Uganda alisema makundi 14 yalitarajiwa kushiriki mjadala jijini Kampala. Ni pamoja na chama tawala, vyama vya upinzani na asasi za kiraia. Mipango imefanywa pia kwa ajili ya mazungumzo mjini Arusha yakifuatiwa na mkutano wa marais wa nchi za EAC chini ya uwenyekiti wa Rais Magufuli.  

Kuna watakaouliza iwapo EAC itafanikiwa kuwasuluhisha Warundi wanaozozana. Makubaliano ya Arusha yalitiwa sahihi na pande zote baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wengine wa Afrika.  Yote haya yamesahauliwa; na kwa mara nyingine Tanzania na nchi za EAC zinaitisha mikutano ya usuluhisho.

Lakini huo ni wajibu wetu. Mgogoro wa Burundi ni dhahiri unazigusa nchi jirani.  Nchi ya kwanza ambayo itaathirika ni Rwanda kwa sababu nchi hizi mbili zinafanana kihistoria, kitamaduni na kikabila. Ndio maana Rais Paul Kagame wa Rwanda aliingilia kati na kumtaka Rais Nkurunziza asigombee muhula wa tatu. Lakini tatizo ni kuwa Rais Kagame mwenyewe hataki kuachilia kiti cha urais. Atawezaje kumshauri mwenziwe?

Nchi ya pili inayohusika moja kwa moja ni Uganda ambako Rais Museveni ameitisha mkutano akiwa msuluhishi. Tangu Julai, mwaka jana aliteuliwa na EAC awe msuluhishi. Lakini na Rais Museveni naye anaendelea kukalia kiti. Mwaka 2005 alibadili katiba ili imruhusu kuendelea kukaa madarakani. Hivyo na yeye naye si rahisi kumshauri Rais Nkurunzinza ang’atuke.

Labda Rais Magufuli ataweza kumshauri. Lakini tatizo la Tanzania ni kuwa inaonekana ina kigeugeu. Hapo awali ilimwambia Nkurunziza aachie kiti. Lakini baadaye ikamnyamazia kimya. Kwa vyovyote vile, itabidi EAC iwasuluhishe Warundi kama alivyofanya Mwalimu.

Kuna wanaosema njia pekee ni kutumia majeshi. Hii si rahisi hata kidogo. Tuangalie Somalia jinsi majeshi ya nje yalivyozama katika matope, yakishindwa kujitoa na yakishindwa kuzuia machafuko. Nadhali Somalia moja yatutosha.

Hata hivyo, AU imeamua kutuma majeshi ya usalama yatakayoitwa Kikosi cha Kiafrika cha Kulinda Usalama nchini Burundi (African Prevention and Protection Mission in Burundi au MAPROBU). Wameamua hata jina. Na huo usalama watakaoulinda uko wapi?

Kikosi hiki kitakuwa na wanajeshi 5,000. AU eti imetoa siku nne kwa Serikali ya Burundi kukubaliana na uamuzi huu, la sivyo kikosi kitapelekwa bila ya idhini ya Serikali. Swali ni je, AU inaweza kutuma majeshi bila ya idhini ya nchi husika?  Katiba ya AU kifungu cha 4 (h) inaruhusu AU kuingilia kati kijeshi kama nchi inakabiliwa na mauaji ya halaiki au uhalifu wa kijeshi au uhalifu dhidi ya mwanadamu. Ni nani wa kuamua iwapo Burundi imeingia katika hali hii? Tumemsikia Waziri Mahiga akisema kuna utulivu. Na Nkurunziza naye ametangaza kuwa anakataa wazo la AU kutuma majeshi yake. Amesema huo utakuwa ni uvamizi wa kijeshi usiokubalika katika nchi huru inayojitawala kama Burundi.

Bunge la Burundi nalo limekubaliana naye kwa kukosoa uamuzi wa UN. Bunge liliitaka serikali isikubali nchi kurubuniwa na AU wakati kuna ‘utulivu’ nchini. Wabunge pia walilaani kuingilia kwa nchi za magharibi katika mambo ya ndani ya Burundi.

Hili suala la nchi za magharibi kujiingiza katika mambo ya Burundi linahitaji maelezo.

Burundi ina madini aina ya nikeli (nickel) ambayo inaongoza katika ubora wake duniani. Utajiri huu unamezewa mate na kampuni za kimataifa ambazo zinataka kuudhibiti. Kampuni za Marekani zimekuwa zikifanya bidii kudhibiti nikeli ya Burundi, lakini serikali ya huko imesaini mkataba na kampuni ya Urusi. Jambo hili limeikasirisha sana Marekani. 

Ni katika muktadha huu ndipo tunaelewa mbinu za magharibi kutumia majeshi huko Burundi. Si kwa kutumia majeshi yao, bali kwa kupitia nchi za Kiafrika.

Asasi ya kutatua migogoro ya kimataifa iitwayo International Crisis Group (ICG) imependekeza kwa Marekani na nchi nyingine za magharibi zifadhili kikosi cha Afrika cha kulinda amani huko Burundi. Ndipo Marekani na EU zimekuwa zikizishawishi nchi za Kiafrika kutuma majeshi Burundi. Baraza la Usalama na Amani la AU limekubali pendekezo ambalo linapingwa na nchi za EAC na za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). 

Ndipo tunaelewa kwanini suala la Burundi linapozungumzwa na Waafrika mkutano huwa unahudhuriwa na Marekani na EU. Hii haifanyiki huko Burundi tu, bali katika Bara zima la Afrika.  

Ni kwa sababu Marekani na wenzake wa Ulaya (EU) wana maslahi yao ya kiuchumi na kisiasa barani Afrika, na ndio maana wametandaza majeshi yao kote. Mfano ni hiki kikosi cha Marekani kiitwacho Africom. Madhumuni yao ni kulinda maslahi ya kibeberu, lakini lugha wanayotumia ni kuwasaidia watawala wa Afrika kulinda na kutunza amani katika nchi zao. Na mara nyingi hutumia bendera ya UN ili kufunika mbinu zao zisijulikane kwa urahisi.

Wanapofanya hivyo hutumia watawala wa Kiafrika na jumuiya zao kama AU au Ecowas kule Afrika Magharibi. Angalia jinsi nchi za magharibi zinavyofadhili majeshi ya “kulinda amani” kule Somalia (AMISOM). Na ndivyo ilivyokuwa kule Afrika Magharibi na DRC. Sasa wanataka kupeleka majeshi Burundi. 

Tumeona kuwa Rais Magufuli akiwa Mwenyekiti wa marais wa EAC ana jukumu la kushughulikia mgogoro wa Burundi kama nchi mwanachama. Lakini rais wetu anamaliza miezi miwili na hajatoka nje ya nchi. Ameamua kushughulikia ‘majipu’ yaliyo ndani ya nchi. Sasa anakabiliwa na ‘jipu’ la Burundi. 

Wakati huo huo Magufuli anakabiliwa na mgogoro uliozuka Visiwani Zanzibar kutokana na kufutwa kwa uchaguzi. Mgogoro huo umechukua sura ya kimataifa kutokana na mabalozi wa magharibi nao kujiingiza. 

Mwaka jana wakati Nkurunziza alipoonyesha nia ya kubaki madarakani, msimamo wa Tanzania ulikuwa kuwa alipaswa kuheshimu katiba ya nchi na makubaliano ya Arusha. Tulitoa hata risala rasmi Machi 2015 tukimwambia Nkurunzinza aheshimu kikomo cha urais.

Hata hivyo, Nkurunziza hakujali na akagombea uchaguzi. Mara moja Tanzania ikaonekana ikibadili msimamo wake na hata ikatuma waangalizi wa uchaguzi. Mataifa na mashirika mengi kama UN na AU yalikataa kutuma waangalizi ili kuonyesha kuwa hawakubaliani na Nkurunziza.

Ndio maana si jambo la kushangaza kuwa Tanzania inapinga kuingizwa kwa majeshi ya AU huko Burundi na badala yake inajaribu kusuluhisha kwa njia ya amani; jambo ambalo ni sahihi kwa wakati huu.

Labda mara hii tutahitaji tena wazee kama Mwalimu Nyerere au Mzee Nelson Mandela ambao walisaidia sana kusuluhisha wakati ule.  Je, Magufuli ataweza kuvaa viatu vyao?