*Waasi wakimbilia porini, washindia matunda mwitu
*Zuma atoa makombora yatumike ikiwa wataendelea
*Hatima yasubiriwa Uganda, silaha njaa kuwatoa porini
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na majeshi washirika ya kimataifa, limewafurumusha askari wote wa kundi la M23 kutoka katika ardhi ya Mji wa Goma, uchunguzi umebaini.
Ukiacha hali hiyo ya waasi wa M23 waliokuwa wanasumbua kwa kuranda na kufyatua risasi hovyo usiku na mchana, habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi hili linaloongozwa na JWTZ, zinaeleza kuwa waasi sasa wanabembeleza kipigo walichokipata Agosti 21, kisirejewe.
“Mazungumzo yanayoendelea Uganda kati ya Serikali ya Rais Joseph Kabila na waasi wa M23, ni wazi yatahitimishwa kwa kumaliza vita. Kinachoendelea ni malalamiko kwenye mazungumzo hayo tu kuwa askari wa Tanzania wanawachapa kupita kiasi,” alisema mmoja wa washiriki wa vikao vinavyoendelea jijini Kampala.
“Wamepata mshituko, hawakutarajia. Walikuwa hawaijui Tanzania na ndiyo maana Umoja wa Mataifa umeona ni bora kikosi hiki kiongozwe na Tanzania kutokana na uzoefu wa Anjuan, Lebanon, Darfur na maeneo mengine ambapo majeshi ya Tanzania yanalinda amani. Mara zote, majeshi yetu yamefanya kazi ya kupigiwa mfano,” kilisema chanzo kingine.
Habari za uhakika kutoka ndani ya JWTZ Tanzania, zinasema kuwa pamoja na mazungumzo kuendelea nchini Uganda, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ametoa makombora ya masafa marefu yanayoweza kusafiri hadi kilomita 1,000 kutoka eneo yaliporushiwa, yakasaidie kufurusha zaidi waasi msituni.
“Ametoa makombora haya yako standby (tayari tayari). Ikiwa mazungumzo yatavunjika, basi yatatumiwa kuwafyekelea mbali huko huko msituni waliko,” kilisema chanzo cha uhakika.
“Tunapata wakati mgumu kweli. Askari wetu wanafika mahala wanasema waruhusiwe wakasafishe hadi hao waliokimbilia misituni, sisi tunawaambia tulieni tu. Tusubiri mazungumzo ya Uganda yaishe, ila kwa kila hali lazima M23 wasalimishe silaha. Wasiposalimisha, hakuna msalie Mtume, hapo tutawachapa vilivyo hao wachache watakaokuwa wamesalia,” kilisema chanzo chetu.
Nchi za Afrika Kusini, Malawi na Msumbiji zinaunda Jeshi la Umoja wa Mataifa linaloongozwa na Tanzania ambalo lipo DRC kuhakikisha linawanyang’anya silaha waasi wa M23, ambao kama si kuingia kwa jeshi hili linaloongozwa na Tanzania walikwishatamba kuiangusha Serikali ya Rais Kabila.
Hadi wiki iliyopita, waasi wa M23 wapatao 1,000 walikuwa wakishikiliwa kama mateka, hali iliyowafanya wakubali mazungumzo na Serikali ya Rais Kabila. Hata hivyo, kwa sasa wanajitutumua wakidai kuwa lazima waingizwe serikalini na kupewa vyeo, vinginevyo DRC haitatawalika, kitu kilichotajwa na JWTZ kuwa ni upuuzi mtupu.
M23 wamelazimika kurudi nyuma baada ya kupigwa na Majeshi ya Umoja wa Mataifa (FIB) yanayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hali iliyowafanya wakubali mazungumzo wakati walikwishakataa katakata kuwa wasingezungumza na yeyote hadi Rais Kabila aondoke madarakani.
Habari kutoka kwenye uwanja wa mapambano zinasema M23 wamepoteza mwelekeo na kukimbia kutoka kwenye ngome yao ambayo wameishikilia kwa muda mrefu.
“Hivi sasa tuko katika kambi yao na tunawashikilia waasi zaidi ya 1,000 wengine wamekimbia, wametawanyika wengine wako msituni hawajui nini cha kufanya,” kimesema chanzo chetu kutoka Goma.
Chanzo chetu kiliongeza kusema kuwa JWTZ na washirika wake wa kijeshi wanachofanya sasa ni kuhakikisha hakuna chakula kinachokwenda huko porini, mafuta ya magari au silaha.
“Wee waache tu. Watakula hizo biskuti na chakula chote walichonacho huko msituni kiishe. Watakula mizizi iishe, njaa itawatoa tu. Tunaangalia kwa karibu isitokee wakatumia ndege, magari au usafiri wowote kuingiza chakula huko msituni. Hii nayo ni silaha nyingine. Njaa itawatoa au watakufa na mizoga yao kuliwa na wanyama,” kilisema chanzo chetu hapa mjini Goma.
Wakazi wa Goma wamezidi kulishukuru Jeshi la Tanzania wakisema kwa kushirikiana na majeshi ya nchi nyingine, amani sasa imerejea. “Usitaje jina langu, maana sijui kama [M23] wameondoka kweli, lakini kwa sasa tunacheza disko hadi usiku. Tunakunywa Simba (bia inaitwa Simba) kisha tunalala bila kusikia milio ya risasi. Kwa hili tunasema asante Tanzania,” alisema mwananchi wa Goma.
Mapigano makali yaliyotokea Agosti 21 hadi Agosti 24 katika vijiji vya Mutaho na Kibati, umbali wa kilometa zaidi ya 20 kutoka Goma, ni ya kihistoria.
Mapigano hayo makali yaliibuka baada ya kuuawa kwa Meja Khatib Shaaban Mshindo wa JWTZ, na wanajeshi wengine kujeruhiwa.
Ofisa mwingine ameiambia JAMHURI wiki hii kuwa tukio la mauaji ya Meja Mshindo liliwakasirisha mno wanajeshi wa JWTZ na wanajeshi wa nchi mbalimbali chini ya Jeshi la Kimataifa la MUNUSCO, wakaamua kutumia mamlaka waliyopewa chini ya Sura ya VII ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuwasambaratisha waasi hao.
“Hawana hamu,” kilisema chanzo chetu na kuongeza: “Walidhani na sisi tunashindia maziwa kama wao huko msituni, tumewachakaza vilivyo. Sasa tunawasubiri wachokoze tena kidogo tu, tumalizie kazi.”
Hadi tunakwenda mtamboni, ilikuwa haijatolewa taarifa rasmi kutoka nchini Uganda yanakoendelea mazungumzo juu ya nini kimeafikiwa, ila kubwa ni utulivu na amani jijini Goma.
“Angalia hapa baa ya Lashante, watu wanakunywa na kusaza. Ilikuwa hakuna muziki siku za nyuma. Furaha ilikuwa imeondoshwa. M23 walikuwa wanafika na kuchukua mabinti kwa nguvu na ukikataa unauawa, lakini sasa nasi tunajiona si binadamu daraja la pili. Tunasema, asante Tanzania,” mwananchi mwingine wa Goma aliiambia JAMHURI.