Kikosi maalumu cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kimepelekwa katika wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, kukabiliana na genge la majahili linaloendesha mauaji ya askari, viongozi na wananchi wasio na hatia.

Kikosi hicho kinatajwa kuundwa na wanajeshi wenye uzoefu wa hali ya juu katika medani za kivita, kikijumuisha makomando.

Habari za uhakika kutoka serikalini zinasema kupelekwa kwa JWTZ kunatokana na aina ya mapambano yanayoendeshwa na wauaji, na kufikia uamuzi wa kupeleka askari wenye uwezo wa kukabiliana nao vilivyo.

“Askari wa JWTZ wanaungana na askari polisi, na tayari kazi imeshaanza. Matarajio yetu ni kuona mauaji haya yanakomeshwa ili kuona wananchi wanarejea kwenye shughuli zao kama kawaida,” kimesema chanzo chetu kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Hii si mara ya kwanza kwa JWTZ kuongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya wahalifu. Mwaka 1998 Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha ilivamiwa na majangili raia wa Somalia waliokuwa na silaha kali.

Polisi wetu walipambana na majangili hao kwa miezi kadhaa bila mafanikio. Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) hiyo aliuawa, huku vitendo vya uporaji na mauaji kwa watalii vikifanywa.

Kwa kuona hali hiyo, ndipo uongozi wa juu wa nchi ulipoamuru kipelekwe kikosi maalumu cha wapiganaji na makamanda wa JWTZ. Kazi kubwa ilifanywa na kikosi hicho, ikiwa ni pamoja na ‘kuwafyeka’ majangili hao. Tangu wakati huo Ngorongoro imetulia.

Wananchi waliozungumza na JAMHURI katika maeneo ya Mkuranga, wameeleza furaha yao kwa ujio wa JWTZ.

“Sasa tumeingiwa na furaha, tunaamini watashirikiana na polisi kutokomeza mauaji haya, tuna imani kubwa na Serikali,” amesema mwananchi mmoja.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amezungumza na JAMHURI, lakini hakuwa tayari kukanusha wala kukubali kuhusu uwepo wa askari wa JWTZ katika ‘uwanja wa mapambano’.

Amesema: “Itaniwia vigumu kueleza hili suala kwa sababu sijaletewa taarifa rasmi. Naomba wananchi wawe na subira hadi tutakapotoa taarifa rasmi. Kwa sasa si wakati wake kulizungumzia.”

Kwa upande wake, Msemaji wa JWTZ ambaye pia ni Mkuu wa Utumishi katika JWTZ, Meja Jenerali Harrison Masebo, amezungumza na JAMHURI kuhusu ushiriki wa wanajeshi kwenye operesheni hiyo, lakini amekataa kuingia katika undani wake kwa maelezo kuwa sharti apate maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, ACP Advera Bulimba, ameulizwa kuhusu kuongezwa nguvu kulikofanywa na JWTZ, na kusema ni vigumu kulizungumzia suala hilo kwani lipo chini ya Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Pwani, Onesmo Lyanga.

“Wasiliana na RPC wa Pwani ndiye anaweza kuzungumzia hilo maana ni mkoa wake. Huyo ana mamlaka ya kuzungumzia…suala hili linahusu mkoa,” amesema Bulimba.

Kamanda Lyanga amezungumza na JAMHURI na kusema kwa sasa hawezi kusema chochote kinachoendelea Rufiji.

JWTZ imekuwa na rekodi ya kufanya vizuri katika medani za mapambano kitaifa na kimataifa. Hatua yake ya kwenda kuongeza nguvu mkoani Pwani, inaakisi maudhui ya kuasisiwa kwa Jeshi hilo.

Mei 18, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, lilitangaza majina ya watuhumiwa 12 wanaodaiwa kuratibu na kutekeleza mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Anatajwa Abdurshakur Ngande Makeo, kuwa ndiye mwasisi wa mauaji hayo.

Alieleza, Jeshi la Polisi limewabaini kwa majina na picha kwa baadhi yao ambao aliwataja watuhumiwa kuwa ni:

1: Faraj Ismail Nangalava

2: Anaf Rashid Kapera

3: Said Ngunde

4: Omari Abdallah Matimbwa

5: Shaban Kinyangulia

6: Haji Ulatule

7: Ally Ulatule

8: Hassan Uponda

9: Rashid Salim Mtulula

10: Sheikh Hassan Nasri Mzuzuri

11: Hassan Njame

Kati ya watuhumiwa hao, watuhumiwa wane picha zao zilikwishapatikana. Nao ni Saidi Ngunde anayetajwa kuwa na makazi Ikwiriri; Omari Abdallah Matimbwa, anayeishi Dar es Salaam pamoja na Faraj Ismail Nangalava na Anaf Rashid Kapera. “Jeshi letu limebaini majina hayo kwa kushirikiana na wasiri wetu huku tukiendelea na uchunguzi zaidi,” amesema.

Watuhumiwa hao inasemekana wamekuwa wakipenda kutembelea maeneo ya Kisiwa cha Simbaulanga na katika Kisiwa cha Saninga ambako kuna Kijiji cha Nchinga.

Maeneo mengine ni Kijiji cha Mfesini, Kata ya Nyamisati na maeneo mengine ya wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

Wauaji hawa ni nani?

Matukio ya mauaji haya ya kutumia silaha dhidi ya polisi, viongozi wa vijiji na wananchi katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji yanahusishwa na vikundi vya vijana wanaopata mafunzo kutoka kwenye kundi la al-Shabaab nchini Somalia.

Kwa miaka minne hadi mitano iliyopita, vijana kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Rufiji, hasa Ikwiriri, wamekuwa wakisajiliwa na kundi hilo la kigaidi, huku wazazi wao wakiambulia ujira wa dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 6).

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wakazi wa Ikwiriri ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini kwa sababu za kiusalama, amesema kumekuwa na wimbi la vijana wenye umri wa miaka 16-25 kupelekwa kwenye mafunzo huko Somalia.

“Hapa Ikwiriri katika kipindi cha miaka kama mitano iliyopita kumekuwa na wimbi la vijana wadogo kupelekwa Somalia. Inasemekana wanakwenda kujiunga na kikundi cha al-Shabaab, lakini vijana hao wamekuwa wanapatikana kupitia kwa mawakala kadhaa kwenye misikiti.

“Si kweli kwamba polisi hapa Ikwiriri hawajui, maana hata ukifuatilia wale viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakitoa taarifa za vijana hao wamekuwa wakiuawa kwa staili inayofanana… sasa hapo unaweza kuona namna zoezi (kazi) linavyokuwa gumu,” amesema.

Chanzo chetu kingine kimemtaja mtu ambaye jina lake tunalifupisha kama S.B., kuwa ndiye hufanya kazi ya udalali wa kuwapeleka vijana hao nchini Somalia, huku wazazi wa watoto hao wakiambiwa kuna ajira huko.

Chanzo hicho kimesema hata baada ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji kupeleka taarifa za uhusika wa S.B, kilichofuata ni mauaji.

“S.B. alipotea hapa Ikwiriri kwa takribani miaka mitatu, hata baada ya kurejea amekuwa na mali nyingi ambazo si za kurithi na haziendani na utafutaji wa halali katika kipindi hicho kifupi. Yamekuwa yanasemwa mengi, lakini ukimgusa andaa sanda kabisa,”  kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limedokezwa kuwa vijana zaidi ya 30 kutoka maeneo mbalimbali wilayani Rufiji, wamechukuliwa kwenda kujiunga al-Shabaab, chini ya udalali wa Bwana S.B.

Chanzo hicho kimesema mmoja na vijana ambaye alichukuliwa alishindwa aina ya kazi na akarudi.

Habari ambazo JAMHURI limezipata zinaonesha kuwa kikundi hicho cha wauaji kimekuwa kikimtumia mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka 18, kuwapelekea chakula huko msituni eneo la Mparange wilayani Rufiji. Jina la mtoto huyo tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma.

“Kijana huyo mdogo amekuwa akitumiwa na hao wauaji kuwapelekea chakula. Mtoto huyo amekuwa akiwahudumia pasipokuwa na simu. Akikamatwa huyo anaweza kusaidia sana upelelezi wa polisi… hapa kila mtu amejaa hofu kuhusu usalama,” kimesema chanzo chetu.

 

Hali ilivyo Mkuranga, Kibiti na Rufiji

Hali ya usalama katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji imezidi kuwa ya wasiwasi, huku vyombo vya usalama vikiweka zuio katika maeneo hayo.

Baadhi ya mazuio hayo ni kupiga marufuku kuendesha pikipiki kuanzia saa 12:00 jioni, wananchi hasa maeneo ya Ikwiriri wilayani Rufiji wamekuwa wakitakiwa kulala mapema.

Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando, ameliambia JAMHURI kuwa hali si nzuri kutokana na ukweli kwamba wananchi hata yeye mwenyewe wako katika sintofahamu ya kiusalama.

Ungando anasema yeye binafsi yuko kwenye hatari. “Naomba nisiwe mzungumzaji maana mwenyewe niko katika ‘danger zone’ viongozi wangu wa vijiji wanauawa, huoni kwamba anayefuata hapo ni mimi? Nisingependa kulizungumzia hata kidogo, unanitafutia balaa, sitaki kuongea kwenye vyombo vya habari, maana nikiongea utaandika kwenye magazeti, na hao wenzetu (wauaji) wanasoma. Hapa mimi nasubiri hatima yangu.”

Wakati Mbunge wa Kibiti, akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, yeye amesema hawezi kuzungumzia jambo hilo, badala yake anasubiri uchunguzi wa vyombo vya dola ukamilike.

 

Matukio la Kibiti

Polisi wanane wameshauliwa wakiwa kazini. Tukio la kuuawa kwa askari wanane limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia baibui.

Wanaume hao ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vizuizi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.

Mei, 2016

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Saidi Mbwana, aliuawa kwa kupigwa risasi.

Oktoba, 2016

Aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu, aliuawa baada ya kuvamiwa na watu wanne waliompiga risasi mbili.

Novemba, 2016

Wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, 2017

Mfanyabiashara Oswald Mrope aliuawa kwa kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017

Watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga, na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kutoroka.

Februari 24, 2017

Watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

April 13, 2017

Polisi wanane waliuawa na watu wasiofahamika katika kijiji cha Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti. Inspekta Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson, H.5503 PC Siwale, H.1872 PC Zacharia, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.

Mei 12, 2017

Katibu wa CCM, Kata ya Bungu, Alife Mtulia, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyambunda, Wilaya ya Kibiti aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake.

Mei 18, 2017

Mwenyekiti wa CCM, Tawi la Njia Nne Wilaya ya Kibiti, Iddy Kirungu, aliuawa na mwanaye Nurdin kujeruhiwa kwa risasi.

Juni 2, 2017

Askari Mgambo Erick Mwarabu alipigwa risasi tatu na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake kitongoji cha Kazamoyo, Rufiji.

Juni 8, 2017

Watu watatu wakazi wa kijiji cha Nyamisati, Wilaya ya Kibiti wanadaiwa kufariki baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Watu hao wametajwa kwa majina ya Hamid Kidevu, Yahya Makame na Moshi Machela.

Juni 3, wazee wa Mkoa wa Pwani walimwomba Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kwenda wilayani Kibiti kuzungumza nao kuhusu hali ya usalama. Siku moja baadaye IGP Sirro alikubali mwito huo.

Katika kikao hicho kilichofanyika Juni 5, katika Shule ya Sekondari Kibiti, IGP Sirro aliwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwafichua wahalifu.

“Pelekeni salamu kwa wauaji hao kwamba ubaya huwa unalipwa kwa ubaya siku zote. Pelekeni salamu kuwa siku zao zinahesabika,” alionya IGP Sirro.

Mwaka 2013 yalitokea wilayani Kilindi mkoani Tanga ambako msikiti wa Madina ulibainika kuwapo katikati ya pori kati ya Tanga na Bagamoyo.

Mwaka 2014 vijana waliokuwa wakipewa mafunzo ya kigaidi walikamatwa mkoani Mtwara wakiwa wanapewa mafunzo tayari kujiunga na al-Shabaab.