Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liko tayari wakati wowote kupeleka vikosi vyake kulinda amani nchini Sudan Kusini.
Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Eric Komba, amesema kwamba kwa sasa wanasubiri maagizo ya kiutekelezaji kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete.
“Ninachoweza kusema ni kwamba jambo hili liko katika hatua za kiserikali na sasa tunasubiri maagizo ya kiutekelezaji kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu.
“Akisema pelekeni jeshi hata leo sisi tuko tayari, kwa sasa hatujui ni askari wangapi wanahitajika — kama ni kikosi, batalioni au brigedi — inayotakiwa kupelekwa huko, sasa akitwambia tupeke hakuna tabu tuko tayari,” amesema Luteni Kanali Komba.
Hatua hiyo ya JWTZ inatokana na Serikali kukubali ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, baada ya kumwomba Rais Jakaya Kikwete kusaidia kupeleka majeshi yake Sudan Kusini.
Lengo la maombi hayo ni mpango wa kupeleka kikosi nchini Sudan Kusini kwa ajili ya kulinda amani kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo.
Mpango huo ulitangzwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jijini Dar es Salaam kwamba Serikali imekubali kupeleka batalioni moja baada ya kuombwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Sudan Kusini imekuwa katika machafuko ambayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine kujeruhiwa.
Membe amesema jukumu la kulinda amani katika Bara la Afrika ni la Waafrika wenyewe na kwamba Tanzania inajiona kwamba ina jukumu la kusaidia kupatikana kwa amani.
Kwa sasa Tanzania ina vikosi vya wanajeshi wa kulinda amani katika nchi za DRC, Darfur (Sudan) na Lebanon. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu 500 na wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni wanajeshi.
Kuanza kwa mgogoro Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, akitangaza kushindwa jaribio la kuipindua Serikali yake nchini humo, alisema kwamba vikosi vya usalama vya Sudan Kusini vimefanikiwa kugundua na kuzima njama za jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali yake.
Rais Salva Kiir Mayardit alisisitiza kwamba aliyekuwa Makamu wake wa Rais, Rick Machar, ni miongoni mwa watu waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga jaribio hilo.
Machar, ambaye alifukuzwa kazi Julai 25, mwaka jana, kwa amri ya Rais, alikuwa tayari ametangaza nia yake ya kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika nchini humo mwaka huu, lakini alizuiwa kufanya hivyo.
Sudan Kusini yenye utajiri mkubwa wa mafuta ilikuwa nchi huru Julai 9, 2011 baada ya kujitenga kutoka Sudan.
Mgogoro huo ulitokea baada ya Rais Kiir kutangaza ghafla kumwondoa madarakani Makamu wa Rais, Riek Machar, na kuvunja Baraza la Mawaziri mwezi Julai.
Sudan Kusini yenye makabila mengi na siasa zake zilizoegemea katika ukabila, imekuwa katika hali ya hatihati tangu ilipopata uhuru wake kutoka Sudan.
Rais Kiir anatoka katika kabila kubwa la Wadinka Ngok, na Machar anatoka kabila la pili kwa ukubwa la Wanuer.
Kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri kuliongeza tofauti kati ya makabila tofauti nchini Sudan Kusini, pia kusababisha kuibuka kwa mgogoro huo.
Historia ya Sudan Kusini
Sudan Kusini iliunda jimbo kubwa katika karne ya 15 na 19, baada ya wahamiaji wa makabila yasiyo Niloti, yaani Waazande, hasa kutoka eneo la Bahr al Ghazal, kuingia katika jimbo hilo.
Katika karne ya 18, watu wa Avungara waliingia na kwa haraka wakaweka mamlaka yao juu ya Waazande. Utawala wa Avungara ulikaa kwa muda bila kupingwa mpaka Waingereza walipoingia katika himaya hiyo mwishoni mwa karne ya 19.
Vizuizi vya kijiografia viliwalinda watu wa Kusini kutokana na kuenea kwa Uislamu, na kuwawezesha kurejesha turathi zao za kijamii na kitamaduni na urithi wao wa kisiasa na taasisi za kidini.
Misri, ambayo ilikuwa chini ya utawala wa Khedive Ismail Pasha, ilijaribu kwa mara ya kwanza kuitawala kanda hiyo katika miaka ya 1870, na kuanzisha jimbo la Equatoria katika sehemu ya kusini.
Gavana wa kwanza wa Misri alikuwa Samwel Baker, aliyeanza kuhudumu mwaka 1869, akifuatiwa na Charles George Gordon mwaka 1874 na Emin Pasha mwaka 1878.
Maasi ya Mahdist ya miaka ya 1880 yaliuyumbisha mkoa huo mchanga, na Equatoria ilikoma kuwapo kama milki ya Misri mwaka 1889. Makazi muhimu katika Equatoria yalikuwa pamoja na Lado, Gondokoro, Dufile na Wadelai.
Sudan Kusini ilitawaliwa kama eneo la pekee wakati wa ukoloni wa Kiingereza hadi 1947 ilipounganishwa na Kaskazini kama nchi moja bila kuwauliza wenyeji.
Wakati wa uhuru wa Sudan mwaka 1956, viongozi wa Kusini walidai haki ya kujitawala ndani ya taifa jipya, lakini mapatano yalishindikana na hali hiyo ilisababisha kutokea kwa vita ya Anyanya kati ya 1956 na 1972.
Kanali John Garang aliunda Chama cha SPLA na kuanzisha vita ya ukombozi wa taifa hilo mwaka 1983, baada ya Sudan Kaskazini kutangaza kuwa taifa hilo linafuata sheria ya Kiislamu.
Vita hiyo ya pili ilikwisha mwaka 2005 kwa mkataba wa amani ulioacha Kusini kama sehemu ya kujitawala ndani ya Sudan hadi ipigwe kura juu ya suala la kujitenga lililopangwa kwa mwaka 2011.
Zaidi ya watu milioni 2.5 waliuawa na wengine zaidi ya milioni tano kuachwa bila makazi, na wengine kuwa wakimbizi.
Baada ya kifo cha John Garang, majeshi ya Southern Sudan Army na South Sudan Defense Force (SSDF) yalisitisha uhasama wao na kuungana Januari 2006, chini ya Azimio la Juba.
SSDF ilianzishwa na Makamu wa Rais wa sasa wa Sudan Kusini, Dk. Riek Machar. Chini ya Azimio la Juba, Jenerali Matip akawa Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan Kusini, na vikosi vyake vya SSDF kuingizwa katika jeshi la Sudan Kusini, na kuongezea safu yake kutoka 50,000 hadi 309,000.
Jumla ikawa askari 359,000. Wote sasa ni jeshi moja linalojulikana kama Jeshi la Sudan Kusini. Jenerali Oyay Deng Ajak aliteuliwa kuwa Ofisa Mkuu wa Watumishi wa Jeshi la Sudan Kusini, hadi Mei 2009 wakati alipompisha Meja Jenerali James Hoth Mai.