Dar es Salaam

Na Aziza Nangwa

Mkuu wa Majeshiya UlinziTanzania,Jenerali Venance Mabeyo, ameyataja mafanikio ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliyoyapata tangu lianzishwe Septemba Mosi, 1964.

Mafanikio hayo ameyataja mjini hapa wiki iliyopita akitoa taarifa ya changamoto na mwelekeo wa JWTZ kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru yatakayofanyika Desemba 9, mwaka huu. 

Mabeyo anasema baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26, 1964 serikali iliendelea kuiimarisha JWTZ kwa kuboresha ongezeko la rasilimali watu, mafunzo na vifaa na hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 1970 ikaanzisha vikosi vingine. 

Anasema kukua kwa jeshi hilo ni moja ya mafanikio ya kujivunia kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru na 57 ya JWTZ, huku ikiendelea kukua sambamba na mahitaji ya ulinzi wa nchi.

Pia anasema hadi sasa hivi kuna kamandi tano zinazotokana na mfumo wa kiuongozi na zote zinafanya kazi chini ya mhimili mmoja. 

Anasema chini ya makao makuu ya jeshi, kamandi ya kwanza inaitwa Jeshi la Nchi Kavu, kamandi ya pili ni Jeshi la Anga, kamandi ya tatu ni Jeshi la Wanamaji, kamandi ya nne ni Jeshi la Kujenga Taifa na kamandi ya tano ya Jeshi la Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi.

Katika hatua nyingine, anaelezea majukumu ya msingi ya JWTZ kuwa ni ulinzi wa nchi dhidi ya uvamizi wa kutoka nje kupitia nchi kavu, majini na angani na jukumu hilo linatokana na kusudio mama la kulinda masilahi ya msingi ya Tanzania.

“Yaani uhuru, haki, undugu, mshikamano, umoja wa kitaifa na demokrasia ambayo yanajumuishwa kwa maneno machache ya msingi kwamba kulinda amani ya taifa,” anasema Mabeyo na kuongeza:

“Hii ni kwa sababu unapoongelea mafanikio ni lazima uwe na kipimo cha kupimia. Katika hili ninaamini kipimo kizuri ni kuyafahamu majukumu yetu na kisha kujiuliza ni kwa kiasi gani au kwa kiwango gani tumeweza kutekeleza majukumu hayo ya msingi kwa ujumla wake.”

Anayataja majukumu mengine kuwa ni kushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU). 

Mengine ni ushiriki wa JWTZ katika operesheni mbalimbali za kimataifa na kikanda. 

Anasema JWTZ imeshiriki katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwamo Msumbiji, Afrika Kusini, Angola, Zimbabwe, Namibia na Vita ya Kagera dhidi ya Idd Amini wa Uganda (mwaka 1978), Comoro na vyinginezo. 

Analitaja eneo jingine kuwa jeshi hilo limeshiriki kikamilifu kusaidia mamlaka za dola za kiraia, vilevile kushirikiana na mamlaka za kiraia katika maeneo mbalimbali hasa majanga, dharura mbalimbali au maendeleo yoyote ya kitaifa. 

Pia anataja eneo jingine ni jeshi hilo kushiriki katika mazoezi ya kijeshi ya kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mazoezi ya kijeshi upande wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Vilevile anasema wanashirikiana na UN na mataifa makubwa kufanya mazoezi ya pamoja ya nchi kavu, ikiwamo Marekani, India, China na Urusi kwa mazoezi ya majini.

Katika hatua nyingine, anasema wanafanya diplomasia ya kijeshi kwa njia ya kujenga uhusiano na majeshi mengine hasa ya EAC na SADC.

“Tunazo ofisi zetu katika balozi zetu mbalimbali zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa SADC na nje ya Afrika,” anasema Mabeyo na kuongeza:

“Kutokana na majukumu hayo jeshi letu limekuwa na mafanikio makubwa kwa ujumla wake na tangu lianzishwe limeendelea kutekeleza majukumu yake hayo kwa weledi, uadilifu, uaminifu, uzalendo, uhodari na kwa utiifu mkubwa. 

“Miongoni mwa mafanikio yetu ni kudumisha amani na utulivu uliopo nchini mwetu na limeshiriki ukombozi na linaendelea kutoa mafunzo kwa majeshi ya nchi mbalimbali jirani, rafiki pamoja na nchi zingine nje ya Afrika. 

“Mafunzo hayo mengine yalifanyikia katika nchi hizo na mengine katika nchi yetu na nikiainisha kwa kifupi tu undani wa mafanikio hayo huwezi kuyaongelea pasipo kuongelea fikra na falsafa za Mwalimu Julius Nyerere kuhusu nafasi ya Tanzania katika jumuiya ya kimataifa.” 

Anasema baada ya kupata Uhuru, Nyerere akasema hautakuwa na maana iwapo nchi nyingine barani Afrika zitaendelea kuwa chini ya makucha ya wakoloni. 

Anasema kutokana na kauli ya Nyerere ndipo sera hiyo ikatekelezwa ipasavyo na JWTZ ikawa ni moja kati ya vyombo vyenye nguvu ya kitaifa, kwa kuwasaidia wapigania uhuru wote baada ya kuundwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1963. 

Anasema Tanzania iliteuliwa kuwa mwenyeji wa Kamati ya Ukombozi ya OAU na makao makuu yake yalikuwa Dar es Salaam, huku lengo likiwa ni kuratibu shughuli za ukombozi na iliongozwa na Brigedia Jenerali Hashimu Mbita akiwa Katibu Mkuu Mtendaji. 

Anasema katika kutekeleza jukumu hilo jeshi hilo lilitoa mchango mkubwa kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapigania uhuru wa vyama vya ukombozi, vikiwamo FRELIMO cha Msumbiji, NPRA cha Angola, ZANU PF cha Zimbabwe, SWAPO cha Namibia na ANC cha Afrika ya Kusini. 

Aidha, anasema jeshi hilo liliunda kikosi maalumu kikiwa na jukumu la kuratibu shughuli zote za ukombozi na kilikuwapo Dar es Salaam na vyama vya wapigania uhuru vilipatiwa mafunzo yaliyoendeshwa sehemu mbalimbali hapa nchini.

“Mfano FRELIMO kilipatiwa mafunzo katika Kambi ya Seventeen kule Nachingwea na Kongwa-Dodoma, SWAPO nacho kilipatiwa mafunzo Mbeya na Kongwa-Dodoma, ANC kilipatiwa mafunzo yake Mazimbu na Dakawa-Morogoro pamoja na Handeni-Tanga na Mgagao-Iringa na PSC cha Afrika Kusini chenyewe kilipatiwa mafunzo Masuguru-Pwani,” anasema. 

Mabeyo anasema mwaka 1986 JWTZ ilishiriki kwa mafanikio makubwa katika Operesheni Safisha na sasa hivi tena ipo Msumbiji chini ya SADC ikishirikiana na Msumbiji, Afrika Kusini, Botswana na Lesotho kuisaidia nchi hiyo kupambana na magaidi.

Anasema jeshi hilo ni nguzo muhimu katika kudumisha amani sehemu mbalimbali duniani kwa kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani katika nchi za Liberia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Sudan eneo la Darfur, Lebanon, Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Anataja ushiriki wa jeshi hilo katika operesheni mbalimbali kuwa mwaka 1993 walipeleka Liberia kikundi chenye jumla ya wanajeshi 850 kuungana na majeshi ya nchi za Afrika Magharibi yaliyokuwa chini ya Nigeria katika kusaidia kurejesha hali ya amani nchini humo kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza mwaka 1989 na kumalizika mwaka 1996. 

Anasema wanajeshi hao walitekeleza jukumu la kurejesha amani kwa takriban miezi 15 na tangu mwaka 2009 wamefanikiwa kutuma vikosi 13 kwa ajili ya kulinda amani maeneo mbalimbali, kwa mfano Darfur vilienda vikosi vitatu katika nyakati tofauti tofauti kuanzia mwaka 2009 hadi walivyomaliza hivi karibuni. 

Pia anasema Tanzania ilifanikiwa kutoa kikosi UN chini ya Luteni Jenerali mstaafu Paul Mella ambaye kwa sasa ni Balozi wetu DRC.

Anasema kabla yake Tanzania ilitoa Naibu Kamanda aliyewahi kuwa Balozi wetu nchini Urusi, Luteni Jenerali Wijonsi Kisamba, pia imetoa Meja Jenerali Henry Kamunde kuwa kamanda na ameendelea hadi ilipofungwa rasmi misheni huko Darfur mwaka 2020.

Anasema jeshi hilo linaendelea kushiriki ulinzi wa amani huko DRC kama sehemu ya MONUSCO huku kikosi cha kwaza kilikuwa chini ya uongozi  wa Luteni Jenerali mstaafu James Mwakibolwa.

Pia anasema kila mwaka kuanzia mwaka 2007 jeshi hilo limekuwa likipeleka kombania mbili za kijeshi kulinda amani Lebanon na hadi sasa wanaendelea na wamekuwa wakituma waangalizi wa amani katika nchi zenye migogoro na wametekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa. 

Anasema maofisa wanadhimu wa jeshi hilo wapo katika nchi zenye migogoro duniani wakishiriki shughuli za ulinzi wa amani na limeshiriki kwa mafanikio makubwa mwaka 2008 katika operesheni ya kuvikomboa visiwa vya Njuani-Comoro dhidi ya Kanali Mohammed Bakari.

Katika hatua nyingine, anasema licha ya mafanikio hayo lakini wapo baadhi ya maofisa na askari wakiwa katika majukumu hayo walipoteza maisha na wengine kupata majeraha yaliyosababisha kupata ulemavu.

“Naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee kutambua mchango wao mkubwa. Nirudie kwa kuwapa pole familia za wanajeshi wetu,” anasema na kuongeza:

“Waliopoteza maisha yao pamoja na mashuja wetu mbalimbali wakilinda taifa letu na wengine wakipigania amani ya mataifa mengine, wote tunawaombea kwa Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina.” 

Anayataja mafanikio mengine makubwa kwa jeshi hilo kuwa ni ile dhana au hali ya kubaki kuwa jeshi la wananchi licha ya mabadiliko mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

 Anasema suala la jeshi hilo kubaki kuwa la wananchi si dogo, pia ni jambo la kujivunia, kwa sababu nchi kadhaa Afrika na duniani kwa ujumla zimeingia katika machafuko kutokana na majeshi yao kuwa na dhana tofauti na JWTZ.

“Jeshi letu mara zote linatakiwa kuwa chini ya udhibiti au mamlaka za kiraia,” anasema na kuongeza: 

“Limeendelea kuwa imara na tayari kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na limeendeleza mshikamano na uzalendo wa hali ya juu, hivyo kubakia kuwa jeshi la wananchi. 

“Dira ya jeshi letu ni kuwa na jeshi dogo shupavu, lenye silaha za kisasa na kuwa tayari katika ulinzi wa Tanzania. Kwa muktadha huo nitumie nafasi hii kwa niaba ya maofisa na askari ninaowaongoza na kwa niaba yangu binafsi kumshukru Rais wetu na Amiri Jeshi wetu Mkuu, Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyolilea na kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

“Kipekee kabisa niwashukuru marais na amiri jeshi wakuu kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tano kwa jinsi walivyoliwekea jeshi letu misingi imara ya kizalendo na kuendelea kuliimarisha hatua kwa hatua hadi lilivyo sasa.” 

Aidha, anasema wakati Tanzania inatimiza miaka 60 ya Uhuru analishukuru Baraza la Mawaziri na viongozi wakuu wa serikali kwa ushauri wanaoutoa mara kwa mara kwa jeshi hilo.

Viashiria vya matishio ya ugaidi 

Kuhusu viashiria vya matishio ya vitendo vya ugaidi kuwapo hapa nchini anasema ni kweli vipo na anawaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuvidhibiti.

“Kama nilivyoeleza kwamba tunayo matishio mengi, tunayo matishio kutoka nje na matishio ya ndani, viashiria vya ugaidi vipo vilevile nchini mwetu,” anasema na kuongeza:

“Ugaidi ni vita kuu inayoanzia mataifa mengine na inasogea kuja nchini mwetu, kama mtakumbuka vizuri vita hii tuliona imeanzia Tanga katika maeneo ya Amboni wakateremka wakaja Kibiti na Mkuranga, tulipambana nao kidogo.

“Nao wakateremka kusini, tukapambana nao kule Mtwara na Ruvuma, wakavuka mipaka, wakaibuka wengine ndiyo sasa unawasikia wako Msumbiji, vita hii ni ngumu.”

Mabeyo anasema vita ya ugaidi inahitaji umakini mkubwa kwa sababu mbinu wanazotumia katika mapigano hayo si zile za utamaduni wa mapigano ya kawaida, kwa kuwa wanapigana katika vikundi vidogo vidogo.

Anasema kazi kubwa inayofanyika kwa sasa ni kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo na msaada mkubwa lazima utoke kwa wananchi.

“Wananchi ndio wanaoishi na vikundi hivyo, wamo miongoni mwetu, bila kufichuliwa na wananchi jeshi la wananchi si rahisi kuwafichua na kupambana nao, sasa msaada mkubwa tunaoupata ndiyo maana tunasema ulinzi huu ni wa Watanzania wote,” anasema na kuongeza:

“Kila mahali ulipo matishio unayoyaona vishirikishe vyombo vya ulinzi na usalama ili viweze kukabiliana nao kikamilifu, hasa kutokana na mbinu wanazozitumia mara nyingine wanashitukiza tu zaidi kidogo.

“Wakiwa katika vikundi vidogo vidogo si rahisi kuwatambua hadi uwe na mbinu za kuwatofautisha na watu wa kawaida, sasa mojawapo ni ugeni kama wameingia eneo lako unaona sura ngeni kwanini unyamaze?

“Ripoti kimya kimya na sisi tutamtafuta, tumeweza kushirikiana na wananchi kukabiliana na hali hiyo, walipofika Msumbiji hali hiyo ilipanuka na wakaendelea kuwatafuta wengine wa kuwaingiza katika vikundi hivyo kushawishi.”

Anasema njia ya kuwashawishi kwa kuangalia vitendo hivyo vya ugaidi ni kwamba wanatumia zaidi dini na wanapofanya hivyo ni rahisi kushawishika kwa sababu viongozi wa dini wanaaminika.

“Kwa hiyo wanapoaminika tayari wanapata wafuasi na wanapopata hao wafuasi wanawapa hayo mafunzo ya kuathiri jamii yetu. Kwa hiyo lazima sisi wote tushirikiane na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” anasema na kuongeza:

“Si wajibu wa jeshi moja. Ni wajibu wa vyombo vyote, lakini pia ni wajibu wa Watanzania wote, tukishirikiana vita hii tutaishinda, tupate elimu ya kidini ambayo ni sahihi.

“Na si ile ya kutupotosha na kuleta maafa na kuangamiza wenzetu kwa imani ambazo kwa kweli siamini kama Mungu anataka watu wafe.”