*Wasubiri wenzao A. Kusini, Malawi zianze za masika
*Kamanda: Matumaini ya Wakongo ni makubwa mno
*Waziri wa Ulinzi asema hali za vijana nzuri Brigedi ya Jeshi la Umoja wa Mataifa (UN) la Kulinda Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) inayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ipo salama na inajiandaa usiku na mchana kuhakikisha amani inarejeshwa katika eneo hilo. Habari za uhakika zinaeleza kwamba operesheni rasmi inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu baada ya vikosi kutoka Afrika Kusini na Malawi, kuungana na wenzao wa JWTZ ambao tayari wapo eneo hilo. Wakati zikiwa zimeanza za “rasharasha”, waasi wameonekana kutii amri ya kuwataka wawe nje ya eneo ambalo MUNUSCO wanawalinda wananchi walio kwenye makambi. Mmoja wa makamanda wa JWTZ walio eneo hilo amezungumza na JAMHURI, na kusema kuwa wito wa kuwataka waasi hao wasalimishe silaha ulilenga kuhakikisha wananchi walio na wasio kwenye makambi wanaendelea kuwa salama. Lengo la uamuzi huo lilikuwa kuzuia mashambulizi ya silaha, yakiwamo mabomu ambayo yalikuwa yakipigwa kwenye kambi za wananchi wasio na hatia. “Tangu tulipotoa msimamo huo hakuna mabomu yanayorushwa tena kwa wananchi, jamaa walikuwa wakirusha yanatua kwa wananchi. Tulichotaka ni kuwapo kwa freedom of movement (uhuru wa kutembea). Tukasema mwenye silaha asiwe maeneo haya. Hilo naona linakwenda vizuri. Tunayemkuta akiwa na silaha tunajua yupo kwenye mapambano,” amesema kamanda huyo. JWTZ walivyopokewa Anasema mapokezi waliyoyapata kutoka kwa wananchi wa Goma na DRC kwa jumla ni makubwa mno. “Bado tupo Goma, matarajio ya wananchi ni makubwa, makubwa, makubwa sana. Matumaini yao ni makubwa mno pengine hata kuliko uwezo wetu. Wanachoamini baada ya kutuona ni kwamba overnight tu tutamaliza kila kitu. “Hatuna matatizo kabisa na watu. Wanajua sifa nzuri ya jeshi letu, wanajua tumeshiriki operesheni nyingi kwa mafanikio na kwa kweli wanaamini kwamba kulala na kuamka amani itapatikana. “Wanajeshi wa hapa wanafanya kazi. Tumekuta wapo wengine wanafunzi wetu - tena wana vyeo hadi makanali - wana furaha sana. Wanaona kwenye jambo hili kama wamekuja hadi walimu wao, basi mambo yatakuwa mazuri. Ninachoweza kusema ni kwamba matumaini ya wananchi wa hapa ni makubwa, lakini kwa kweli inabidi juhudi za pamoja za kurejesha amani hapa,” amesema kamanda huyo ambaye kwa kuwa si msemaji rasmi, tunalihifadhi jina lake. Ameongeza kwamba baada ya vikosi vya Afrika Kusini na Malawi kuwasili, “shughuli” ndipo itakapoanza rasmi. Ushupavu wa JWTZ JWTZ imeshiriki operesheni nyingi kwa mafanikio makubwa. Imeshiriki Operesheni Kumekucha dhidi ya Wareno mwaka 1960; Operesheni TEGAMA – Msumbiji, dhidi ya majeshi ya Rhodesia na Afrika Kusini (1975-1980); Operesheni Safisha–Msumbiji, dhidi ya Mozambican National Resistance au Resistência Nacional Moçambicana (RENAMO) mwaka 1986-1988; Operesheni dhidi ya mamluki waliovamia Kisiwa cha Ushelisheli mwaka (1981-1982), Operesheni Demokrasia Comoro (Machi 2008) iliyomng’oa Kanali Bakar kutoka kisiwa cha Anjouan. JWTZ imeshiriki katika operesheni za kulinda amani chini ya Majeshi ya Umoja wa Mataifa. Mifano ya karibuni ni ya Liberia, Darfur na Lebanon. JWTZ ina hazina kubwa ya uzoefu kutokana na operesheni hizo. Siri kubwa ya mafaniko ya JWTZ ni umoja, ujasiri, nidhamu na weledi. Waziri wa Ulinzi anena Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alipoulizwa na JAMHURI hali ya makamanda na wapiganaji wa JWTZ waliopo DRC, alisema ni nzuri na kwamba wana ari ya kutekeleza kile kilichoufanya Umoja wa Mataifa uwapeleke huko. “Askari wetu wanaendelea vizuri kabisa, hawajaanza kazi rasmi kwa kuwa wanawasubiri wenzao wa Afrika Kusini na Malawi wawasili. “Kwa sasa wanaendelea sawa kabisa wakiwa wanasoma mazingira yalivyo. Viongozi wa Maziwa Makuu wamekuwa na kikao juzi, walichokubaliana, na ambacho kwa kweli ndiyo msimamo wa Tanzania, ni kuhakikisha amani inapatikana katika ukanda huu. “Serikali ya DRC na waasi wa M23 wanaendelea na mazungumzo. Hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais Kikwete amelizungumza vizuri suala la amani katika ukanda huu. “Jeshi letu lipo salama na lipo tayari kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha amani inarejeshwa DRC, lakini njia ya amani ni nzuri zaidi,” amesema Nahodha. Tambo za M23 Kinyume cha tambo za baadhi ya makamanda na wapiganaji wa kundi la M23, wapo walioamua kusalimisha silaha - ingawa si wengi - na wengine wameondoka kwenye maeneo yaliyoamuriwa na MONUSCO. Wanajeshi 3,000 wa UN wapo mashariki mwa DRC wakiwa na dhima ya kuyanyang’anya silaha makundi ya waasi, wakiwamo M23. Tayari raia wanne wa Rwanda waliokuwa wakipigana upande wa M23 wametoroka na kwenda kuomba hifadhi nchini Uganda. Wamesema walilazimishwa na Jeshi la Rwanda kujiunga na waasi wa M23 mashariki mwa DRC; madai ambayo yanazidi kuthibitisha taarifa ya Marekani na ile ya Umoja wa Mataifa ya kwamba nchi hiyo ndiyo inayofadhili mapigano hayo. Mmoja wa Wanyarwanda hao amesema asilimia 90 ya wapiganaji wa M23 ni wanajeshi wa Rwanda. Wanajeshi hao, miongoni mwao yumo aliyejitambulisha kuwa ana cheo cha kapteni katika Jeshi la Rwanda. Amesema ameamua kuasi baada ya kuona watu wengi wasio na hatia wakiuawa. Amemwelezea Rais Paul Kagame wa Rwanda kama Amiri Jeshi Mkuu wa M23. “Kila anachosema ni lazima kitekelezwe,” amesema. Msemaji wa Rais Kagame, Yolande Makolo, amepuuza madai hayo akisema hayana maana. “Tunapaswa kuacha uvumi, propaganda na kulaumu na kuendelea na suala la kuleta amani,” amesema. Mwingine aliyesema kwamba ni mwanafunzi wa udaktari wa binadamu, anasema alitekwa na wanajeshi wa Rwanda akiwa katika mpaka wa Gisenyi mnamo Agosti 2012. Anasema alipelekwa karibu na mpaka na huko aliwatibu majeruhi zaidi ya 300 walioumizwa kwenye mapigano. “Walikuwa wakiwachukua na kuwapeleka mstari wa mbele kwenye mapambano wakiwa hawajahtimu mafunzo,” amesema. Msemaji wa Jeshi la Rwanda, Joseph Nzabamwita, amesema atakuwa tayari kuzungumzia madai hayo endapo tu atapewa majina ya hao wanaodai kwamba ni raia wa Rwanda. Ameongeza kwamba wametunga habari hiyo ili waweze kupata hadhi ya ukimbizi. Wiki iliyopita, Marekani iliitaka Rwanda kuacha mara moja kuiunga mkono M23. Kumekuwapo taarifa zisizotiliwa shaka na Marekani na Umoja wa Mataifa kuwa Rwanda imepeleka vikosi vyake mashariki kwa DRC kuwasaidia waasi hao. Tangu kuanza kwa mashambulizi ya M23 mnamo Aprili 2012, watu zaidi ya 800,000 walio mashariki mwa DRC wameyakimbia makazi yao. Jeuri ya M23 UN iliwapa wapiganaji wa M23 saa 48 kusalimisha silaha, la sivyo watakabiliwa kijeshi. Kikosi cha MONUSCO kinasaidiana na Jeshi la DRC kuwadhibiti waasi hao. Kimekubaliwa kutumia nguvu dhidi ya waasi wanaolaumiwa kwa kuwaua raia katika maeneo karibu na mji wa Goma. Julai, mwaka huu, mapigano kati ya M23 na Jeshi la DRC yaliibuka, na UN iliishutumu M23 kwa kuwaua holela raia katika eneo la Mutaho, Goma. Kitendo cha waasi wa M23 kupuuza amri ya UN ya Julai 30, mwaka huu, inayowataka wasalimishe silaha kimekifanya kikosi cha MONUSCO kingie “kazini” kwa kuhakikisha yeyote anayekutwa na silaha anadhibitiwa kama adui mpiganaji. Hali ya usalama iliyokuwa imezorota mashariki mwa nchi, sasa imeanza kutia matumaini. Maelfu ya wananchi waliokimbia makazi, baadhi wameanza kurejea. Majeshi ya MONUSCO yakiwa na silaha kali na za kisasa, yameahidi kurejesha hali ya amani na utulivu katika eneo hilo. Wanajeshi wamekuwa wakishangiliwa kila wanakopita, hali inayoashiria kuwa wananchi wameridhia kuwapa ushirikiano. Agizo la UN liliwataka watu wote katika Jimbo la Kivu Kaskazini (inayohusisha Goma na Sake) ambao si sehemu ya wanajeshi wa Serikali ya DRC, wasalimishe silaha zao ndani ya saa 48. Watu zaidi ya milioni moja wanaishi Goma na Sake, na kando ya barabara inayounganisha maeneo hayo. Kambi ya dharura ya Mugunga ina wakimbizi zaidi ya 70,000 waliokimbia makazi yao kutokana na vurugu zilizosababishwa na waasi. Uganda, Rwanda zazidi kukana Kwa mara nyingine, Rwanda na Uganda zimekana madai yanayotolewa na UN kuhusu kuwaunga mkono waasi Mashariki mwa DRC. Uganda inasema Umoja huo unatafuta mtu wa kumlaumu kwa kushindwa kwa jeshi lake mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa. Ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) imesema majeshi ya Rwanda na Uganda yamewapatia silaha waasi. Wanyarwanda wakimbilia Uganda Raia kadhaa wa Uganda wameendelea kuomba hifadhi katika nchi jirani ya Uganda. Licha ya juhudi za Rwanda kutaka raia wake walioko ugenini warejee nyumbani wakiwamo waliokimbia nchi mwaka 1958 baada ya mapinduzi ya ufalme, Wanyarwanda wengi wangali na hofu ya usalama wao. Miezi miwili iliyopita wanafunzi 16 wa Rwanda walitorokea Uganda kwa madai ya kulazimishwa kujiunga na wapiganaji wa M23 wanaoendesha harakati zao Mashariki mwa DRC. Baadhi ya wakimbizi wamedai kutoroka makundi ya waasi baada ya kulazimishwa na serikali kujiunga nayo. M23 ni nani? Jina M23 limetokana na mazungumzo ya amani ya Machi 23, 2009 ambayo waasi hao wanadai Serikali ya DRC baadaye iliyapuuza. Mazungumzo hayo yaliwezesha waasi hao kujiunga katika Jeshi la DRC kabla ya kuasi Aprili 2012 na kuanza mapambano. Kundi hilo pia linajulikana kwa jina la Congolese Revolutionary Army. Linaundwa na watu wa kabila la Watutsi. Kumekuwapo madai na uthibitisho kadhaa kuwa linaungwa mkono na Rwanda na Uganda, ingawa mataifa yote hayo yamekanusha. Umoja wa Mataifa umeweka vikwazo vya kusafiri na kuzuia mali za viongozi wa waasi hao kuanzia Desemba, mwaka jana. Miongoni mwa walengwa ni kiongozi wa kundi hilo, Sultani Makenga. Machi, mwaka huu Kamanda Mkuu wa M23, Bosco Ntaganda, alijisalimisha kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Post Views: 492