Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIKA kuhakikisha changamoto za wafanyabiashara zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka, Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo (JWK) kwa kushirikiana na wataalam pamoja na wadau mbalimbali wameanzisha Jukwaa la Biashara na Huduma (JBH).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Oktoba 10, 2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana amesema lengo la jukwaa hilo ni kuwaleta pamoja wafanyabiashara, watoa huduma, viwanda, na wadau wengine wa biashara ili kuleta nguvu ya pamoja katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabaili.

“Sisi sote tunajua kuwa biashara ni nguzo muhimu katika kuendesha uchumi wa Taifa. Hata hivyo safari ya kufanya biashara si rahisi, hasa kwa wafanyabiashara wengi wa Kariakoo na maeneo mengine nchini. Pamoja na jitihada nyingi na njema ambazo zimekuwa kikwazo katika maendeleo na ustawi wa biashara zetu,” amesema.

Amebainisha baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa taarifa na ujuzi, ukosefu wa teknolojia, mitaji na upatikanaji wa mikopo, soko la Kariakoo kudorola katika masoko ya kikanda, urasimu na sera za biashara pamoja na miundombinu.

“Umuhimu wa jukwaa hili ni mkubwa sana ikiwemo kuunganisha wafanyabiashara na masoko, viwanda, watoa huduma, wawekezaji, biashara mtandao, kuingiza bidhaa zilizozalishwa Tanzania katika masokjo EAC na SADC, kuimarisha ushirikiano na mafunzo, kupunguza urasimu pamoja na kutoa huduma za kiufundi na uwezeshaji.

“Jukwaa la wafanyabiashara ni mwito kwa kila mmoja wetu kwa sekta binafsi, serikali na washirika wa maendeleo kushirikiana kwa dhati na kujenga mustakabadhi bora wa biashara katika eneo hili. Sote tuna jukumu la kuhakikisha kuwa tunachukua hatua za kimkakati kwa ajili ya kuwezesha biashara zetu, kuongeza ushindani na kujenga uchumi imara,”.

Naye Katibu Mtendaji wa Jukwaa hilo, Fredy Leopold amesema uzinduzi wa Jukwaa la Biashara na Huduma (JBH), unatoa mwanga mpya kwa maendeleo ya biashara Kariakoo, Tanzania, na Afrika Mashariki kwa ujumla.

“Leo, tunapoanzisha jukwaa hili, tunafungua milango ya fursa mpya za kiuchumi na maendeleo kwa wafanyabiashara, viwanda, watoa huduma, wadau wa biashara, na jami kwa ujumla.

“Jukwaa hili kwa kutambua umuhimu wa teknolojia katika maendeleo ya biashara linahimiza matumizi ya mifumo ya biashara za mtandaoni e-Commerce, kutangaza bidhaa mitandaoni, kutoa na kupata taarifa za biashara kwa njia ya mtandao,” amesema.