Hali ya kutoelewana iliyopo kati ya Rwanda na Uganda, nchi mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inatishia utangamano wa jumuiya hiyo.
Uhasama kati ya nchi hizi mbili ni wa muda mrefu na umewahi kusababisha mapambano ya silaha kati ya majeshi yao ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Zipo tuhuma kutoka kila upande kwamba kuna njama za kushawishi hujuma dhidi ya serikali zao. Kila nchi ina wapinzani ambao nchi moja inatuhumu wanasaidiwa na hasimu wake.
Lakini si Uganda na Rwanda pekee zenye ugomvi. Kuna kutoelewana kati ya Rwanda na Burundi, kila nchi ikiituhumu nyingine kwa tuhuma za kusaidia wapinzani dhidi ya serikali zao.
Somalia, nchi ambayo imewasilisha tangu 2013 maombi ya kujiunga kwenye Jumuiya, nayo imeingia kwenye mgogoro na Kenya juu ya umiliki wa eneo la bahari kati ya nchi hizo mbili. Ni mgogoro unaoonekana utaamuliwa kwa njia za amani na itakuwa vizuri uamuliwe kabla ya Somalia kupokewa kama mwanachama mpya wa Jumuiya.
Hata Tanzania na Rwanda zimewahi kuwa na uhusiano mbaya kipindi cha serikali iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete; uhusiano ulioharibika baada ya Rais Kikwete kushauri Rais Kagame afanye mazungumzo na waasi waliokuwa wanapigana vita dhidi ya jeshi la Rwanda. Ushauri huo haukupokewa kwa mikono miwili, na ilifikia hatua tukaanza hata kusikia vitisho na minong’ono ya uwezekano wa Tanzania kupigana na Rwanda. Hayo tuliepushwa.
Ugomvi kati ya majirani ni jambo ambalo linatarajiwa. Lipo tangu enzi na enzi na haliishi kwa ndoto pekee. Tatizo ni dogo zaidi kwa binadamu majirani, lakini gumu baina ya nchi jirani. Binadamu anaweza kuhama eneo ambalo linamkutanisha kila siku na ndugu au jirani asiyeelewana naye, lakini huwezi kuiondoa nchi Afrika na kuihamishia Australia kwa madhumuni ya kukwepa jirani mkorofi.
Umuhimu wa kuwepo uhusiano mzuri kati ya nchi wanachama za Jumuiya unaongeza uwezekano wa kupatikana kwa manufaa kadhaa ya kibiashara na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kukua kwa biashara miongoni mwao, kujiongezea nguvu ya pamoja ya kujadili maslahi ya Jumuiya, kupanuka kwa soko la bidhaa na huduma, kuvutia kwa urahisi uwekezaji, na kuimarishwa zaidi kwa hali ya usalama. Pia, kwa sababu ya uwepo wa miradi ya pamoja, kuna unafuu wa gharama ya miradi kama ya miundombinu, mawasiliano, na utunzaji wa mazingira.
Lakini haya yote hayawezi kufikiwa kwa urahisi katika mazingira ya uhasama kati ya nchi wanachamana. Ndiyo maana suala la kutafuta suluhisho la haraka, na Ikiwezekana la kudumu, na maridhiano kati ya Uganda na Rwanda ni muhimu kabisa.
Raia wa Afrika Mashariki wanakabiliwa na matatizo mengi katika jitihada zao za kuendeleza na kuboresha maisha yao. Na suala la msingi kabisa la kuwapa fursa ya kupambana na hali hiyo ni kwa serikali zao kuwajengea mazingira ya amani na usalama ndani ya nchi zao na baina ya nchi yao na nchi jirani.
Mwaka 1978 Serikali ya Tanzania iliamua kuanzisha vita dhidi ya Uganda iliyoongozwa na Jenerali Idi Amin baada ya kuvamiwa kwa eneo la Kagera; hatua iliyochukuliwa baada serikali kuamua kuwa hazikufanyika jitihada za kutosha na Umoja wa Nchi Huru za Afrika kutafuta suluhu kwa njia ya amani. Tunafahamu kuwa vita ile ilisababisha vifo na hasara kubwa ya kiuchumi kwa nchi zetu, na ni miaka ya hivi karibuni tu serikali ya Uganda ilimaliza kuilipa Tanzania deni la vita hiyo.
Kwa sasa hatuoni kama kutoelewana kati ya Uganda na Rwanda kunaweza kusababisha vita, lakini hatujui kama hilo haliwezi kutokea. Vita ya Kwanza ya Dunia ilianza baada ya mtu mmoja kumpiga risasi na kumuua mwanamfalme wa himaya ya Austro-Hungary, Franz Ferdinand. Kifo chake kikawa kama njiti ya kiberiti iliyolipua moto na kuanzisha vita katika mazingira ya uhasama ambayo tayari yalijengeka kwa muda baina ya mataifa makubwa ya Ulaya.
Kwa sababu ya kinachoonekana kama uhusiano wake mzuri na nchi zote mbili, Tanzania ina nafasi nzuri sana ya kushika jukumu la kusuluhisha mgongano huu kati ya Uganda na Rwanda ndani ya taratibu zilizowekwa kwenye mkataba wa ushirikiano wa Jumuiya.
Iwapo itapata hiyo nafasi siyo suala muhimu. Muhimu zaidi ni kwa nchi hizo mbili kuzima uhasama uliojengeka kati yao ili kulinda maslahi mapana zaidi ya ushirikiano wa Afrika Mashariki.