Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

JUMLA ya watahiniwa 557,731 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2024 ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 529,321 na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,410.

Mtihani huo ambao unaanza kesho Novemba 11 hadi Novemba 29, 2024 umehusisha jumla ya shule za Sekondari 5,585 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 961.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 10, 2024 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed amesema kati ya watahiniwa wa shule 529,321 wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66.

Amesema pia wapo watahiniwa 1,088 wenye mahitaji Maalum na kati yao wenye uoni hafifu ni 601, wasioona ni 56, wenye uziwi ni 209, wenye ulemavu wa akili ni 39 na wenye ulemavu wa viungo ni 183.

“Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 28,410 waliosajiliwa, wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana ni 17,243 sawa na asilimia 60.69. Aidha wapo watahiniwa wa kujitegemea wenye mahitaji Maalum 18 kati yao wenye uoni hafifu ni 01, wasioona 16 na mwenye ulemavu wa viungo 01.

“Maandalizi yote kwaajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Aidha ametoa wito kwa kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya Mitihani unaimarishwa na kwamba vituo hivyo vinatumika kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania.

“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote walioteuliwa kusimamia Mtihani, kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Wasimamizi wahakikishe kuwa, wanafanya kazi ya usimamizi kwa weledi na kwa kuzingatia Kanuni za Mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwa apate haki yake.

“Kwa upande wa watahiniwa, Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka minne. Hivyo ni matarajio kuwa watafanya mtihani wao kwa kuzingatia kanuni za Mitihani. Baraza halitarajii mtahiniwa yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu. Mtahiniwa atayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani,” amesisisitiza.