Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
MKURUGENZI Mtendaji Wakala wa Uwezeshaji Wannachi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan amesema kuwa uwepo wa mifumo ya kidijitali katika wakala huo na taasisi zote za serikali nchini itaongeza uwazi na uwajibikaji.
Burhan ameyasema hayo jana visiwani Zanzibar wakati akihojiwa katika kipindi cha Tatua kinachorushwa na ZBC Tv Zanzibar, ambapo amesema mifumo ya kisasa ya kidijitali italeta mageuzi makubwa ya ufanisi wa kazi katika maeneo mbalimbali.
Amesema ni muda muafaka kwa Zanzibar kuingia katika mifumo ya kidijitali na ZEEA imeshaanza mapema kuhakikisha inaingia katika mifumo hiyo ili kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“ZEEA tumeanza kupambana mapema ili tuweze kwendana na haya mabadiliko ya teknolojia ambayo yataleta uwazi na uwajibikaji katika utendaji na kukuza uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema Burhan.
Aidha Burhan amesema katika kipindi cha miaka miwili ndani ya miaka minne ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussen Mwinyi, wamefanya mabadiliko makubwa hasa katika kutatua changamoto zinawakabili wajasiriamali pamoja na kutengeneza miundombinu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema kwanini walipoanza vitu vyote vilikuwa vinakwenda kwa mfumo analogi sasa wanakwenda kwenye mabadiliko ya teknolojia kwa kuendesha vitu kidigitali.
“Ni muda muafaka sasa wananchi kuwa tayari kupokea mabadiliko haya kwani nchi zilizoendelea nyingi uchumi wao upo kwenye kidijitali, muda huu tunaokwenda unatutaka kuingia katika mfumo huo mpya,” amesema Burhan
Kuhusu ZEEA na mikopo kidijitali
Burhan amesema tayari wanaendelea na maandalizi ya mikopo hiyo ya kidijitali kwa kufanya mafunzo kwa watendaji wao kisha watakwenda kwenye halmashauri zote na baadae wataanza kutoa vipindi tofauti tofauti vya kuwaeleza wananchi ni namna gani wanaweza kupata mikopo hiyo kwa njia ya kidijitali.
“Njia hii ya mikopo kidijitali itakuwa ni suluhisho la matatizo mengi yaliyokuwepo hapo awali, tunakubali kuwa tulikuwa tunachelewa kutoa mikopo hapo mwanzo, unaweza kuomba ukaja kupata baada ya miezi miwili au mitatu, sasa tunaondoa hiyo changamoto.
“Sasa hivi kuna mikopo ambayo itaanza kutolewa kwa muda wa saa 24, ipo itakayokwenda siku tano hadi sita pia itakuwepo mingine ambayo itachukua siku 14, hiyo ni kutokana na ukubwa wa fedha inayoombwa, ila mikopo ya 100,000 hadi milioni mbili haitazidi siku moja,” amesema Burhan
Aidha amesema katika kuwawezesha wananchi kiuchumi hadi sasa tayari wameshatoa mikopo ya Bilioni 34.9 wakiwafikia moja kwa moja watu 24,696 ikiwa wanawake 14, 441 na wanaume 10, 251.
“kwenye mafunzo ya ujasiriamali hasa ya elimu ya kifedha, uokaji, mazao ya nyuki, digital marketing tumeweza kuwafikia watu 9,805 ikiwa wanawake 7,319 na wanaume 2,436. Aidha katika kupata masoko endelevu, tumekuja na Tamasha la Fahari ya Zanzibar ambalo litafantika kila mwaka, pia tuna mfumo wa ZEEA Shop ambao utawanyanyua wajasiriamali kwa kuwaweza kuuza bidhaa zao mtandaoni ndani na nje ya nchi,” amesema Burhan
Asisitiza urejeshaji wa mikopo
Hata hivyo Burhan amewataka wale wote wanaokopa kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa fursa na watu wengine kuweza kukupa na kukuza mitaji pamoja na biashara zao.
“Yapo mabadiliko makubwa kwa kundi hili la wajasiriamali kwani wapo watu ambao walianza kupata mikopo wamemaliza na wanachukua kwa kuongeza kiwango cha mwanzo alichochukua, ila tunasisitiza kuwa ni muhimu kurejesha kwa wakati fedha ambazo wanakopesha ili kutoa fursa na wengine kukopa,” amesema
“Hata hivyo nisistize juu ya elimu wa kifedha ni muhimu kwa wajasiriamali kupata kwani wengi wanapata fedha lakini hawana nidhamu ya kuzisimamia, unapopata fedha na huna usimamizi mzuri utaweza kuendelea. Nisisitize mafunzo ya kifedha au elimu ya kifedha ni muhimu sana,” amesema na kuongeza
“Hali ya urejeshaji wa mikopo kwa sasa ipo 60 kwa 40 maana wapo wanaofanya vizuri na wanaolegalega, niendelee kusisitiza fedha hizi zinatakiwa kurejeshwa haijalishi ni za serikali, tunasema unachukua mkopo kwa manufaa yako lakini urejeshe ili Taifa liendelee,” amesema
Amesema fedha za mikopo zipo na wataendelea kutoa na kubainisha kuwa kwa mwaka jana walipewa Bilioni 15 ambazo ziliingia na zimerejesha na mwaka huu wamepewa Bilioni 46 hivyo zikikopwa na kurudi wanaongeza uwezo wa kupewa nyingine nyingi zaidi.
“Tumshukuru Rais Dkt. Mwinyi maana nimefanya utafiti duniani hakuna taasisi ambazo zinatoa mikopo ambayo haina riba, ila maono ya Rais kutupatia mikopo ambayo haina riba ni makubwa na yanalengo la kukomboa wananchi na uamskini,” amesema