Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amezindua Jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 jijini Dar es Salaam, litakalotumiwa na wadau kujadili fursa na hatua mbalimbali za kuboresha Sekta ya Fedha.

Fursa na hatua hizo ni pamoja na huduma ujumuishaji na endelevu za kifedha kwa njia ya kidigitali pamoja na kushirikishana namna bora ya kukuza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi ili kukuza na kuimarisha Sekta ya Fedha nchini.

Jukwaa hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Fedha kutoka Sekta za Umma na Binafsi wakiwemo kutoka benki na taasisi za fedha, kampuni za bima, vyama mwavuli vya sekta ya fedha, vyama vya ushirika wa akiba na mikopo na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha.

Uzinduzi wa jukwaa hilo umehudhuriwa pia na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu El-maamry Mwamba, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sauda Msemo na Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Festo Fute.

Akizungumza katika Hafla hiyo, Dk Nchemba amewahimiza wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuweka fedha zao Benki na kwamba Rais ameielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kutofunga akaunti za wateja inaowadai kodi, jambo ambalo TRA, wameanza kulitekeleza.

Ameahidi pia kuwa Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na Taasisi zake itaendelea kuzichukulia hatua kali Taasisi zinazotoa mikopo yenye riba kubwa (mikopo kausha damu) kwa kuwa inatweza utu wa wakopaji wanaonyang’anywa mali zao kwa kushindwa kulipa mikopo waliyokopa kwenye Taasisi hizo.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, rof. Adolf Mkenda, ameipongeza Wizara Fedha kwa kuandaa Jukwaa hilo na kwamba Wizara yake imetambua umuhimu wa masuala ya uchumi na fedha na imeandaa Mtaala Mpya wa Elimu utakaowawezesha wanafunzi kupata elimu ya ujasiriamali pamoja na biashara ili kuwajengea maarifa ya kujikwamua kiuchumi.

Amewataka wakopaji kutumia fedha wanazokopa kwa ajili ya kutekeleza miradi itakayowaongezea fedha ili wapate tija ya mikopo yao badala ya kuzitumia fedha za mikopo kwa malengo yasiyokusudiwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu El-maamry Mwamba amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha nchini imeandaa Jukwaa la wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 ili kubadilishana mawazo na uzoefu, kupeana taarifa, kujengeana uwezo, kushirikishana katika mafanikio na changamoto na kutafuta suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazoikabili sekta ya fedha nchini.

Amesema malengo ya Jukwaa hilo ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi cha miaka mitatu (2020/21-2023/24) na kushirikishana mbinu bora za kiutendaji na uzoefu katika Sekta ya Fedha.

Katika hafla hiyo nyaraka zilizozindulia ni Mkakati wa Upatikanaji wa Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa kati wa Mwaka 2023/24 – 2028/29, Mwongozo wa Mitaji halaiki (Crowdfinancing) pamoja na Mwongozo wa Utoaji Hatifungani kwa kutumia mfumo wa Sheria (Sukuk) kwa Kampuni na Taasisi za Umma wa Mwaka 2023.