Na Eleuteri Mangi,JamhuriMedia,Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Balozi wa Uswisi hapa nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa Leo Näscher kuhusu ushirikiano katika eneo la Utamaduni na Sanaa baina ya nchi hizo mbili.
Kikao hicho kimefanyika Machi 9, 2023 katika ofisi za Wizara hiyo yenye Makao yake Makuu katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Yakubu ameeleza azma ya Serikali katika kusimamia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambazo zinatoa ajira kwa vijana wengi na zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi nchini na namna watakavyoshirikiana katika kubadilishana utaalam na uzoefu katika sekta hizo.
Naye Leo Näscher Naibu Balozi wa Uswisi hapa nchini ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa amesema wana Jukwaa la Maendeleo ya Sekta ya Utamaduni (DGP) ambalo linaundwa na Balozi mbalimbali ambapo kwa sasa linaongozwa na Wenyeviti ambao ni Uholanzi na Uswisi wataendelea kushirikiana na Wizara hiyo na watakuwa kiunganishi na wadau mbalimbali wa sekta za Utamaduni na Sanaa wakisaidia katika nyanja za utaalam na ushauri.