Ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa Mfugale Flyover, Tazara jijini Dar es Salaam uliofanyika Septemba 27, 2018. Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alieleza kwanini ametaka daraja hilo lipewe jina la Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale…
…Lakini napenda tu kuwapongeza pia Wizara ya Ujenzi pamoja na TANROADS, pamoja na consultant ambao wote kwa pamoja walisimamia mradi huu.
Hongereni sana makandarasi pamoja na wahandisi washauri, pamoja na kampuni zote zilizoshiriki katika ujenzi wa daraja hili zuri la aina yake katika Jiji la Dar es Salaam.
Nitumie fursa hii kuishukuru serikali ya Japan kwa kutuunga mkono katika kutekeleza mradi huu. Daraja hili limegharimu takribani Sh bilioni 106.695. Asilimia nyingi zimetolewa na Serikali ya Japan na sisi pia serikali tumechangia asilimia zingine zilizobaki.
Tunawashukuru sana marafiki zetu hawa. Na niseme kwamba Japan ni marafiki zetu wa kweli na wa muda mrefu. Tumeshirikiana nao kwenye miradi mingi ya maendeleo, kwenye sekta ya miundombinu ya usafiri na umeme, elimu, afya, kilimo, maji, ujenzi nk.
Napenda Mheshimiwa Balozi ufikishe shukrani zetu nyingi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Japan kwamba tunathamini sana ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Japan. Asante sana.
Ninajua Mheshimiwa Balozi ametuaga hapa kwamba hivi karibuni muda wake umeisha na anarudi nyumbani. Hatukufurahi sana kukuona wewe unarudi nyumbani, lakini tunajua hata utakapokwenda nyumbani wewe utakuwa balozi mzuri wa Tanzania. Naomba ukayaseme yote mazuri ya Tanzania na ukahamasishe wawekezaji wengi waje hapa Tanzania.
Ndugu zangu, mabibi na mabwana, shukrani zangu pia napenda kuwashukuru sana Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi huu. Nampongeza Profesa Mbarawa ambaye wakati wa ujenzi wa daraja hili ukianza yeye ndiye alikuwa Waziri wa Ujenzi.
Lakini kwa namna ya pekee kabisa napenda nimpongeze Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, ambaye ameshiriki kikamilifu katika kubuni, kuandaa michoro na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa daraja hili. Hongera sana Mhandisi Mfugale na wote mlioshirikiana nao.
Binafsi namfahamu Mhandisi Mfugale. Nilifanya naye kazi kwa karibu wakati wote nikiwa Waziri wa Ujenzi. Hivyo namfahamu kama mchapa kazi, mzalendo, mwaminifu na mbunifu katika shughuli zake.
Mengi yameelezwa, lakini yako mengi pia ambayo hayakuelezwa hapa. Nakumbuka kwenye miaka ya 84 – 87 [1984, 1987] hivi, Injinia Mfugale akiwa anafanya kazi kule kwa watani zangu Songea, wakiwa wamejenga kambi yao nafikiri ni Matomondo pamoja na Kilimasera -walipofanya kazi zao wakati wa jioni sasa lazima wajipumzishe kwenye kijumba walichokuwa wamekijenga. Kesho yake waliamka saa nne wako nje. Hiyo nayo ni changamoto ya Injinia Mfugale aliyoipata kule Songea kwa watani zangu.
Hiyo Profesa Lema inawezekana haijui kwa sababu engineering ya kule ni special. Kwamba umeingia na mainjinia wako, kwenye jumba lile mlilokuwa mnajenga, lakini kesho yake mnaamka mko nje wote mmelala. Hiyo nayo ni engineering ya watani zangu kule Matomondo na Kilimasera.
Lakini si hilo tu, wakati wakiwa Matomondo wakichimba barabara wakati huo wanatengeneza nafikiri ni kwenye 87 [1987] greda lilikuwa linakatika ile fremu yake. Kila wakileta greda linakatika. Mpaka marehemu Mzee Gama akaenda akawaomba pale kwenye kijiji kwamba hawa wanaotengeneza barabara hii ya changarawe ni kwa ajili ya maendeleo yenu. Tangia hapo halikukatika tena greda lile.
Lakini inawezekana kutokana na hilo, Mfugale akaona njia nzuri ni kuoa huko huko kwa Wangoni kwa hiyo alipotoka kule kuhamishiwa huku Dar es Salaam aliondoka na mke. Sasa sifahamu hizo zilikuwa mbinu za kiinjinia au ulikuwa ni utaalamu mwingine. Nampongeza sana Mheshimiwa Mfugale.
Lakini injinia huyu Mfugale, pamoja na sifa zote zilizotajwa hapa; za kujenga daraja la Mkapa ambalo refu kuliko madaraja yote yaliyopo katika Afrika Mashariki na Kati, lime-cover eneo ya kilometa karibu 10.
Akajenga daraja la umoja, ninakumbuka wakati wa daraja la umoja linaandaliwa kujengwa niliitwa na Rais wa Msumbiji na Mzee Mkapa, Ikulu. Nikaambiwa tunataka daraja lile tupate majibu yake.
Nilipoenda ofisini nikamuita Injinia Mfugale, nikamwambia sasa nataka uchore design ya daraja la umoja. Alikaa ofisini kwa siku tatu bila kulala, na akalichora likakamilika. Lilipokwenda kupelekwa kwa marais wawili wa Msumbiji na Tanzania wakalikubali na daraja likaanza kujengwa. Siku lilipokuwa likifunguliwa, wala hakutambulishwa kama alifanya kazi ya kulisimamia hilo daraja. Nilipopata nafasi ya kusalimu, kwa sababu wakati huo sikuwa Waziri wa Ujenzi, nikataja tumpongeze Mfugale kwa daraja hili kwa kujenga.
Kwenye mwaka 2005, katika changamoto hizo ambazo alizipata Mfugale; mwaka 2005 alipewa tuzo na Mzee Mkapa kule Songea kama mfanyakazi bora na yeye kwa kutambua kuwa palikuwa na mainjinia wawili – yeye akiwa injinia wa barabara za vijijini na mwenzake alikuwa marehemu Mjungi ambaye alikuwa anashughulikia barabara za trunk road.
Lakini Mfugale alishughulikia barabara upande wa Kusini ndiye alisimamia ujenzi wa kwanza wa Barabara ya Somanga- Matandu kilometa 38 kwa kujenga kwa kutumia fedha za ndani. Lakini huyo huyo Mfugale ndiye alisimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Nangurukuru hadi Mbwemkuru kwa kutumia fedha za ndani. Yule mwenzake marehemu Mjungi alisimamia ujenzi wa barabara ya central corridor kuanzia Dodoma, Manyoni hadi Singida, kuiunganisha kipande kile.
Na walikuwa wakurugenzi wakuu wa barabara kwenye mwaka 2007, 2008. Hawa waliokuwa wasimamizi wakuu wa barabara na madaraja katika Wizara ya Ujenzi, baada ya kupewa maagizo fulani na wakubwa wao wakayakataa, wakaamuliwa kufukuzwa. Wamshukuru Katibu Mkuu aliyekuwepo ambaye alizuia kufukuzwa kwao kwa sababu palikuwa kinyume cha sheria na wao kwa sababu walikuwa wameamua kusimamia maadili ya kihandisi.
Nilitegemea wakati huo kwa sababu Wahehe huwa wana tabia ya kujinyonga, Mfugale angejiua, lakini yule mwenzake ambaye alikuwa siyo Mhehe, marehemu Mjungi alikwenda kuchukua pistol akajipiga risasi. Na leo ni marehemu kwa sababu ya kusimamia maadili ya kazi yake ya kihandisi. Hiyo ndiyo gharama ya kuwa mwaminifu katika kazi. Mfugale aliamua kuendelea kukaa, mpaka niliporudi tena Wizara ya Ujenzi nikamkuta yupo amewekwa kwa kupewa dawati tu anasoma magazeti. Wanapokwama mahali fulani utaalamu wanamuita kwa kumuuliza, hiyo ndiyo gharama ya kuwa mwaminifu.
Baada ya hapo nikamteua kuwa Chief Executive wa TANROADS. Tulikuta ujenzi wa kilometa moja umeshafika bilioni 3 kwa kilometa. Akaanza tena kushusha gharama ya construction per kilometa. Huyo ndiye Mfugale ninayemfahamu. Huyo ndiyo Injinia Mfugale ambaye wakati huo alikuwa hatembei na fimbo, leo anatembea na fimbo. Uaminifu wake wa kazi kubwa alizozifanya katika nchi hii.
Nataka kuwaambia ndugu zangu Watanzania, hauwezi kusahaulika kamwe. Amesimamia Daraja la Nyerere, amesimamia Daraja la Kikwete, amesimamia madaraja mengi katika nchi hii. Huyo ndiyo Mfugale.
Mheshimiwa Sheikh wa Dar es Salaam amezungumza hapa, anataka flyover nyingi hapa Dar es Salaam. Nataka kuwaeleza wana Dar es Salaam sasa hivi imeshatangazwa tenda ya kujenga barabara kutoka Mbagala- Gerezani- Kivukoni-Chang’ombe hadi Magomeni, jumla ya kilometa 21.
Ambapo fedha hizi zitatolewa za mkopo wa African Development Bank, lakini katika hivyo patajengwa flyover Chang’ombe pamoja na Mhasibu House au Machinjioni napo panajengwa flyover na tenda zimeshatangazwa. Kwa hiyo Sheikh Mkuu hii si flyover ya kwanza, zinakuja zingine.
Lakini si hiyo tu, pale Ubungo panajengwa inter-change ambayo itakuwa na level tatu. Kwa watani zangu Wazaramo maana yake ni ghorofa tatu. Magari yanapita hapa, yanapita juu, yanapita juu. Kazi zimeshaanza na hiyo interchange. Mfugale Flyover imegharimu bilioni 106.8, interchange ya Ubungo itagharimu bilioni 247, kwa hiyo kama haka ni ka-Mfugale lile litakuwa li-Mfugale. Na kazi kubwa zinazofanyika sasa hivi ni kuhakikisha umeme unachimbiwa ndani, na mabomba; kazi ambazo zinaendelea vizuri. Ila kazi ya kuinua kwenda juu itakuwa ni nyepesi sana.
Nataka kuwahakikishia Ubungo Interchange nayo itakuwa flyover ya aina yake kwa hapa Dar es Salaam. Ndiyo maana nilitoa mfano siku moja ndugu zangu Wazaramo, au Wakwere watakaokuwa wanatoka Bagamoyo au Kibaha akikosea flyover ni mahali gani pa kupitia anaweza akajikuta yuko Mwenge kumbe alikuwa anaenda Buguruni.
Lakini si hilo tu, tumeamua barabara ya kutoka Kimara hadi Kibaha, karibu kilometa 19.2 zijengwe njia sita, upande huu njia tatu na upande mwingine njia tatu. Lakini tutajenga service road upande mmoja na upande mwingine, kwa hiyo patakuwa na njia nane.
Na kandarasi tayari yupo, na fedha zile zote zinalipwa na Serikali kwa asilimia 100, bilioni 140. Tunaibadilisha Dar es Salaam, na ndiyo maana tulipokuwa tukibomoa bomoa nyumba kule wapo watu waliokuwa wanalalamika.
MFUGALE NI NANI?
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Patrick Mfugale, alizaliwa Ifunda mkoani Iringa.
-Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Consalata Fathers mjini Iringa
-Mwaka 1975 alihitimu elimu ya shule ya Sekondari Moshi.
-Mwaka 1977 aliajiriwa katika Wizara ya Ujenzi
-Mwaka 1983 alijipatia shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Rocky, India
-Mwaka 1991 alisajiliwa kama mhandisi mtaalam.
-Mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa.
-Mwaka 1994-1995 alipata shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Loughborough, Braunshweig nchini Uingereza
-Mwaka 2003 alipokea tuzo ya Distinguished Engineering Accomplishment.
-Aliteuliwa kuwa Mhandisi Mkuu wa Madaraja nchini Tanzania wakati huohuo na akiwa masomoni nchini Uingereza. Mwaka 1995 alitafiti na kutengeneza mfumo wa madaraja nchini.
-Alitengeza mfumo wa usimamizi wa madaraja (Tanzania Bridge Management System)
-Mwaka 2014 alisajiliwa kuwa Mhandisi Mshauri na kuwa mwanachama wa Chama cha Wahandisi Tanzania.
-Ametumia muda wake mwingi kama mtaalamu wa madaraja.
Alibuni daraja la Malagarasi lenye mita 178 kwa Sh milioni 300.
-Baadhi ya madaraja aliyojenga:
Daraja la Mkapa, Daraja la Umoja (linalounganisha Tanzania na Msumbiji), Daraja la Rusumo, Daraja la Kikwete,
Daraja la Nyerere, ameshiriki ujenzi wa madaraja takribani 1,400 nchini. Amebuni na kusimamia barabara za kitaifa zenye urefu wa takriban kilomita 36,258. Ni Mwenyekiti wa Kikosi cha Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), na Mjumbe wa Timu ya Majadiliano ya Miradi Mikubwa ya Umeme. Mwaka 2018 alipata tuzo ya uhandisi ya Engineering Excellency.
.tamati….