Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua Mtanzania Joyce Msuya kuwa Naibu Katibu Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira duniani, UNEP.

Ofisi kuu za shirika hilo la UN lipo jijini Nairobi, Kenya.

Bi Msuya atachukua nafasi ya Ibrahim Thiaw wa Mauritania, ambaye amemaliza muda wake wa kuhudumu.

Hadi wakati wa kuteuliwa kwake Jumatatu, Bi Msuya alikuwa mshauri wa Makamu Rais wa Benki ya Dunia kwa ukanda wa Asia Mashariki na Pacific jijini Washington, DC wadhifa alioushikilia tangu mwaka jana.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, kwa mujibu wa UN alisema “Bi Msuya ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 kwenye nyanja za maendeleo ya kimataifa kuanzia masuala ya mashirika, mikakati, uendeshaji, ufahamu wa usimamizi na ubia alioupata wakati akifanya kazi huko Afrika, Amerika Kusini na Asia.”

Alishika nyadhifa mbalimbali katika ngazi ya uandamizi kwenye Benki ya Dunia ikiwemo mwakilishi wa Benki ya Dunia na Mkuu wa ofisi ya benki hiyo hiyo Korea Kusini na mratibu wa taasisi ya Benki ya Dunia inayosimamia Asia Mashariki na Pasifiki nchini China.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji huyo mteule wa UNEP ana shahada ya uzamivu kwenye masuala ya sayansi ya biolojia ya viumbe viini na viumbe vidogo pamoja na sayansi ya kinga mwilini kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, Canada.

Ana shahada ya kwanza katika biokemia na kinga  ya mwilini kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde, Scotland.

Bi Msuya ameolewa na ana watoto watatu.