Na Moshy Kiyungi
Tabora.
Pasipo kumtaja gwiji la muziki huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabasele utakuwa hujakamilisha historia na maelezo ya muziki upaswavyo kusimulia.
Nguli huyo atabaki kuwa baba na nyota kuu ilioleta maendeleo na mabadiliko kwenye muziki wa rumba nchini humo.
Kabasele alizaliwa Desemba 16,1930 mjini Matadi huko DRC. Baba yake aliitwa Andre Tshimala na mama yake, Hortense Malula. Kabasele ndiye aliyekuwa kitinda mimba kwenye familia ya watoto sita.
Yaelezwa kwamba alikuwa mwanamuziki wa kwanza kuvitumia vyombo kadhaa vya muziki na kusababisha yatokee mabadiliko kwenye muziki.
Vyombo hivyo ni pamoja na tarumbeta, Clarinet, Saxophone na ngoma. Mwanamuziki huyo alifahamika kwa majina ya Grand Kalle. Ndiye raia wa kwanza huko DRC kutumia gitaa la umeme, kumiliki bendi yake binafsi ya African Jazz mwaka 1953 na kuwa na studio ya kurekodi muziki ya Surboum.
Pia aliwalea ‘kimuziki’ Rochereau Tabu Ley na Nico Kasanda. Kabasele na bendi yake ya African Jazz, walikuwa wa kwanza kusafiri kwenda nje ya DRC. Walifika katika nchi kadhaa za barani Ulaya zikiwamo Ubelgiji,Ujerumani,Italia na Ufaransa.
Kwenye miaka ya 1960, alitungua wimbo wa Independance Cha Cha, ulipendwa katika sehemu tofauti za bara la Afrika. Kibao hicho kilikuwa kikiisifia DRC kupewa Uhuru kutoka mikononi mwa wakoloni.
Alisoma Shule ya Msingi ya Institute Saint Joseph, iliyokuwa ikimilikiwa na shirika moja la mapadre jijini Kinshasa. Akiwa shuleni humo, alijiunga na kwaya la Kanisa Katoliki akiwa na miaka nane.
Kabasele alikuwa mwimbaji mzuri huku akitumia kwa umaridadi sauti yake ya tenor, huku akiendelea na masomo ya sekondari kwenye shule ya Ecomoraph. Umaarufu wake ulipelekea kuwa kivutio na kipenzi cha wengi shuleni.
Licha ya uimbaji wa nyimbo, Kabasele pia alikuwa akipenda michezo na kupelekea kupendwa hususan na mashabiki wa wanawake. Licha ya sifa zote hizo, Kabasele alikuwa na utovu wa nidhamu. Mapadre wanadiriki kuchukua hatua ya kumfukuza shule.
Katika kipindi cha ukoloni, shule takriban zote zilikua zikimilikiwa na mapadre, kwa hiyo ikamjia vigumu kwa Grand Kalle kupata shule nyingine itakayomkubali.
Kwa kuwa hapakuwa na shule inayomkubali, ilimbidi atafute kazi. Kabasele akabahatika kuajiriwa kama Katibu kwenye kampuni tofauti za jijini Kinshasa.
Mwaka 1947 kutokana na ushawishi wa rafiki yake, Georges Dula maarufu kama Geoder alipelekwa kujiunga na kundi la muziki la OTC. Bila kusita alikubaliana na pendekezo hilo, kwa kuwa aliona kwamba njia yake ya kuwa ‘nyota’ inaanza kufunguka.
Kuna kipindi alitoa wimbo wa Palmolive ambapo Grand Kalle aliwasifia wasichana kwamba ni warembo na wananukia manukato mazuri kama ya sabuni ya Palmolive.
Mwaka 1950, wazo likamjia aende kujaribia kipaji chake kwa Moussa Benatard, mfanyabiashara Myahudi na mmiliki wa studio ya OPIKA.
Baada ya Myahudi huyo kufanyiwa majaribio, akaona kwamba Kabasele ana kipaji, ila anastahiki asaidiwe, aongozwe, afundishwe namna ya kuimba kwenye studio.
Ndipo alipowekwa chini ya usimamizi wa mpiga gitaa mashuhuri Zacharie Elenga ‘Jimmy’. Wakafanikiwa kutoa vibao vingi vya Ondruwe, Maboko Likolo, Baninga Baninga, Makombo ya Jimmy na Putulu Emata.
Baada ya kuona amepata mafanikio ya nyimbo hizo kuwa mazuri, Granda Kalle akazidi kujipa moyo kwa kuchapa kazi vilivyo, akiwa na nia ya kutaka kujitegemea.
Mwaka 1954, Grand Kalle bendi yake ya African Jazz walipata zabuni ya kwanza kutumbwiza katika jiji la Bangui, Afrika ya Kati kwenye uzinduzi wa ukumbi wa Bar Dancing Bar Le Rex.
Ziara yao hiyo ilimfurahisha Grand Kalle sio kimapato, bali kuona yeye na kundi lake wanakubalika hadi kimataifa. Grand Kalle na kundi lake wakapata sifa nyingi kutokana na nyimbo nzuri kama Parafifi iliyorekodiwa 1957, Nzela Mosika, Ce n’est pas la peine de divorcer maintenant na nyingine nyingi.
Mwaka 1959, Orchestra African Jazz ikawa kwenye kipindi kigumu kutokana na utumiaji mbaya wa fedha. Yasemekana Kabasele alitokea kuwa mbinafsi aliyeshindwa kuwajali wanamuziki wenzie.
Ujio wa Tabu Ley Rochereau kwenye bendi hiyo, ukaleta nguvu mpya.
Tabu Ley akaja na wimbo wake wa Kellya uliopendwa na mashabiki wa muziki wa rumba.
Kundi hilo likaja kupata fedha nyingi waliposafiri kwenda Ulaya mwaka 1960, kutoa motisha na kuwaunga mkono wanasiasa wa DRC wakati wa mazungumzo ya uhuru wa nchi hiyo jijini Brussels, Ubelgiji.
Safari yao hiyo ya Ulaya iliwaletea sifa nyingi na mafanikio. Wakatoa vibao vilivyoweka hadithi kwenye historia ya rumba nchini DRC hadi sasa.
Nyimbo walizoachia wakati huo zilikuwa za Indépendance Cha Cha na Table ronde zilizokuwa utunzi wake Kabasele. Nyimbo nyingine zilikuwa Naweli Boboto na Sentiment Emonani zilizotungwa na Vicky Longomba, Tosekana na Mawonso Pamba za Dechaud Muamba , Sophia Motema na Merengue Soubidou wa Niko Kasanda.
Aidha alimuongeza mwimbaji Mujos, akaja kujiunga akitokea bendi T.P. OK. Jazz, kutokana na ushauri wa Tabu Ley.
Mwaka 1963, kukatokea kwa mara nyingine tena mgawanyiko mkubwa, sababu ikiwa ni wanamuziki kupiga kelele kutopewa pesa ingawa kazi wanaifanya ipasavyo.
Kwa safari hii takriban wanamuziki wote walijiondoa akiwemo Tabu Ley wakaenda kuunda bendi yao mpya ya African Fiesta. Kitendo hicho kilimuumiza Grand Kalle, lakini alijipa moyo, akaanza kuisuka upya bendi ya African Jazz.
Rafiki na mfadhili wake Jean Foster Manzikala, alimnunulia vyombo vipya vya muziki. Kikosi cha wanamziki wa bendi hiyo wakati huo kiliwajumuisha Nedule Papa Noël, Kambele Damoiseau, Jeannot Bombenga, Mathieu Kuka, Nsita Rolly, Alex Mayukuta, Casino Mutshipule, Munange Maproko na Yuma Michel Sax.
Ikatokea purukushani nyingine iliopelekea wanamuziki kujiondoa, na kupelekea African Jazz kuwa mwanzo wa kuangamia kimuziki.
Kwenye miaka ya 1969-1970, Kabasele alihama jiji la Kinshasa, akaweka maskani yake jijini Paris nchini Ufaransa. Akiwa jijini humo, alishirikiana na wanamuziki Manu Dibango, Don Gonzalo, Lutula Edo Clary, Jeannot Bombenga, wakaunda bendi ya African Team.
Bendi hiyo ikatoa vibao vingi vikiwamo Gauche-droite égal débordement, Africa mbiance, Bana Congo na Cuba, Laurent Fantôme na Cambridge. Nyingine zilikuwa wa Mayi ya Piyo,Safari Muzuri, Disciplini, KDL na Edona Souzy.
Hata hivyo African Team haikudumu kwa siku nyingi, nayo ikasambaratika. Kati ya 1973 na 1980, Kabasele akawa adimu jukwaani.
Alifanya onesho la mwisho kwenye ukumbi wa Hotel Intercontinental jijini Kinshasa. Baada ya hapo, hali yake kiafya ikawa inazorota na kipesa akawa anadidimia vibaya.
Joseph Kabasele ‘Ggrand Kalle’ aliyefahamika zaidi kama mzee wa msimamo, mzee wa kanuni, baba wa rumba, alifariki dunia jijini Paris, Ufaransa Desemba 11, 1983 akiwa na mri wa miaka 53.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema, Amina.