Mwanamuziki maarufu wa Uganda, Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleon, amenunua jozi moja ya kiatu aina ya raba kwa dola 12.5 za Marekani (sawa na Sh milioni 27 za Tanzania).

Wakati baadhi ya mashabiki wa muziki wakimbeza kwenye mitandao ya kijamii wakidai msanii huyo anajionesha, yeye amewajibu haraka, aksiema: “Nimeizawadia miguu yangu jamani.”

Mwanamuziki huyo alinunua viatu hivyo Nike Air Mag jijini Nairobi, Kenya alikoenda kwa ziara ya kimuziki na mara baada ya kuvinunua alivitangaza kwenye mtandao.

“Jifurahishe ungali hai, jipende ungali hai,” anasema Chameleon na kuongeza: “Narudishia miguu yangu shukrani. Siku imekuwa ikinibeba na kuhangaika jukwaani.

Chameleon anakumbusha kuwa miaka minane iliyopita nusura awe mlemavu wa miguu kutokana na ajali mbaya.

Msanii huyo alipokerwa zaidi na wapinzani kwenye mtandao, akajibu tena: “Sasa kama siwezi kutoa dola elfu 12.5 kununua kiatu. Basi Wachina wanauza viatu bei rahisi sana…nendeni mkanunue.”

Mwimbaji huyo wa wimbo wa ‘‘Wale Wale, waliobarikiwa na Mungu’, anasisitiza “Haya si majivuno kamwe, bali ni njia yake ya kumshukuru Mungu kwa kunijalia na kunipa uwezo kama huo.”

Wimbo huo kwa sasa ndiyo gumzo baada ya takwimu zake kuonekana unapendwa na watu wengi. Rekodi zinaonesha umetazamwa na watu zaidi ya milioni 1.3 katika mtandao wa You tube kote.