Na Isri Mohamed Jamhuri Media Dar es Salaam.
Oktoba 01, Chama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyokutana katika kikao chake maalumu jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake na Rais Samia Suluhu Hassan imemteua Jokate Mwegelo kuwa Katibu Mkuu wa UWT akitolewa kwenye nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Korogwe.
Nafasi hiyo ni moja kati ya nyadhifa zenye hadhi ya juu na kwa kifupi tu tuseme CCM wamemuamini Jokate, na kwenye makala hii nitakupitisha kwenye safari yake ya maisha tangu anazaliwa mpaka hapa alipofikia.
HISTORIA YAKE, KUZALIWA NA ELIMU
Jokate Mwegelo amezaliwa Machi 20, 1987 huko jijini Washington, D.C. Nchini Marekani, ambapo wakati huo wazazi wake walikuwa wanafanya kazi.
Amekulia jijini Dar es Salaam, Tanzania, na kupata elimu ya msingi katika shule ya Olympio na baadaye St. Anthony High School, na kumalizia elimu ya sekondari katika shule ya Loyola High School.
Watu wengi wanashangaa Jokate kuingia kwenye rada za siasa bila ya kujua kuwa ni mhitimu wa shahada ya sayansi ya siasa na falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
SAFARI YAKE YA UMAARUFU..
Safari yake ya umaarufu ilianza mwaka 2006 aliposhiriki na kushinda mataji ya Miss Kurasini na Miss Temeke yaliyompa tiketi ya kushiriki shindano kubwa zaidi la Miss Tanzania na kuibuka mshindi wa pili.
Nyota ya Jokate ilizidi kung’aa na mwaka 2007, alipata nafasi ya kucheza filamu yake ya kwanza inayojulikana kwa jina la Fake Pastors, akiwa na Vincent Kigosi maarufu kwa jina la Lay, Lisa Jensen, mshindi wa tatu wa Miss Tanzania 2006 na marehemu Adam Kuambiana na hapo ndipo Watanzania walipoona kipaji chake kingine cha uigizaji.
Mwaka 2010 akaonekana katika filamu ya Chumo iliyoandaliwa na Media for Development International, ikielezea kuhusu elimu juu ya ugonjwa wa malaria.
Filamu hiyo ilimpa mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa tuzo ya muigizaji bora wa kike kwenye tuzo za Zanzibar International Film Festival mwaka 2011, na kisha kuchaguliwa kama mwigizaji wa Pan-Afrika katika tuzo za 2012 za Nigeria Entertainment Awards.
Vilevile amepata kuonekana kwenye tamthilia maarufu ya Siri Ya Mtungi, iliyoandaliwa na Jordan Riber na kuongozwa na Karabani, mnamo mwaka 2013, na Mwaka 2014, alicheza uhusika wa “Ndekwa” katika filamu ya Mikono Salama, ambayo ilimpa tuzo nyingine ya Zanzibar International Film Festival akiwa mwigizaji bora wa kike wa filamu za Kiswahili.
Aidha amewahi kujihusisha na muziki ambapo alishirikishwa katika nyimbo kadhaa ikiwemo wa Japo nafasi wa marehemu Cpwaa, na wimbo wa Kings and Queen wa AY akiwa na Amani, kutoka Kenya.
Mwaka 2013, alitoa wimbo wake mwenyewe akiwa na Lucci, unaoitwa ‘Kaka na Dada, na Mwaka 2015, akaachia wimbo wake mwingine unaoitwa Leo akiwa na mwanamuziki maarufu kutoka nchini Nigeria Ice Prince.
Mbali na uigizaji na muziki mwaka 2012 Jokate Mwegelo alifungua kampuni yake ya Kidoti Loving ambayo ina dili na kutengeneza bidhaa mbalimbali za urembo na hasa Nywele.
Kampuni yake ilifanya vizuri sana kwa kuzalisha bidhaa zingine kama mabegi ya shule na ndala, mafanikio hayo yalipelekea mwaka 2017, kupata tuzo ya malkia wa nguvu katika kipengele cha ubunifu wa biashara. Na mwaka huo huo alitajwa kuwania tuzo ya mjasiriamali wa mwaka katika tuzo za Africa Youth Awards.
SAFARI YA SIASA..
Awali Jokate hakujulikana kujihusisha na siasa hadi ulipofika mwaka 2017 ambapo aliteuliwa na Umoja wa Vijana wa chama cha CCM (UVCCM) kuongoza Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi ya umoja huu akiwa Kaimu Katibu wa idara hiyo na mwezi Machi 2018 aliondolewa katika nafasi hiyo kwa azimio la kamati kuu ya UVCCM…
Jokate pia alikuwa miongoni mwa wanachama 450 wa chama tawala cha CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Hata hivyo hakufanikiwa kupata fursa hiyo.
Mwisho wa mwezi Julai 2018 aliteuliwa na Hayati Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe na amefanya kazi kubwa huko ikiwemo kuanzisha kampeni ya Tokomeza Zero iliyosaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa morali wanafunzi kusoma, lakini pia amevitangaza kwa ukubwa vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo ikiwemo hifadhi ya Pugu Kazimzumbwi.
Baada ya Rais Samia kuingia madarakani Juni 19, 2021 alimuhamisha kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya Temeke, ambapo napo pia alimuhamisha na kumpeleka Korogwe alipohudumu mpaka jana Oktoba 1, 2023 alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT)
Kwa miaka ya hivi karibuni Jokate amekuwa akitazamwa kama mfano wa kuigwa na mabinti wengi kutokana na alipotokea na alipo sasa.
Kila la kheri Jokate Mwegelo katika majukumu yako mapya.