Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, John Bocco ametambulishwa kuwa mshambuliaji wa Klabu ya JKT Tanzania.
Bocco ambaye ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania tayari ameshaanza mazoezi na klabu yake mpya tayari kwa kujiandaa na msimu ujao.
Msimu uliopita haukuwa mzuri kwa Bocco kutokana na kutopata nafasi ya kuanza kwenye kikosi na hata kuwa sehemu ya wachezaji wa akiba, huku namba yake ikichukuliwa zaidi na Jean Baleke na Moses Phiri.
Katika msimu huo wa 2023/24 Bocco alicheza mechi tano pekee akitumia dakika 185 uwanjani, akifunga mabao mawili tu.
Taarifa za Bocco kusajiliwa zimeonekana kuwashtua wengi kwani Juni 10, 2024 klabu ya Simba ilimtambulisha Bocco kuwa kocha wao wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ambapo tayari alishaanza kazi hiyo.
Bado haijafahamika kama ni kibunda cha kutosha alichowekewa na JKT ndio kilichomfanya aikache kazi ya ukocha na kurudi kusakata kabumbu au laah.