Miaka 55 iliyopita, tarehe kama ya leo, yaani Julai 10, 1963 Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilizaliwa. Kuanzishwa kwake kulikuwa ni utekelezaji wa Azimio la Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Aprili 19, mwaka huo chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wazo la kuwa na JKT lilitokana na mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth League), uliofanyika Tabora mwaka 1958.

Lilikuwa ni wazo la Katibu Mkuu wa TANU Youth League, Joseph Kizurira Nyerere. Lengo kuu la kutaka kuundwa kwa JKT lilikuwa ni kuwandaa vijana katika mambo makuu yafuatayo:

UADILIFU: JKT iwajenge vijana kuwa waaminifu, wakweli na wa kutegemewa na taifa.

UMOJA NA MSHIKAMANO: Kuwaandaa vijana kuwa jamii yenye mshikamano na umoja wa kitaifa bila kujali itikadi zao za kitamaduni, kisiasa na kidini.

KUJITOLEA: Kuandaa vijana kuwa na moyo wa kujituma na kujitolea.

UZALENDO: Kuwaandaa vijana wawe na moyo wa uzalendo, udugu na kuipenda nchi yao.

NIDHAMU: Kuwafundisha vijana kuwa watiifu na wenye heshima.

KUPENDA KAZI: Kuwaanda vijana kuwa jamii yenye kutekeleza wajibu na moyo wa kupenda kufanya kazi.

JKT ilifanya ina mchango mkubwa mno kwenye ujenzi wa taifa letu. Mafanikio yake hayana mfano. Kwa bahati mbaya, miaka 30 baadaye, yaani mwaka 1993, Serikali ililazimika kusimamisha mafunzo kwa vijana wa kujitolea na mwaka 1994 ikasimamisha pia mafunzo kwa vijana wa Mujibu wa Sheria. Hatua hiyo ilisababisha kudorora kwa kiwango cha juu mno kwa shughuli za msingi za JKT.

Desemba 30, 2005 Rais Jakaya Kikwete, akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza mpango wa kurejesha mafunzo ya JKT, na pia kufufua shule za kitaifa za sekondari.

Rais Kikwete alijipa dhima hiyo ngumu na ya busara kwa kutambua kazi kubwa, nzuri na iliyotukuka iliyotokana na vijana kupita JKT. Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, JKT ndiyo ‘Jando la Taifa’. Kupitia jando hili la kitaifa, vijana wa rangi zote, makabila, dini hukutana, huishi na kufanya mafunzo na kazi wakiwa pamoja kama ndugu wamoja.

Uamuzi wa Rais Kikwete uliwagusa Watanzania wengi hasa wale waliopata bahati ya kupita kwenye chombo hicho na kufaidi mafunzo na malezi yake. Watu wengi, wakiwamo wabunge waliunga mkono uamuzi wa rais.

Haikuwa kazi rahisi kuirejesha JKT hasa kutokana na sababu za kiuchumi. Pamoja na yote hayo, ilipotimu Machi 26, 2013 mafunzo ya JKT yalirejeshwa upya katika kambi ya Ruvu mkoani Pwani. Wabunge 22 walikuwa miongoni mwa wale walioanza kupata mafunzo hayo.

Miaka 55 si haba. Kama taifa, tumejitahidi kuwa na mipango madhubuti yenye kulenga kuwaandaa vijana ili wawe raia wema na wazalendo. Mataifa mengi yana kiu ya kuwa na utaratibu wa aina hii, lakini yameshindwa. JKT ingekuwa ni majengo, bila shaka wengi wetu tungejitokeza kusifu ukubwa na uzuri wake. Kwa kuwa si kitu kinachoonekana moja kwa moja kwa macho, imetuwia vigumu baadhi yetu kujua faida nyingi na nzuri zilizotokana na chombo hiki adhimu.

Kwa wale waliopata mafunzo ya JKT, sijawahi kumsikia anayebeza au kupuuza faida alizopata. Wale waliopita huko, hata kama leo wana mitazamo tofauti ya kisiasa, bado wameunganishwa na JKT. Mimi hupenda kusikiliza simulizi za waliopita JKT katika makambi mbalimbali. Huwasikia wakiwakumbuka maafande wao. Hurejea nyimbo za kizalendo. Husimulia namna walivyokabiliana na mazingira magumu na kuyamudu, na kadhalika na kadhalika. Kwa ufupi ni kuwa katika haya mafanikio tunayoyaona leo ya Watanzania kuwa wamoja, mchango wa JKT ni mkubwa kweli kweli.

JKT imewafanya vijana wa Tanzania wamudu kuishi katika mazingira tofauti na yale ya asili yao. Yamewafanya vijana wa Tanzania waoleane bila kujali makabila au kanda wanazotoka. JKT imewaunganisha Watanzania kiasi cha kuwafanya watu wajione ni wamoja – wasiokuwa na vimelea vya ubaguzi. Hii ni tunu kubwa isiyopaswa kupuuzwa au kufanyiwa mzaha.

Kuna wakati tulikuwa na mjadala uliohusu faida za JKT. Wengi wetu kwenye ule mjadala tukawa tunaeleza namna Jeshi hili lilivyowaunganisha vijana wa Tanzania waliopata bahati ya kupita huko. Tukawa tunajenga hoja ya faida kama ile ya kuwapo uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Upande wa waliotupinga ukatuuliza swali kwamba, “Kama JKT imejenga uzalendo, mbona mafisaidi wengi ni wale waliopita huko?” Hili lilikuwa swali gumu, lakini lenye kujibika. Hata wanafunzi wa Yesu wapo walioasi. Hao wachache hawawezi kuondoa kazi nzuri ya wale waliotii na kuiishi imani.

Inakisiwa kuwa idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 55 sasa, asilimia 84 kati yao ni vijana walio chini ya umri wa miaka 40! Kwa maneno mengine, asilimia 16 pekee ya Watanzania ndio sisi tunaoitwa wahenga! Takwimu hizi hazina budi kutufumbua mambo na kuwa chachu kwetu ya kuiandaa Tanzania njema kwa kizazi kijacho. Kundi hili lisipoandaliwa au kujengewa misingi ya uzalendo na utii, Tanzania inaweza kuwa kwenye hali mbaya.

Jambo linalosikitisha zaidi ni kuona yale mambo mazuri – pamoja na JKT – yaliyokuwa misingi ya kuujenga umoja na uzalendo wetu, yanafutika kwa kasi. Kwa mfano, Chipukizi ilikuwa sehemu nzuri mno iliyowaandaa watoto kuwa wazalendo wa baadaye wa taifa letu. Tuliimba nyimbo zilizotujengea uzalendo. Tulishirikiana watoto wa rangi, makabila, kanda na matabaka yote. Leo Chipukizi haipo, na kama ipo, basi ni ya chama fulani. Vijana hawawezi kujengewa uzalendo kwa misingi ya tofauti zao za kiitikadi. Haiwezekani CCM wawe na Chipukizi, Chadema wawe na Chipukizi, CUF wawe na chipukizi wao halafu tutarajie kuwa na taifa lililo moja. Tunapaswa kuangalia kitu au vitu gani vinavyoweza kuwaunganisha Watanzania hata wakaweza kujiona wamoja. Vitu hivyo au hayo mambo tuyaainishe sasa.

Tulikuwa na shule za kitaifa za sekondari. Leo ni kama hazipo. Shule hizi, pamoja na JKT zilisaidia kuwajenga Watanzania na kuwafanya wajione ni wamoja. Haya mambo hatuna budi kuyarejea ili pamoja na JKT, tuweze kuwa na vijana waliojengwa na kuwa wazalendo wa kweli kwa taifa lao.

Tulisoma vitabu vilivyofanana. Tuliimba nyimbo za kitaifa zilizofanana. Mfano, wakati wa mchaka mchaka tuliimba: “Alisemaaa alisema alisema Mwalimu [Nyerere] alisema

vijana wangu wote mmelegea, sharti muanze mchaka mchaka … chinja”. Leo Watanzania hatuna nyimbo wala salaamu za kitaifa vizazotuunganisha. Sana sana tuna salaamu za Bwana Asifiwe, Asalaam Aleikum, Tumsifu Yesu Kristo, na kadhalika. Sijasikia salaam ya wasioamini kwenye hizo imani. Tunaweza kudhani hizi salaamu ni za maana kwa sababu zinagusa imani zetu, lakini ukweli ni kuwa hizi si salaamu za kuwaunganisha watu wa taifa moja. Zinaibua hisia za udini. Kwanini tusiwe na salaamu fulani fulani ya kitaifa isiyo na vimelea kwa kiimani? Zamani kulikuwa na ‘Uhuru”, na aliyejibu akasema “na Kazi”. Je, tumekosa ubunifu?

Tunaposhangilia timu ya taifa hatuna wimbo wa kututambulisha kuwa sisi ni Watanzania. Hatuna. Tunahangaika kutafuta ‘vazi la taifa’ (nguo) badala ya ‘vazi la moyo na akili’ ambalo ni uzalendo. Uzalendo si suala la hiari kama lilivyo vazi. Uzalendo ni suala la kufundishwa na kufundishika. Uzalendo unaanza kujengwa kwa watoto, na si kusubiri hadi watu wawe wameshaota sharubu tayari.

Kuna mambo yanayopaswa kuwa chachu ya kutuwezesha kurejea kwenye maudhui ya kuwajenga vijana ili wawe raia wema. Mambo yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii yanatosha kuonyesha ni kwa namna gani uzalendo wa baadhi ya Watanzania ulivyoanza kutoweka na umuhimu wa kuanza kuujenga kwa kasi inayostahili.

Tunaelekea kuacha kuzungumza ‘lugha moja’ ya ujenzi wa nchi. Tunaona Serikali ikinunua ndege, jambo ambalo ni muhimu, lakini kuna genge linalopinga au kubeza uamuzi huo. Hili si jambo zuri kwa nchi yenye watu wanaotaka kusonga mbele kimaendeleo.

Nawapongeza JKT na kuwaomba makamanda na wapiganaji waendelee kuwa ‘chuo’ mahiri cha kuwaandaa vijana ili wawe na moyo wa uzalendo, utaifa, kujitolea, na kupenda kuchapa kazi. Tuhakikishe tunakuwa na vijana walio raia wema na walio tayari kulijenga taifa. Tuwe na kizazi kinachokosoa panapostahili kukosoa, na kusifu kunakostahili kufanya hivyo. JKT iwe chuo cha kufuta tabia mbaya ya vijana ya kulalamika tu, badala yake kiwe chuo cha kufundisha ujasiri na uthubutu wa kuyashinda maisha. Hongera JKT.