JKT ni mtima wa Taifa (5)Napenda kukumbusha wahusika kuwa wakati utaratibu wa kuwaita vijana kwa mujibu wa sheria ukiandaliwa katika ile (White Paper No. 2 ya mwaka 1966), katika ibara ya 9, kulianishwa masomo ya kuwafundisha vijana wote katika JKT.
Masomo kadhaa yalifikiriwa katika mafunzo yale. Masomo yaliyoainishwa kuwafundisha yalikuwa 12, nayo ni:-1. Misingi ya Siasa (Principles of Politics).2. Historia ya Siasa (Political History of Tanzania).3. Serikali (The Government).4.
Ujamaa na Uchumi wa Kujitegemea (Socialism and Economic of Independence).5. TANU NA ASP (TANU and the ASP Organisation).6. Elements of Book- Keeping.7.
Mambo ya kila Siku ya Afrika na Ulimwengu (International and African Current Affairs).8.
Jiografia ya Elimu ya Msingi tu (Geography for ex Primary).9. Historia ya Elimu ya Msingi tu (History for ex Primary).10. Kiswahili na Maandiko yake (Swahili language and literature).11. Utamaduni wa Mtanzania (music, drama and dancing, nyimbo, ngoma, traditional arts and crafts).12. Michezo (sports and games).
Hapa ndipo ningependa kuuliza Serikali imejiandaaje katika mafunzo ya namna hiyo? Somo namba 5 najua kabisa halitakuwapo, maana itikadi ya chama tawala kwa mfumo wa vyama vingi haiwezekani.
Walimu wa hayo masomo mengine wameandaliwa? Vyama vya siasa vimekaa kukubaliana kuwa katika ujenzi wa Taifa letu lenye uzalendo nini kifundishwe katika URAIA? Hii ni changamoto kwa viongozi wa JKT wakati huu. Kwa upande wa mafunzo ya kijeshi sina shaka yoyote, maana JWTZ ina wataalamu wengi na wazuri sana.
Uwezo wao ulionekana katika Yita ya Uganda kumwadhibu nduli Idi Amin na siku za karibuni kule Visiwa vya Ngazija (Comoro). Hivyo mafunzo ya kijeshi ninaamini mitaala ipo na wakufunzi wapo.
Hapa ningeomba nitoe ushauri wa bure kabisa. Uongozi wa JKT na wabunge watarajiwa kujiunga katika kambi za JKT, wamwone Balozi Job Lusinde, kuruta wa Ruvu Kikosi Kazi B, akiwa Mbunge na Waziri mwaka 1968.
Uzoefu wake kwa Kamanda ODDO na Afande Deis Amdelemani na shuruba za wiki zile mbili, utasaidia sana kuwapa moyo waheshimiwa wabunge vijana watarajiwa kujiunga JKT mwakani.
Hawapaswi kuogopa maisha mapya katika shule za JKT (CTS).Nimalizie kwa kusema hali ya uzalendo inahitajika sana wakati huu katika nchi yetu.
Uongozi wa JKT umeonesha wazi utayari wake kufunza vijana wote maadili mema ya kitaifa (national ethics) kujenga umoja, kuaminiana na mshikamano kwa vijana wote wa mujibu wa sheria, wa kujitolea na watu wazima (mature age) wanaoomba kutoa huduma hii kwa Taifa letu.
NIA YA KUJENGA TAIFA LETU SOTE TUNAYO; SABABU ZA KUJENGA TAIFA LETU SOTE TUNAZO NA UWEZO WA KUJENGA TAIFA LETU UPO. Kwa nini tusifanikiwe? Kila kijana wa nchi hii ajione kuwa yeye ndiye hasa mjenzi wa Taifa hili.
Warumi wa kale walikuwa na ‘motto’ namna hii “Potuerunt hi, potuerunt he, quare non ege?” yaani kama kijana yule ameweza na msichana yule ameweza, kwa nini mimi (fulani jina lako) nisiweze? Basi, nami nitaweza tu.
Twende kazini kulijenga Taifa hili kupitia JKT ambacho ndiyo MTIMA WA TAIFA HILI.
Kazi moja tuliyonayo mbele yetu nayo ni kujenga Taifa la TANZANIA.
Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).