Nimejaribu kurejea kirefu maneno ya Mwalimu kuonesha uchungu wake kwa wasomi waliosema miili itakwenda, lakini mioyo yao haitakuwa huko National Service.
Hili lilimchoma sana Mwalimu, hasa akitafakari kuwa mwalimu au daktari akiingia National Service basi ‘limwili’ litakuwa pale, lakini moyo wake wa kuhudumia watoto darasani au wagonjwa hospitalini hautakuwapo. Hii maana yake hawatafanya kazi zozote za taaluma zao.
Kuanzia Aprili 1967 vijana wa mujibu wa sheria wamekuwa wakimiminika kwa wingi kuitika mwito ule wa Huduma ya Taifa. Si hao tu, hata watu wazima wenye moyo wa uzalendo wamekuwa wamejiunga katika kambi za JKT kwa mpango wa kujitolea miezi mitatu. Bila kumung’unya maneno, tangu Sheria hii Na. 64 ya 1966 ianze kutumika, vijana wengi wa mujibu wa sheria wamepikika katika kambi za JKT.
Aidha, viongozi kadhaa wa ngazi ya kitaifa wamepikwa katika kambi hizi. Kwa kuwa JKT ilikuwa inapanuka, basi shule za mafunzo ya awali ziliongezwa kutosheleza mahitaji mapya. Kwa hiyo, kambi za Makutupora na Oljoro nazo mwaka 1969 zikageuzwa kuwa shule za mafunzo, yaani zikawa CTS.
Hatimaye kambi za Bulombora, Msange, Mlale na Mgambo nazo zikawa CTS kwa kutoa mafunzo ya awali. Sasa JKT ikawa na kambi nane zenye kutoa mafunzo ya awali. Kambi hizo ni Ruvu (Pwani), Mafinga (Iringa), Oljoro (Arusha), Mlale (Ruvuma) Makutupora (Dodoma), Mgambo (Tanga), Msange (Tabora) na Bulombora (Kigoma).
Mwamko wa kujitolea kwa huduma ya Taifa ulikuwa mkubwa sana katika Taifa letu. Wazee wengi hasa waliokuwa makatibu tarafa, wakuu wa wilaya, wabunge hadi baadhi ya mawaziri walijiunga na JKT kwa ule utaratibu wa mature age yaani watu wazima kujitolea kwa huduma kwa Taifa.
Kama nakumbuka vizuri, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwaunga mkono baadhi ya wabunge na baadhi ya ma-DC pale Mafinga katika Operesheni Mwenge. Nilikuwa Mwalimu wa siasa pale Mafinga wakati huo.
Basi, aliagiza atayarishiwe kulala pale pale kambini ili ashiriki vipindi vya jioni na mchakachaka asubuhi yake, kisha ndipo azungumze na wanakambi wote pale; yaani alitaka akutane na wabunge wote na ma-DC na wengine wote. Alifika kikosini saa 10 alasiri Jumatatu, Julai 22 na kuondoka Jumanne, tarehe 23 baada ya chakula cha mchana saa nane kurejea Dar es Salaam.
Kabla yake, huko nyuma wazee wa Operesheni Kazi B waliingia Ruvu Februari 10, 1968 na kufanya gwaride lao la kuhitimu katika Uwanja wa Taifa Februari 24, 1968. Kundi hili liliongozwa na Waziri Mkuu Rashidi Kawawa, Spika wa Bunge Chifu Adam Sapi Mkwawa, mawaziri kadhaa wakiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais Aboud Jumbe Mwinyi, Job Lusinde, Johnson Kihampa, Andulrahman Babu, Hasnu Makame na wabunge kadhaa. Walihudumia Taifa kwa wiki mbili.
Nimeamua kuandika makala hii, kwanza, kuonesha furaha yangu kwa JKT kupata uongozi mpya wenye dira ya kujenga UZALENDO kwa vijana wa Taifa hili na kufufua uadilifu na uaminifu miongoni mwa kizazi kipya cha Taifa hili.
Uadilifu wa mtu mmoja mmoja na hatimaye wa Taifa zima unahitajiwa sana wakati huu, ili kufuta dhana iliyoanza kuonekana kuwa baadhi ya viongozi wa Taifa hili wanaonesha tabia ya UFISADI na wanatumia madaraka yao vibaya na hawajali wala hawaonei uchungu mali za umma!
Hali namna hii inalivunjia heshima Taifa letu. Taifa huru halina budi kuwa na maadili mema. Wazungu wanasema integrity of a nation ambako kila mmoja analionea fahari Taifa namna hiyo.
Pili, nimefurahishwa na tamko la Serikali wakati wa Bunge la Bajeti 2012/2013 kuwa mwaka ujao utaratibu wa kuwaita vijana wa mujibu wa sheria utarudishwa katika chombo hiki.
Si hilo tu, bali tamko lilionesha kuwa nafasi zitatolewa kwa waheshimiwa wabunge vijana wenye moyo wa uzalendo wa kulijenga Taifa letu kupita katika JKT kutoa huduma kwa Taifa lao. Ni uamuzi wa busara na ningependa sana kuwahimiza wajiunge upesi.
Kwa mshangao sana nilisoma makala ya ndugu yangu Charles Charles katika JAMHURI toleo la Jumanne Julai 24-30, 2012 uk. 12. Makala ile mimi binafsi sikuifurahia; kisa? Kwanza kabisa iliwakatisha tamaa waheshimiwa wabunge iliposema, “JKT ya wiki tatu kwa wabunge ni utani!”
Mimi nikiwa Mwalimu wa Siasa katika JKT tangu mwaka 1964 na niliyeona mabadiliko mbalimbali ya JKT, nilishuhudia wabunge wakiwamo mawaziri waliopitia Operesheni Kazi B pale Ruvu kwa wiki mbili walivyonufaika na kusifia mafunzo yale. Sikuelewa mwenzangu Charles anayesema wiki tatu ni utani ana maana gani!
Pili, nilishuhudia Baba wa Taifa pale Mafinga akishirikiana na waheshimiwa wabunge kina Maalim Nabahani (Lindi), Yakobo Chibwana (Tunduru), Dolar (Kisarawe), Kibuga (Iringa) na ma-DC kina Haruna Taratibu (Dodoma), Iddi Sungura (Tabora), Madenge (Bagamoyo) na wengine kadhaa wakihenya.
Ushauri wangu ni huu. Mtazamo wetu uwe wa kujenga (constructive approach) Taifa na kamwe usiwe wa kukatishana tamaa (negative approach).
Ndugu yangu Charles ameelezea kirefu uzoefu wake kule Msange Tabora na kambi nyingine za JKT, ambamo mimi mzee nimezipitia (mathalani Buhemba nikiwa CO mwaka 1971-1972) Rwamkoma tulianzisha enzi za Mzee Nkulila mwaka 1966, Mgulani ndipo nilipoingilia Jeshi mwaka 1964.
Tukija kwa upande wa JWTZ, nadhani waheshimiwa wabunge hawaombi kupitia JWTZ, bali wao wanataka kutoa huduma kwa Taifa lao angalau kwa muda. Hili litasaidia wanapojadili bajeti, basi watasaidia JKT iongezewe uwezo wa kutekeleza majukumu yake.
Kwa mtazamo wangu mtu mwenye moyo wa kujenga uzalendo katika Taifa hili hata akikaa kwa siku mbili tu mahali au katika taasisi fulani, inampa wigo mpaka zaidi katika maisha. Kule kuchanganyika na wengine na kufanya mambo pamoja kunasaidia sana kumjenga mtu na kusiliba upungufu katika uhusiano.
Ndiyo sababu nikasema wazo la waheshimiwa wabunge kujiunga kwa muda katika maisha ndani ya kambi za JKT, ni hatua kubwa sana na inaonesha ukomavu wa fikra katika kujenga uzalendo ndani ya Taifa.
Ndugu Charles Charles awaulize baadhi ya waheshimiwa wabunge waliopata kuswekwa na kulala katika mahabusu yoyote ile katika gereza angalau kwa siku chache hivi ataona wigo mpana wa adha wanayopata mahabusu? Hata kama alilala siku moja tu inatosha. Atakuwa amejionea mengi sana . Hivyo kukaa kambini siku 21 tutasaidia sana kuwajengea umoja na uzalendo wa kitaifa.