Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

JESHI la kujenga Taifa (JKT )limetoa wito kwa Vijana waliohitimu Elimu ya Sekondari Kidato cha sita kwa Mwaka 2024 kutoka Shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria ili kujengewa uzalendo , umoja na stadi za maisha.

Aidha Jeshi hilo limeonya baadhi ya watu wasio waadilifu kuacha vitendo vya kitapeli kwani mafunzo hayo yanatolewa bure huku Jeshi hilo likibainisha kuwa Vijana watatakiwa kuripoti wakiwa na Vifaa mbalimbali ikiwemo Shuka za kulalia.

Hayo yameelezwa leo Mei 24,2024 na Brigedia Jenerali Hassan Mabena ambaye ni Mkuu wa utawala tawi la JKT,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu wito huo wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria Mwaka 2024 .

Ametaja kambi ambazo vijana hao wamepangiwa kuwa ni JKT Rwamkoma-Mara,JKT Msange-Tabora,JKT Ruvu-Pwani,JKT Mpwapwa,Makutupora JKT-Dodoma,JKT Mafinga-Iringa,JKT Mlale-Ruvuma,JKT mgambo na JKT Maramba-Tanga.

Nyingine ni JKT Makuyuni-Arusha,JKT Bulombora,JKT Kanembwa na JKT Mtabila-Kigoma,JKT Itaka-Songwe,JKT Luwa na JKT Milundikwa-Rukwa,JKT Nachingwea-Lindi,JKT Kibiti-Pwani na Oljoro JKT-Arusha.

“Tunawataka vijana kuripoti wakiwa na vifaa ambavyo watavipata na orodha kamili ya majina ya Vijana hao na Makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo ya makambi hayo yalipo na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz,”amesema Brigedia Jenerali Mabena.

Licha ya hayo amesema, “Naishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani imeendelea kuboresha makambi na vijana wote watakao wasili hakutokuwa na changamoto yoyote,

” Mafunzo haya yamekuja baada ya kuona sio wote wanaishia kuwa wanajeshi au waajiriwa hivyo wengine waweze kutoka na ujuzi uwasaidie huko watakapokwenda,”amesema