Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kituo cha matibabu ya magonjwa ya moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) kimezidi kutanua wigo wa matawi yake nchini.
Kituo hicho ambacho kiliasisiwa nchini mwaka 2015 mpaka kufikia mwaka huu 2025 kinakwenda kutimiza miaka 10 ya uendeshwaji wake huku kikijivunia baadhi ya hatua muhimu zilizopigwa na kituo hicho katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Kituo hicho kimezindua rasmi tawi lake jipya maeneo Oysterbay ,Dar es salaam litakalokuwa likitoa huduma kwa wananchi wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ya moyo.
Akiongoza hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, Waziri wa afya, Dkt:Jenista Mhagama amekipongeza kituo hicho kwa kuchochea kuleta unafuu kwa watanzania kupata huduma za kimatibabu ya moyo ndani ya nchi na ukilinganisha gharama za kubwa za matibabu zinazotolewa nnje nchi.
Aidha Waziri Mhagama ameelezea mipango ya serikali kupitia wizara ya Afya katika kuboresha sekta ya nchini ambapo mpaka kufikia sasa zaidi ya billioni 30 katika kuboresha sekta hiyo.
“Naipongeza taasisi ya JKCI, kwani kwa kupitia wao wamesaidia kupunguza gharama za wagonjwa kwenda kutibiwa nnje ya nchi na kuleta wepesi wa upatikanaji wa huduma ndani ya nchi.”
“Serikali imezidi kuwekeza kwenye vifaa tiba na uchunguzi, zaidi ya billioni 30 zimetengwa kwaajili ya kuboresha ujuzi katika sekta ya afya.”
Dkt: Mhagama ameongeza pia kwa kutoa rai kwenda kwa taasisi hiyo kuongeza jitihada za kukitangaza kituo hicho kimataifa kupitia mabalozi wa nchi zenye mahusiano mazuri ya kidiplomasia walioko hapa nchini ili kituo hicho kizidi kutanua wigo wake kwenye anga za kimataifa.
Kwa upande mwingine pia Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho cha JKCI, Dkt: Peter Kisenge akihutubia wakati wa uzinduzi wa tawi la kituo hicho amesema kuwa wanajivunia kuwa na vifaa tiba vya kisasa na timu ya madaktari bingwa wa kimataifa huku akiongeza kuwa lengo lao ni kusambaza kituo hicho kila sehemu .
Kwa mujibu tafiti Kituo cha JKCI kinatajwa kama kituo namba moja ukanda wa Afrika mashariki na kati katika utoaji huduma za kimatibabu ya magonjwa ya moyo.
Tawi hilo la kituo hicho la Oysterbay limezinduliwa rasmi leo hii na litakuwa likitoa huduma zake kwa saa zote 24 .