Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata tuzo ya ushindi wa utoaji wa huduma bora za afya kwa mwaka 2025 katika kundi la Hospitali maalum na Taifa.
Tuzo hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kufunga maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa yaliyokuwa yakifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma.

Akitoa tuzo hiyo Mhe. Jenista ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuzingatia usafi wa maeneo ya kazi, utoaji wa huduma bingwa na bobezi, pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wateja (customer care services).
“Taasisi hii imezingatia usafi wa mazingira na usalama kwa wagonjwa wanaowahudumia, nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya”, alisema Mhe. Jenista
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI itaendelea kuboresha huduma inazozitoa huku ikiendelea kufikisha huduma hizo kwa wananchi waliopo mikoani kupitia kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwekeza vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi yetu na kuifanya taasisi hii kuwa kituo cha ubora Afrika Mashariki na kati katika kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Naye mkazi wa Dodoma Grace Ringo ameipongeza Taasisi hiyo kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji matibabu ya moyo.
“Taasisi hii iliweza kuokoa maisha ya mtoto wangu aliyekuwa na matundu mawili kwenye moyo wake, walimfanyia upasuaji wa kuziba matundu hayo mwaka 2014 akiwa na miezi nane na sasa ana miaka 11 na afya yake ipo vizuri kabisa”, alisema Grace
Aidha Grace amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Taasisi hiyo na kuweza kusaidi watoto kama ambavyo wakwake alisaidiwa.

