Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Namtumbo

Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI ), imeanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Akizindua huduma hizo Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alisema, kuwa zoezi la uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi litasaidia kuokoa maisha ya watu wengi ambao awali walishindwa kupata huduma hizo kutokana na gharama ya kufuata matibabu nje ya wilaya hiyo ikiwemo Hospitali ya Rufaa Songea,Peramiho na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa akiongea na wananchi wa jimbo lake ambao wamefika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo kucheki afya zao bure.

Kawawa,ameishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kuleta madaktari bingwa watakaotoa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo, uzito mkubwa na presha.

Amesema,zoezi hilo litasaidia kuokoa maisha ya Watanzania hususani wakazi wa ĺNamtumbo wanahitaji kupata huduma za uchunguzi lakini kutokana na changamoto mbalimbali hawakuweza kuzipata.

“Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inatarajia kuitumia Hospitali ya Wilaya Namtumbo kama kituo kidogo cha uchunguzi wa matibabu ya moyo ili kusaidia wananchi wenye hali ya chini mkoani Ruvuma kupata huduma karibu za matibabu”alisema Kawawa.

Hata hivyo Kawawa,ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta zaidi ya Sh.bilioni 2.3 zilizosaidia kuboresha miundombinu ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo.

Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Namtumbo wakiwa kwenye foleni ya kuchekiwa afya ya magonjwa ya moyo.

Amesema,fedha hizo zimetumika kujenga jengo la huduma za meno, macho,jengo la mama ngojea na jengo la mama, baba na mtoto.

Kawawa ametaja miundombinu mingine iliyotekelezwa katika sekta ya afya kuwa ni ujenzi wa kituo cha afya Ligera na Magazini vilivyogharimu Sh.bilioni 1 na vifaa tiba vilivyosambazwa katika Zlzahanati na vituo vya afya wilayani humo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt Aaron Hyera amema uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya afya uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita umesaidia sana kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati na baada ya kujifungua.

Dkt.Hyera,uwekezaji wa miundombinu katika sekta ya afya wilayani humo umewezesha kutoa huduma kwa ubora zaidi hasa ikizingatiwa baadhi ya vijiji viko umbali wa zaidi ya kilometa 200 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Namtumbo mjini na vituo vya afya vilivyopo.

“Hii ni mara ya tatu kuwa kambi ya uchunguzi na matibabu ya huduma za moyo kutoka kwa Madaktari Bingwa katika wilaya yetu, tunaishukuru sana Serikali na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kwa kuleta huduma hizi” amesema.

Pia amesema,wataalam hao watasaidia kuwapatia ujuzi zaidi wataalam waliopo Wilayani humo hasa kwenye masuala ya moyo na wananchi watapata huduma za magonjwa hayo bila kwenda Mikoa mingine kufuata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa kuwa zitapatikana katika Hospitali ya Wilaya na vituo vya afya vilivyopo katika Wilaya hiyo.

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Baraka Ndelwa amesema, zoezi hilo litafanyika kwa muda wa wiki moja na katika Hospitali ya Wilaya,kituo cha afya Lusewa na kituo cha afya Mputa.

Amesema ,katika zoezi hilo wanapima magonjwa ya moyo, kisukari na wananchi watapata elimu ya namna gani ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa na wale watakaobainika kuwa na shida kubwa watapewa rufaa ya kwenda Muhimbili.

Ametoa wito kwa wananchi wa Namtumbo, kutumia fursa hiyo kwenda kupata huduma ya uchunguzi wa magonjwa hayo ili kufahamu hali za afya zao.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili kuhusiana na huduma hizo wameishukuru serikali kwa kuwaletea huduma hizo ambazo awali walikuwa wanashindwa kumudu kutokana na gharama za upimaji lakini pia imewarahisishia kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo wamemuomba Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluu Hassan kuona umuhimu wa kuwawekea huduma hizo kuwa endelevu na si vinginevyo.

Please follow and like us:
Pin Share