TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)–Hospitali ya Dar Group leo imezindua mtambo wa kisasa wa kuzalisha hewa ya oksijeni wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 500, utakaopunguza gharama za ununuzi wa oksijeni kutoka katika vituo vingine.

Mtambo huo umenunuliwa nchini Uturuki na kukabidhiwa kwa JKCI-Dar Group na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ambapo kiasi cha Sh milioni 320 zilitumika kwaajili ya ununuzi wa mtambao na Sh milioni 70 kwaajili ya kasha la kuhifadhia mtambo, usafirishaji na Sh milioni 136 kwaajili ya kusimika na kusambaza hewa wodini na sehemu nyingine zenye uhitaji.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Delila Kimambo amesema mtambo huo unatumia umeme na kuzalisha hewa ya oksijeni yenye ujazo wa milimita za mraba 21 yenye kasi ya mita tano kwa saa wakati wa kujaza.

“Una vifaa vingi ndani yake vikiwemo kifaa cha kupima ubora wa oksijeni, kifaa cha kujaza hewa, tanki la kupokea hewa ina lita 1000 na talinalopokea hewa ya oksijeni wakati wa kutoa lina lita 1000,” amesema.

Dk Kimambo amefafanua kuwa kutokana na umuhimu wa hewa hiyo JKCI –Dar Group ilikuwa inanunua oksijeni kwa kujaza mitungi kutoka kwa watoa huduma mbalimbali kwa gharama kubwa hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuishiwa oksijeni au kutopata iliyo salama.

Amesema mtambo huo utapunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia zaidi ya 3.7 kwa mwaka wa kwanza na kila sehemu inayotumia oksijeni imeunganishwa.

“Hivyo italeta urahisi wa utoaji huduma kwa wagonjwa wetu na pia uzalishaji ukiongezeka tutatoa huduma hii kwa hospitali zinazotuzunguka,

JKCI-Dar Group ina vitanda na inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje 400 hadi 600 kwa siku,” amefafanua.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu ambaye katika hotuba yake fupi, ameomba gharama za oksijeni ziwe chini ili kuusaidia Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF) kutokulipa gharama nyingi kwa wagonjwa.

“Sasa kuna nyumba za ICU zina chaji Sh 500,000 bila dawa, Mungu ametupa oksijeni na mradi huu uwe sehemu ya kuwapunguzia gharama na wao wapate huduma safi. Tumuige Rais (Samia Suluhu Hassan) shughuli zake ni fupi lakini zina matokea makubwa katika nchi yetu. Tumepata Rais anayependa watu na taifa lake, anahakikisha watu wasipate mahangaiko ya afya.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika afya kwenye Jimbo la Ilala, Kata ya Mchikichini pia anajenga hospitali kubwa ya Sh bilioni 5.3 ambapo kituo hicho kitakuwa mteja wa oksijeni itakayozalishwa.

Kwa upande Mkurugenzi wa Idara ya afya ya Uzazi, Mama na Mtoto akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya afya, Dk Ahmed Mkawani amesema mtambo huo utasaidia kuhudumia wananchi.

“Wizara inawapongeza kwa kubadili mwonekano wa huduma hapa mmekunza ajira za Watanzania hapa Dar Group na JKCI imeondoa rufaa za nje ya nchi mambo yote ya moyo yanafanyika hapahapa.

Dk Makwani amesema sasa hospitali zote za rufaa nchini zinazalisha oksijeni na mahangaiko sasa yamepungua.