*Yabainika ndiye mwasisi wa makundi CCM

*Akemea dhambi iliyomwingiza madarakani

 

Staili ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete, inatajwa kwamba haitakuwa na msaada mkubwa wa kuiwezesha Sekretarieti mpya kutekeleza ahadi na maazimio ya Mkutano Mkuu wa Nane uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni.

Madai yameanza kuibuliwa kwamba hata kushindwa kung’ara kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kulitokana na Mwenyekiti kutokuwa na msimamo wa dhati katika baadhi ya mambo mazito.

 

Unatolewa mfano kwenye suala la kujivua gamba ambalo Mwenyekiti Kikwete ameonyesha kuwagwaya wanachama wanaodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kuikosesha mvuto CCM mbele ya umma.

 

Habari kutoka ndani ya CCM zinasema kwamba mara kadhaa Mwenyekiti alishauriwa achukue uamuzi mgumu dhidi ya wanachama wanaotuhumiwa, lakini mara zote amekuwa akipoza mambo.

 

“Mambo yote mazito yanayoamuriwa na vikao vya chama yamekuwa wakipoozwa na Mwenyekiti. Mukama alidhani anaweza kuungwa mkono na Mwenyekiti, matokeo yake akajikuta akijichumia lawama kutoka kwa baadhi ya wanachama,” amesema mmoja wa wanachama wa CCM.

 

Anasema kwa kawaida Mwenyekiti Kikwete amekuwa mtaalamu wa “kukwepa lawama”, si ndani ya Chama pekee, bali hata serikalini. Ni kwa sababu hiyo, maazimio mengi (soma uk. 8 & 9) ya Mkutano Mkuu wa Nane yanaweza yasitekelezeke, hasa suala la kupambana na rushwa ndani ya chama.

 

“Mara zote hataki aonekane kuwa yeye amechukua uamuzi fulani wa kuwaudhi wengine, si ndani ya chama tu, bali hata serikalini. Hakuna waziri aliyeondolewa na Rais Kikwete mwenyewe. Alichofanya ni kuhakikisha kelele za wananchi zinakuwa nyingi na yeye kuamua kuchukua uamuzi wa kumwondoa waziri au mawaziri kwa kigezo cha ‘sauti ya wananchi’,” amesema.

 

Mifano inayotolewa ni ile ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kuandamwa hadi kujizulu bila Rais Kikwete kusema jambo lolote wakati wote wa sakata hilo.

 

“Lowassa alipojiuzulu ndipo akazungumza mbele ya wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba ile ilikuwa ajali ya kisiasa,” amesema.

 

Mfano mwingine ni wa miezi kadhaa iliyopita ambako mawaziri walituhumiwa kwa rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na uzembe.

 

Muda wote Rais alikaa kimya, na ndipo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alipoweka mkakati wa kuwashawishi wabunge kuorodhesha majina kwa nia ya kumwondoa madarakani Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

 

Kwa kuona kuwa huenda kweli Pinda angeg’olewa, Rais Kikwete aliamua kufanya mabadiliko makubwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa baadhi ya mawaziri; na hivyo kuinusuru Serikali yake.

 

Kwa mririko wa matukio hayo na mengine, ndiyo maana baadhi ya wana CCM wanasema wazi kwamba uongozi mpya ndani ya chama hicho unaweza usifanye lolote la maana kutokana na kukwazwa na Mwenyekiti Rais Kikwete.

 

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula, ametamba kwamba ndani ya miezi sita chama hicho kitakuwa kimewashughulikia wanachama wanaotuhumiwa kuingia madarakani kwa rushwa.

 

Ahadi hiyo inaelekea kuwa ngumu mno kutekelezeka, hasa ikizingatiwa kuwa rushwa ilitamalaki mno kwenye uchaguzi ndani ya chama hicho katika ngazi nyingi. Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, ni miongoni mwa waliolalamikia vitendo vya rushwa baada ya kuangushwa katika uchaguzi wa ujumbe wa NEC Wilaya ya Hanang’.

 

Dk. Benson Bana amtetea

 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, yeye ametetea staili ya uongozi wa Rais Kikwete, akisema inakidhi muktadha wa siasa za kileo.

 

Ameiambia JAMHURI kwamba Sekretarieti mpya ya CCM pekee haiwezi kufanya kitu chochote cha maana, bali kinachotakiwa ni kuwa na mfumo wa uongozi unaowajibika pamoja.

 

“Sekretarieti ni kama Baraza la Mawaziri, inafanya kazi kwa mfumo kama ilivyo kwa Baraza ambalo linafanya kazi kwa mujibu wa Katiba.

 

“Utendaji wa Rais Kikwete ndiyo unaofaa kwa siasa za kisasa, ukiwa Rais dikteta unaweza usifanikiwe. Amejitahidi sana kuweka mfumo. Hakuna kiongozi ambaye ni mtimilifu kwa asilimia mia moja. Ukiona kiongozi ni mtimilifu kwa asilimia mia moja, ujue huyo ni dikteta.

 

“Hata Baba wa Taifa kwenye hotuba yake moja alisema kuna mambo ya msingi yeye na wenzake waliyafanya wakati wa uongozi wao, na hayo yanapaswa kuchukuliwa na awamu zinazofuata; lakini yale mabaya waliyoyafanya yanapaswa yaachwe.

 

“Mheshimiwa Kikwete ana udhaifu wake, lakini ana mazuri yake. Kwa muktadha wa leo, tabia anayoonyesha ya uongozi ni nzuri. Akifanya kinyume anaweza kujikuta kila siku anafikishwa mahakamani.

 

“Kinachotakiwa ndani ya CCM na vyama vyote ni kuwa na mfumo wa kukemea na kushughulikia rushwa. Hiyo si kazi ya mtu mmoja, wanapaswa watumie sekretarieti hadi za wilaya. Kinana (Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana) ni dhahabu, lakini yeye kama mtu mmoja hawezi kubadili kitu ndani ya CCM. Kinachotakiwa ni mfumo wa pamoja. Kwa mfano, kwa sasa Chadema iko juu, hayo mazingira ni changamoto kwa CCM. Chadema wamekuwa wakirusha hoja na kuacha CCM wakihangaika kujibu. Sasa naona kinachofanywa na kina Kinana ni kujaribu kujitoa kwenye chama cha kujibu hoja za Chadema, na kuwa chama cha kuibua hoja zinazopaswa kujibiwa na kina Chadema na wengine.

 

“Mukama (aliyekuwa Katibu Mkuu) hakufiti pale kwa sababu ni msema ukweli, yeye anataka kusema ukweli; huo ni mwelekeo tofauti na wa utendaji wa kimkakati ambao anao Kinana. Wameteuliwa juzi na sasa wameanza mkakati, hiyo ndiyo inatakiwa…wasiwe wa kujibu mapigo tu. Wawe waangalifu kwa sababu Chadema wana vijana kama kina Zitto ambaye anarusha kitu, anakaa kando, CCM wanahangaika kujibu. Siasa ndivyo hivyo,” anasema Dk. Bana.

 

Mitandao ya urais

 

Mwenyekiti Kikwete amekemea mitandao ya urais, kwa kile alichosema inahatarisha umoja na mshikamano wa chama, ingawa binafsi anaunga mkono mikakati ya wanachama wanaotaka kuwania nafasi hiyo.

 

Hata hivyo, yeye ndiye mwasisi wa mitandao ya kuusaka urais ndani ya chama hicho, dhambi anayojinasibu kuikemea kwa sasa. Mwaka 2005 aliweka bayana namna alivyoweka mikakati ya kuhakikisha anashinda kiti cha urais baada ya kukikosa mwaka 1995 aliposhindwa na Benjamin Mkapa.

 

Katika mahojiano yake na Tido Mhando wa BBC; alisema hivi:

Tido: Wakati wa uteuzi wa chama, Rais Mkapa alitoa hotuba ambayo wengi walidhani alikuwa anakupigia debe wewe. Je, hili lilikushangaza hata wewe binafsi?

 

Kikwete: Yaani wewe kweli mimi nitashinda kwa hotuba ya jukwaani pale. Ndugu yangu, nilishinda kwa jitihada kubwa ambazo niliziweka mimi na marafiki zangu. Ukweli ni kwamba ilituchukua muda kujijenga. Tulitengeneza mtandao wa watu nchi nzima wa watu wanaotuunga mkono. Tulifanya juhudi kubwa ya kuzungumza na wana-CCM.

 

Tido: Lakini wakati kiongozi mkubwa kabisa, anapokuja mbele ya wajumbe na kutoa matamshi ambayo yanaonyesha dhahiri yanaelekeza kwamba yeye anamuunga mkono fulani, na ilijihidhirisha hata katika mkutano ule pale watu walipoanza heka heka za Kikwete…Kikwete moja kwa moja.

 

Kikwete: Mimi sijui ni kupigiwa debe kwa vipi hasa. Hotuba ya Rais, yeye alichokuwa akizungumza tu ni kwamba… Mimi nadhani hotuba yake ilikuwa inasisitiza kwamba; kwanza alichokisema kwamba moja; CCM kama CCM, tuchague watu, lakini tusisahau huyu tunayemchagua sasa, hatimaye tutampeleka kwa watu. Na huko kwa watu, ni lazima sisi kama chama, kama tunataka kushinda, ni lazima tutambue matarajio ya watu.

 

Kwa sababu haiwezekani muwe mmekaa tu pale kwenye mkutano, mkajifanya kama vile mmefunga masikio, yaani mmeziba masikio, na macho mmeyaziba, hamuoni na wala hamsikii huko mnakotoka wanasema nini.

 

Lakini pia, hata wale wanakuja kwenye Mkutano Mkuu wanatoka katika kila wilaya ya nchi yetu. Ni vizuri kwao wakaangalia matumaini ya watu, na muangalie matumaini ya wale mnaowategemea watakwenda kupiga kura. Sasa, sina hakika kama kwa kusema hivyo alikuwa na maana yangu mimi!

 

Tido: Kulikuwa na vitu vingi pale. Oh, mchague mtu ambaye amekulia kwenye chama hiki, anayekifahamu vizuri sana . Ukiangalia kwa undani, ukilinganisha na wagombea wenzako uliokuwa nao pale, sifa zote hizo zilikuwa zimeiva kwako.

 

Kikwete: Lakini, niseme. Hivi, hivi ni mwana-CCM gani, atateua mtu ambaye hana historia na hicho chama. Hata kama utataka kunilaumu kwa hilo , bado nitaendelea kusema si kweli.

 

Tido: Hapana si kwamba tunakulaumu, lakini tunasema alionyesha wazi kwamba chama kimchague Kikwete.

 

Kikwete: Mimi sijui bwana, sijui. Mimi ningependa kuamini kwamba nilifanya jitihada kubwa kushinda, na wasije wakafika mahali wakarahisisha mitihani niliyoipitia. Nilifanya jitihada kubwa sana .

 

Sisi ni katika wale tunaoamini kwamba mwisho wa uchaguzi mmoja, ni mwanzo wa uchaguzi mwingine. Sisi tulianza mwaka 1995, tukaweka mkakati wa mwaka 2005.Nilifanya kazi kubwa kujenga mtandao. Nilifika mahali, kila mahali ukinitajia Ngara yuko nani, nakwambia yuko fulani. Nikawa nawajua watu kwa majina. Nimefanya kazi kubwa sana . Ndiyo, nakiri kwamba uzoefu wangu nao katika chama ulinirahisishia. Kwamba hawa watu ninawafahamu, nimeshaishi nao, ndiyo msingi ambao mimi ninadhani umesaidia.

 

Lakini wanaodhani nilishinda kwa hotuba ya Rais wanatafuta kurahisisha tu ili ionekane kwamba kama isingekuwa hotuba ile watu wasingenichagua. Hata kidogo! Mimi nilianza zamani. Ninaamini tu kwamba nilifanya jitihada mimi mwenyewe ya kuwaomba wana-CCM waniunge mkono, na ninashukuru walinikubali baada ya kuwaeleza nia yangu ni nini.