Rais Jakaya Kikwete ameusifu utendaji wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC), Nehemia Mchechu, kwamba umerudisha heshima ya shirika hilo.
Ameisifu pia Bodi ya NHC, wafanyakazi wa shirika hilo kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa mkurugenzi huyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa nyumba 290 unaotekelezwa na shirika hilo katika eneo la Kibada Kigamboni, Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Kikwete alishukuru kumpata mtu makini wa kuongoza shirika hilo.
“Ni mbunifu (Mchechu), mchapakazi, amerudisha heshima ya NHC ambayo ilikuwa imepotea na kudharaulika kwa kiasi kikubwa, sasa imerudi katika mstari, kwa kweli ni kiongozi mzuri lakini mgema akisifiwa tembo hulitia maji…,” alisema Rais Kikwete.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa nchi amezitaka taasisi za fedha nchini kutoa mikopo kwa bei nafuu kwani riba ya asilimia 18 ni kubwa na inawafanya walalahoi washindwe kunufaika na huduma hiyo.
“Bila kufanya hivyo watu watatafuta nyumba hapo hapo walipo kwa kuwa aliyepo mahakamani atataka rushwa hospitali, naye atauza dawa na wa Dawasco naye ataka rushwa Tanesco pia ataunganisha umeme bila idhini ya shirika, tutazalisha vishoka wengi.
“Wizara, Benki Kuu na taasisi za fedha zikae na kuhakikisha hilo linafanyika, hiyo itaondoa watu kufikiria rushwa katika maeneo yao ya kazi ili kupata fedha za kufanyia maendeleo yao.
“Siridhiki na kasi ya benki na sidhani kama zinakopesha watu wa chini na ndiyo maana watu hawajui na hawakopi huko. Mikopo ndiyo itakayowasaidia watu kumiliki nyumba,” alisema.
Amesema ni muhimu wizara ikaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi kwa watu wote ikiwa ni pamoja na ununuzi wa viwanja ili watu waweze kujenga.
Rais Kikwete aliipatia NHC changamoto ya kufikiria kuanzisha taasisi yake ya fedha iweze kuwakopesha wateja wa nyumba zake na pia kulikopesha shirika hilo.
“Anzisheni muweze kukopa kwenye taasisi yenu, hiyo itasaidia katika kufanikisha mambo, mtapunguzaa riba na wengine watajifunza kwenu,” alisema Kikwete.
Awali, Mchechu alisema nyumba hizo 290 kila moja itaunzwa kati ya Sh milioni 45 na Sh milioni 52. Hata hivyo, alisema shirika hilo linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya kununua ardhi kwa gharama kubwa.
“Pia kutengeneza miundombinu ya eneo la miradi yetu nayo ni gharama kubwa wakati ni kitu ambacho kilitakiwa kifanywe na mamlaka nyingine,” aliongeza.
Aliiomba Serikali kuondoa kodi kwenye mauzo ya nyumba zenye thamani isiyozidi Sh milioni 100 kusaidia watu wengi kuzinunua kwa gharama ndogo. Hata hivyo, Rais Kikwete alisema hawezi kuruhusu kodi kuondolewa kwenye mauzo hayo, ila atawezesha kupunguzwa kwa kodi hiyo.
“Mimi kwenye hilo la kufuta sipo ila kwenye kupunguza tunaweza tukafanya hivyo kwa kujadiliana na mamlaka husika kwa kuwa kodi ndiyo inayoiendesha Serikali yetu,” alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo pia kuzionya halmashauri nchini kuacha kufanya ardhi kuwa ni chanzo cha mapato kwa kuuza kwa bei ghali, kwani tabia hiyo itasababisha wananchi washindwe kuinunua.
“Halmashauri zisigeuze ardhi kuwa chanzo cha mapato, hiyo ni mbaya sana na hatutafika pazuri, kwani watu watashindwa kununua ardhi,” alisisitiza.