Je, unamfahamu mnyama duma (Cheetah)? Wengi wanajua tu kwamba ni kati ya wanyama wenye kasi sana.
Duma anakimbia zaidi ya maili 60 kwa saa, lakini wengi wasichokijua kuhusu mnyama huyu ni uwezo wake mkubwa wa kubadili uelekeo kinyume na alikokuwa anakimbilia kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo. Hapa amewashinda wanyama wengine wote.
Wengi wetu tuna kasi sana ya maisha, kasi ya kutafuta ajira, kasi ya mahusiano, kasi ya kutafuta elimu nzuri, kasi ya kuzisaka fursa na kwingineko kwingi. Swali ni: Je, endapo kunatokea mabadiliko ya ghafla kwenye eneo fulani maishani mwako, una uwezo kiasi gani wa kubadili kasi yako ili uendelee kukimbia kwenye uelekeo mwingine?
Au ndiyo uelekeo ukibadilika na wewe unalala chali na kuanza kulalamika? Amua kubadilika. Kila asubuhi jiambie: “Nataka kuwa kama duma.”
Kila asubuhi unapoamka, amka na wazo jipya. Kila asubuhi weka malengo kwenye vipaumbele vyako.
“Kila asubuhi ninaisikia sauti ya ushindi ndani ya akili yangu. Na moyo wangu unaniambia: Utafanikiwa” aliandika mtu fulani.
Jifunze jambo kutoka kwa Jessica Cox. Jessica Cox ni rubani mwanamke asiye na mikono. Jessica Cox ni mwanamke Mmarekani aliyezaliwa mwaka 1983 bila mikono, lakini ndiye mwanamke wa kwanza duniani kupata leseni ya kurusha ndege.
Huyu ni mwanamke anayeongoza ndege kwa kutumia miguu yake. Jessica Cox katika kitabu chake cha “Disarm Your Limits” anasema: “Kila asubuhi ninaamka nikiwa nimejaa roho ya ushindi katika maisha yangu.”
Kila asubuhi jiamini kabla hujaaminiwa. Kila asubuhi jijenge kabla hujajengwa. Kila asubuhi jitambue kabla hujatambuliwa.
Kila asubuhi jipende kabla hujapendwa. Jessica Cox aliamini kwamba anaweza kuwa rubani licha ya kwamba hana mikono.
Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo inayokufanya usijiamini. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya uvivu. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya laana. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya umaskini.
Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya kukawia kufanikiwa. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya kukataliwa na kujikataa. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya kutangatanga. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya sauti za kushindwa. Kila asubuhi unapoamka vunja minyororo ya hofu.
Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia watu wengine wakifanikiwa huku yeye akiwa anakumbatiwa na umaskini.
Kila mtu ana fungu lake. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki, nafasi, uwezo na uchaguzi wa kufanikiwa.
Ahadi ina nguvu. Ahadi ni muujiza. Kila asubuhi jitahidi kufanya jambo fulani. Jiahidi kwamba utafanikiwa. Jiahidi kwamba utakuwa mtakatifu. Jiahidi kwamba utakuwa mfanyabiashara mkubwa. Jiahidi kwamba utakuwa mwanandoa mwaminifu.
Jiahidi kwamba utakuwa mtii kwa Muumba wako. Jiahidi kwamba utakuwa kiongozi bora. Jiahidi kwamba utakuwa bilionea. Amini! Amini! Amini!
Kila asubuhi amka na moyo wa uthubutu. Mhamasishaji, Les Brown anasema: “Ili uwe mtu ambaye haujawahi kuwa ni lazima ufanye mambo ambayo hujawahi kufanya.”
Woga hauna mtaji lakini uthubutu una mtaji. Ukiogopa hauwezi kufanya chochote, lakini ukithubutu utafanya chochote. Kuna muujiza mkubwa umejificha ndani ya kile unachoogopa kukifanya.
Kila asubuhi, piga hatua. Mwandishi wa insha na mashairi wa Marekani, Ralpha Waldo Emerson anasema: “Maisha ni hatua, si kituo.” Maisha yana thamani kama unapiga hatua. Umri wako wa kutambaa umepita. Piga hatua.
Kila asubuhi jiulize maswali. Jiulize maswali ya mafanikio. Unapotaka kufanikiwa usiogope kuuliza maswali.
Maswali ni nusu ya majibu. Unapojiuliza swali unakuwa uko karibu kupata jibu la swali unalojiuliza.
Mjasiriamali na mtunzi wa vitabu, Robert Kiyosaki, anasema: “Watu waliofanikiwa sana katika maisha ni wale ambao huuliza maswali. Kila mara wanajifunza. Kila mara wanakua. Kila mara wanasukuma mambo.” Unapojiuliza huwa unataka kupata majibu. Mwandishi wa Marekani, Tony Robbins, anasema: “Watu waliofanikiwa wanauliza maswali zaidi na matokeo yake wanapata majibu mazuri zaidi.”
Kila asubuhi uliza maswali na jiulize maswali.