Unapoamka asubuhi kutoka kitandani unajiuliza swali gani?
Unapomsikia jogoo akiwika alfajiri unajiuliza nini? Je, kila asubuhi unajiuliza kuhusu hatima ya maisha yako?
Kila asubuhi imebeba ujumbe wa maisha yako. Kila asubuhi Mungu anakuambia: “Nimekuamsha salama mwanangu mpendwa. Ninakupenda sana. Fanya kazi kwa bidii.”
Kila asubuhi imebeba mafanikio yako. Mwandishi wa kale aitwaye Anon anasema: “Kila asubuhi unakabidhiwa saa 24 za dhahabu.” Kila kunapokucha kila mtu anapokea bure zawadi ya siku mpya.
Hatupokei zawadi hiyo kwa sababu sisi ni watu wema kuliko wengine ambao hawajafanikiwa kuiona asubuhi tuliyoiona sisi. HAPANA.
Kila asubuhi tunayoipokea ina malengo na makusudio maalumu katika maisha yetu. Tuitumie kila asubuhi tunayokutana nayo kama fursa ya kubadilika kimaono, kiupendo, kiuchumi, kiimani na kiafya.
Aliyekuwa mkurugenzi wa Apple, Steve Jobs, wakati akizungumza na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Stanford mwaka 2005 alisema: “Kila nikiamka asubuhi huwa ninajiuliza: Kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho kuishi duniani, je, ningefanya ambacho ninataka kukifanya leo? Je, ningeishi kama ambavyo ninataka kuishi leo? Na kama jibu langu lingekuwa HAPANA, basi hapo ningejua kuwa kuna kitu ninatakiwa kukibadilisha.”
Martin Luther, kwa upande wake alisema: “Hata kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho bado ningefanya kazi ambayo ingezaa matunda kwa ajili yangu au kwa anayekuja nyuma yangu.”
Je, kwa upande wako kama leo ndiyo ingekuwa asubuhi yako ya mwisho ya kuishi hapa duniani ungefanya nini?
Kila asubuhi kimbia. Kila asubuhi ni lazima uwe na mbio za kuyatafuta mafanikio yako yalikojificha.
Mtu mmoja alisema: “Kila asubuhi swala huamka akijua wazi kuwa lazima awe na kasi zaidi kuliko simba ili asiliwe. Lakini pia kila asubuhi, simba huamka akijua wazi kwamba lazima awe na kasi kuliko swala ili asilale njaa.” Kimbia kwa kasi kama swala ili usiliwe na simba. Kimbia kwa kasi kama simba ili usishinde njaa.
Bila kujali kama wewe ni simba au swala, ni lazima kila asubuhi uwe na kasi ya kuyatafuta mafanikio unayoyataka.
Kila asubuhi unatakiwa kuamka na moyo uliojaa roho ya ushindi. Kila asubuhi ni lazima ujione kama mshindi. Kila asubuhi ni lazima upige hatua 99 za kuyasogelea mafanikio yako. Asubuhi ya leo ndiyo itakayoibadilisha asubuhi ya kesho yako.
Je, unafahamu siri ya asubuhi? Asubuhi ni siku nyingine. Kila asubuhi unakabidhiwa kalenda ya maisha yako. Kila asubuhi umri wako unaongezeka. Kila asubuhi unakumbushwa kuzitubu dhambi zako. Kila asubuhi unakumbushwa kuiombea kazi yako. Kila asubuhi unakumbushwa kumwombea mke/mume wako, watoto, marafiki na majirani zako.
Yule mwandishi wa kale aitwaye Tecumseh (1768-1813) anasema: “Unapoamka asubuhi toa shukrani kwa ajili ya uhai wako na nguvu. Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha yako ya kuishi. Kama huoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako.”
Kila asubuhi, kila mwenye pumzi hupokea muda wa saa 24 bure. Hakuna anayepokea zaidi. Kila mtu hupokea kwa haki kabisa. Kila mtu hupokea kwa kiwango sawa na hukitumia kadiri anavyotaka. Mwandishi H. Jackson Brown Jr katika makala yake ya ‘Time Management’, anasema: “Usiseme hauna muda wa kutosha. Unayo idadi sawa kabisa ya saa kwa siku ambazo zilitolewa kwa Hellen Keller, Pasteur, Michelangelo, Mama Tereza, Leonardo da Vinci, Thomas Jefferson na Albert Einstein.”
Je, unamfahamu mnyama duma (Cheetah)? Wengi wanajua tu kwamba ni kati ya wanyama wenye kasi sana.
Duma anakimbia zaidi ya maili 60 kwa saa, lakini wengi wasichokijua kuhusu mnyama huyu ni uwezo wake mkubwa wa kubadili uelekeo kinyume na alikokuwa anakimbilia kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo. Hapa amewashinda wanyama wengine wote.
Wengi wetu tuna kasi sana ya maisha, kasi ya kutafuta ajira, kasi ya mahusiano, kasi ya kutafuta elimu nzuri, kasi ya kuzisaka fursa na kwingineko kwingi. Swali ni: Je, endapo kunatokea mabadiliko ya ghafla kwenye eneo fulani maishani mwako, una uwezo kiasi gani wa kubadili kasi yako ili uendelee kukimbia kwenye uelekeo mwingine?
Au ndiyo uelekeo ukibadilika na wewe unalala chali na kuanza kulalamika? Amua kubadilika. Kila asubuhi jiambie: “Nataka kuwa kama duma.”