“Kama unafikiri wewe ni mdogo kiasi cha kuleta tofauti, haujawahi kukesha usiku kucha ukiwa na mbu,” ni methali ya Kiafrika.
Mbu ni viumbe wadogo sana, lakini wakati wa usiku tukiwa tumelala huwa wanafanya maajabu makubwa. Unaweza kuwa umelala na haujashusha chandarua ukafyonzwa damu na mbu mmoja, ukiamka unajikuta umevimba usoni, mikononi, miguuni na hata mwili mzima na unaweza kufikiri kulikuwa na jeshi la mbu chumbani kwako, kumbe ni mbu mmoja tu.
Mbu huyo huyo anaweza kukuambukiza malaria ambao ni ugonjwa unaoua watu wengi duniani kila siku hasa watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka mitano. Shirika la Afya Duniani (WHO) liliripoti kuwa takriban watoto 303,000 wa Kiafrika chini ya miaka mitano waliaga dunia mwaka 2015. Pia watu milioni 212 walikutwa na maambukizi ya malaria, huku vifo 429,000 vikitokea.
Kama mbu ambaye ni mdudu mdogo anaweza kufanya mambo haya, kwa nini wewe ushindwe kufanya kitu cha tofauti? Methali hii ya Kiafrika niliyoanza nayo hapo juu inatukumbusha kwamba kila mtu anaweza kufanya kitu cha tofauti na kikaleta mchango mkubwa katika jamii. “Usiogope kung’ata vitu vikubwa, jifunze kwa mbu,” alisema Bangambiki Habyarimana.
Usijidharau na kusema mimi ni mdogo au umri umekwenda. Umri wako kuwa mdogo hiyo ni fursa ya kuanza mapema, lakini umri wako kuwa mkubwa si hoja ya wewe kutokuwa na uwezo wa kufanya kitu kitakacholeta tofauti katika jamii inayokuzunguka na taifa kwa ujumla.
Colonel Sanders alianzisha KFC (Kentucky Fried Chicken), mgahawa wa kuuza kuku waliokaangwa akiwa na miaka 66, baada ya kushinda jaribio la kujinyonga akiwa na umri wa miaka 65; muda ambao alikuwa amekata tamaa na hana hamu tena ya kuendelea kuishi.
Akiwa na umri wa miaka 88, KFC ilimfanya awe bilionea. Leo hii KFC ipo zaidi ya nchi 180 duniani, ikiwa na vituo 19,952. Vituo 4,563 kati ya hivyo vikiwa nchini China (kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia).
Lakini pia, ukisema wewe bado ni mdogo kufanya kitu fulani, hivyo ni visingizio na havitakupeleka kokote. Niliandika kitabu changu cha kwanza kinachoitwa ‘Barabara ya Mafanikio’ nikiwa na umri wa miaka 20. Siku zote huwa nasema: “Maisha huanza ukiwa na miaka 20.”
Kama mimi niliweza, wewe unaweza pia. Kuanza mapema katika umri mdogo ni fursa kubwa kwani utajua mambo mengi mapema, utakosea sana na kujifunza mambo mengi, hivyo utatanuka kifikra na kiutendaji, utaweza kufanya mambo makubwa, kwa weledi mkubwa.
“Kabla ya miaka 25, fanya makosa mengi kadiri uwezavyo,” anasema Jack Ma. “Huwezi kufanya kitu kile kile kwa njia ile ile na kutarajia kitu cha tofauti kutokea,” anakumbusha Beth Moore.
Kila mtu ana kitu cha tofauti alichozaliwa nacho na anadaiwa kukileta dunia na kukifanyia kazi. Mimi na wewe tunalo jukumu hilo. Kuna vitu ambavyo umezaliwa navyo ambavyo unavyo wewe peke yako. Mimi na jirani yako hatuna.
Sauti yako ni ya kipekee. Hakuna mtu mwenye sauti kama yako. Macho yako ni ya kipekee, dunia nzima hakuna mtu mwenye macho kama yako. Hivyo unaweza kuona fursa ambazo mimi na wenzangu hatuzioni.
Alama zako za vidole hazifanani na za mtu mwingine yeyote. Kama huamini nenda kaulize polisi. Jambo la kushangaza zaidi, katika mamilioni ya watu waliowahi kuishi na wanaoendelea kuishi leo hii, hakuna hata mmoja mwenye mapigo ya moyo kama yako. Wewe ni wa kipekee. Wewe ni wa tofauti, hivyo unaweza kufanya kitu cha tofauti.
Wewe ni wa tofauti, hivyo tunatarajia utuletee kitu cha tofauti na cha kipekee. Na dunia siku zote inawapokea kwa mikono miwili watu wanaofanya vitu vya kipekee. Nakubaliana na mwanafalsafa na mhamasishaji, Jim Rohn, aliyewahi kusema: “Wewe ni maskini kwa sababu watu hawajui lolote kuhusu wewe.”
Kama watu wakijua kwamba vitu ulivyonavyo ni vya kipekee na wewe umekuwa tayari kuvitoa na kuvionyesha mbele yao, lazima watakulipa, hauwezi siku zote kukosa pesa mfukoni.